Wafuasi wa Chadema wa mjini Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, wakiwa katika
maandamano ya kumsindikiza Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Dk Wilbroad
Slaa baada ya kumaliza kuhutubia mkutano uliofanyika katika Viwanja vya
Shule ya Msingi Ndua mkoani humo.
Viongozi wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameponda tabia ya
makada wa CCM wanaotangaza nia ya kugombea urais kufanya hafla
zinazotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo.
Viongozi hao wamesema vitendo hivyo vinaonyesha
kuwa chama hicho tawala hakichukii ufisadi na hivyo hakiwezi kuwa na
mgombea safi.
Makada hao wamelipia muda wa matangazo ya moja kwa
moja kwenye vituo vya redio na televisheni, kufanya maandalilizi ya
gharama kubwa kwenye sehemu walizotangazia nia, kuandaa vipeperushi na
mabango ya thamani huku baadhi wakituhumiwa kusafirisha watu kutoka
sehemu mbalimbali kuhudhuria hafla hizo. Akihutubia wakazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa,
katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema Serikali ya CCM ni kama
ya watu wa ukoo mmoja wenye tabia zinazofanana.
Alisema Serikali imejaa tuhuma nyingi za rushwa na
ufisadi na kwamba, kinachotakiwa ni kuinyima kura zote wakati wa
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Katibu huyo alisema wale wote wanaojitokeza
kutangaza nia ni ‘mafisadi’ ndio maana wanatumia nguvu ya fedha
kuwanunua Watanzania, jambo ambalo alisema ni kinyume cha maadili. “Ni hatari sana kuwachagua viongozi kwa fedha, hawa wanataka kuliangamiza Taifa,” alisema.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
anashangaa chama kilichoasisiwa na mjamaa Mwalimu Julius Nyerere,
vijana wake wanafanya sherehe kubwa kwenye jambo dogo. “Hata mwanasiasa mkongwe Kingunge (ngombare Mwiru)
anakwenda kuwa mpambe kwenye shughuli inayokiuka taratibu,” alisema na
kuongeza kuwa hiyo ni ishara mbaya.
Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi alihoji wanaotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo, watazirudishaje. Alisema kama makada hao walifanya kazi halali, hawawezi kuwa na fedha zinazoweza kugharimia sherehe kubwa kama hizo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mfumo mbaya wa CCM ndio unaonyesha chama hicho hakichukii mafisadi. “Kama chama kingekuwa kinachukia ufisadi, kingeandaa utaratibu wake ili
watu wote wanaotangaza nia wawe na nguvu sawa,” alisema Mbatia.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment