Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Pereira Ame
Silima, amesema moja ya mambo ambayo hayakufanyika vizuri
mwanzoni wakati wa uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa ni kutovifanya
vitumike kupiga kura katika uchaguzi mkuu.
Amesema kama kitambulisho hicho kingeboreshwa kingeweza kutumika
kwa ajili ya kupiga kura, hivyo kusingekuwapo uandikishaji wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura.
Waziri huyo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa
ufunguzi wa kongamano la kimataifa la uandikishaji wa vitambulisho vya
Taifa lijulikanalo kama ‘Govetnment Forum on Electronic Identity in
Africa', unaofanyika Afrika kwa mara ya kwanza na kujumuisha wataalam
zaidi ya 300 wa ndani na nje ya Afrika.
“Kama tungejipanga mwanzo vizuri ni wazi kusingekuwapo haja ya
mchakato unaoendelea wa kuandikisha kwa kutumia BVR, ni nafasi kwetu
kujifunza na kujirekebisha na pia watajifunza kutoka Tanzania,” alisema.
Silima alisema siku zijazo vitambulisho hivyo vitaboresha zaidi ili
kutumika kwenye maeneo mbalimbali, na kwamba kwa siku za usoni
vitatumika kwenye malipo mbalimbali. Aliwataka Watanzania wanaoshiriki katika kongamano hilo kupokea na
kutumia teknolojia inayotoka kwenye makampuni mbalimbali duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida),
Dickson Maimu, alisema watu milioni 6.1 wameandikishwa katika maeneo ya
Zanzibar, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro na Tanga na
kwamba watu milioni 2.5 wamepatiwa vitambulisho.
Alisema kongamano hilo linalojulikana ‘Govetnment Forum on
Electronic Identity in Africa’, limeleta pamoja nchi 24 ambazo
zitajadili kwa kina changamoto zilizopo kwenye uandikishaji, uandaaji wa
vitambulisho vya Taifa na jinsi gani vitatumika kwa maendeleo ya Taifa.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment