Social Icons

Pages

Wednesday, June 03, 2015

SUMAYE: NIMEJIPIMA NIKAONA NINATOSHA URAIS

Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akiwa na mkewe Esther pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Ubungo, Charles Keenja akielekea katika mkutano wake wa kutangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM,  Dar es Salaam jana.
Waziri Mkuu  wa zamani, Frederick Sumaye ametangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM, huku akibainisha kuwa amejipima, ametafakari na kujiridhisha kuwa anatosha kushika wadhifa huo wa juu nchini.
“Kama kuna mtu mwingine amekamilika kuliko mimi niambieni na nitampisha (katika mbio za urais),” alisema Sumaye wakati akitatangaza nia hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari, akitumia takriban saa moja na nusu kueleza sifa za Rais ajaye na vipaumbele vyake.
Sumaye, mmoja wa makada sita waliokuwa wamefungiwa na CCM kwa kukiuka taratibu za kampeni, alikuwa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kipindi chote cha miaka kumi na pia alikuwa mbunge wa Hanang hadi alipoamua kutogombea nafasi hiyo mwaka 2010.
Waziri huyo mkuu wa zamani amekuja na kauli mbiu ya Uongozi Bora: Komesha Rushwa, Jenga Uchumi, huku akibainisha vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kujenga na kuimarisha uchumi.
Vipaumbele vingine ni kulinda Muungano, mshikamano, amani na utulivu na kuboresha huduma za kijamii na maisha ya Watanzania, kupambana na maovu ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya, mauaji ya kishirikina, uhusiano wa kimataifa na masuala muhimu ya uhifadhi wa mazingira, kilimo, ajira, ulinzi wa rasilimani na michezo na utamaduni.
Sumaye alisema Watanzania wanataka Rais anayetambua uzito wa kazi iliyopo mbele yake na wananchi wote na awe tayari kuwa Jemedari wa Jeshi hilo ili kupata ufumbuzi wa matatizo yao yanayowakabili.
Alisema wananchi wengi wanamfahamu kwa utendaji wake naye anajua wanachokihitaji na sifa za Rais wanayemhitaji, hivyo yeye ndiye anayefaa kwa nafasi hiyo. “Mtu anayetaka kuwa Rais ni lazima awe tayari kujipima, kutafakari, ajiridhishe, kuwa anatosha kiafya, kiakili, kimaadili na kidhamira kuwaongoza Watanzania. “Kama kuna mtu anapungukiwa kimojawapo, hana sifa za kuwaongoza Watanzania,” alisema Sumaye huku akishangiliwa na baadhi ya wafuasi waliomsindikiza katika mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Hyatt Regency.
Alisema kiongozi huyo awe tayari kupimwa na umma vigezo hivyo na siyo ajipime na kwamba yeye yupo tayari kupimwa na umma. Katika hotuba yake hiyo iliyokuwa ikirushwa na baadhi ya televisheni na redio nchini, alisema Watanzania wanahitaji Rais atakayekuwa mtumishi wa kuwaongoza na siyo bosi, na pia awe mtu atakayewaongoza kwa uadilifu.
Sifa nyingine za kiongozi huyo ni kuwa mzalendo wa dhati anayejua Watanzania walipotoka, wanapopitia na wanakoelekea; mwaminifu, mjasiri, mtiifu wa sheria na katiba na anayeheshimu mipaka ya cheo chake. “Tunamtaka Rais mwenye msimamo na anayekubali kushauriwa, aliye tayari kutengeneza Serikali inayowajibika kwa umma na atakayelinda masilahi ya umma na siyo masilahi yake na rafiki zake,” alisema Sumaye. Mbunge huyo wa zamani wa Hanang, alisema Rais anatakiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia na kukuza uchumi nchini kwa kuondoa matabaka kati ya walionacho na wasionacho.
Aliongeza kuwa Rais ajaye anatakiwa kutoa huduma stahiki za jamii kwa kuondoa matabaka katika kupata elimu na afya bora.

Kwa nini katangazia Dar?
Awali akianza hotuba yake, Sumaye aliyewahi kugombea urais mwaka 2005 wakati Jakaya Kikwete aliposhinda na baadaye kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, alisema ameamua kutangazia nia yake jijini Dar es Salaam kwa sababu anataka kura za wananchi wote siyo tu wananchi wa maeneo ambako anatokea kama wanavyofanya watangazania wengine.
“Sitaki watu wa Hanang’ wanipe kura kwa sababu mimi ni wa kwao au wa Musoma waninyime kura waseme huyo siyo wa kwetu, mimi ni wa Tanzania nzima na kazi hii ni ya Watanzania wote. Nimetangazia Dar es Salaam kwa kuwa ni mji mkuu kwa maana ya majiji,” alisema.
Sumaye alisema ana uzoefu wa kutosha katika nafasi mbalimbali za uongozi wa kisiasa na kiserikali kwa kuwa mbunge, naibu waziri na hatimaye Waziri Mkuu kwa miaka kumi katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa. Alitumia muda huo kubainisha mafanikio mbalimbali waliyoyapata akiwa Waziri Mkuu, yakiwamo ya kupunguza mfumuko wa bei kutoka asilimia 27 hadi asilimia 4.1 na kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Sh27 bilioni kwa mwezi hadi Sh200 bilioni.
Alisema walipambana kwa hali na mali kuondoa vitendo vya rushwa kwa kuanza na kuunda tume za kupambana na rushwa na kuanzishwa utaratibu wa wananchi wa kupiga Kura ya Maoni kwa watu wanaowahisi ni wala rushwa, jambo lilisababisha watumishi wengi wa Serikali wasimamishwe au kustaafishwa kwa maslahi ya umma.
 Sumaye, ambaye katika hotuba yake alikuwa akikemea rushwa mara kwa mara, alisema yeye ni mwadilifu asiyehusishwa na tuhuma zozote za kifisadi tofauti na wanasiasa wengine wanaokemea ufisadi bila kuonyesha kwa vitendo. “Leo unasikia mgombea anasema hatutaki kiongozi masikini. Unaomba urais kwa Watanzania masikini halafu unasema hatutaki kiongozi masikini… hakutaka tu kusema tunataka kiongozi tajiri,” alisema.
“Unasema mimi siyo tajiri lakini unatafuta nafasi ya kwenda Ikulu utafikiri utajiri unapatikana huko. Kama unataka utajiri nenda kafungue kampuni ufanye biashara na kukimbizana na polisi,” alisema Sumaye bila kumtaja mgombea aliyekuwa akimzungumzia.
Alisema akipata ridhaa ya kuwa Rais, atapambana na maovu ya ufisadi na rushwa kwa kuunda chombo maalumu kitakachokuwa kikifanya uchunguzi wa rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi. “Chombo hiki kitachunguza kwa wiki na baadaye kukufikisha mahakamani. Baada ya wiki moja au mbili unahukumiwa, kama ni viboko au kwenda jela,” alisema Sumaye.
Akielezea kwa undani vipaumbele vyake, Sumaye alisema atatekeleza ilani ya CCM kikamilifu na kuhakikisha anasimamia ukuzaji wa uchumi kwa kuwa ndiyo msingi wa mafanikio wa kila nyanja ya maisha ya mwanadamu. Alisema uchumi umekuwa ukikua kwa namba, lakini hauwagusi watu wa vijijini ambao ni masikini wa kutupwa, hivyo yeye atahakikisha unauimarisha katika maeneo yote ya vijijini na mijini kwa kuimarisha kilimo na viwanda. Sumaye alisema huwezi kuboresha afya na elimu bila kuwa na msingi imara wa kupata mapato stahiki na mgawanyo mzuri wa rasilimali kwa Watanzania wote.
Waziri huyo wa zamani wa Kilimo na Mifugo alisema atahakikisha mfumo mzima wa kilimo unaimarika na siyo kuimarisha sehemu moja ya kuleta matrekta nchini wakati huduma zinazochangia uzalishaji kama mbegu, utafiti, mfumo mzuri wa utunzaji mazao zinazorota.
“Siyo kama nakosoa kuhusu matrekta kwa sababu hata wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere yalikuwepo, lakini hayakufanya kazi kiufanisi. Unaweza ukawa na trekta likalima ekari 50, lakini una uwezo wa mbegu za ekari tatu, kupalilia na kuhifadhi mazao kwa kiwango hicho. Ila mimi nikipata ridhaa nitaboresha hayo na kutafuta masoko ya uhakika,” alisema huku akishangiliwa. Pia, alibainisha kuwa atahakikisha anakuza na kulinda viwanda vya ndani ili kuzuia Tanzania kuwa dampo la bidhaa za nje zisizohitajika. “Ni muhimu kuendeleza viwanda ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa ajili ya matumizi ya ndani na bidhaa za kuuza nje ya nchi ili kuongeza utajiri kwa fedha za kigeni,” alisema.
Kuhusu suala la ajira, Sumaye alisema atahakikisha anatoa elimu bora ya ufundi katika ngazi za chini hasa kwa kuweka mikondo ya ufundi katika shule za kata na pia kuongeza uwekezaji katika viwanda vidogo vya kuongeza mazao ya kilimo na kuwekeza katika kilimo kutaondoa tatizo la vijana kutokuwa na kazi.
“Mfumo wetu unawaandaa vijana kuendelea na elimu ya juu badala kuwawezesha kuwa na uwezo wa kumudu changamoto za maisha kwa kila hatua ya kielimu anayoifikia mwanafunzi. Hivyo uzalishaji wa madarasa ya ufundi katika shule zetu utakuwa muhimu ili vijana kujiajiri,” alisema.
Kuhusu huduma za jamii alisema kipaumbele chake ni kuweka elimu bora kwa watu wote kwa kuhakikisha anatafuta rasilimali za kutosha zitakazosaidia kuondoa mwanya wa walichonacho na wasionacho. “Tunataka shule nzuri za Serikali ambazo zitachukua vijana wenye akili kutoka vijijini ili waweze kusoma bila kujitofautisha na shule binafsi, hospitali nzuri ambazo Watanzania wanaweza kupata huduma bora muda wote…mtu akishindwa kutibiwa Aga Khan basi akienda Mwananyamala atibiwe bila kuona tofauti,” alieleza.
Sumaye alitumia pia mkutano huo kupangua tuhuma mbalimbali za kashfa dhidi yake na utawala wake, zikiwemo ununuzi wa rada, ubinafsishaji wa nyumba za serikali, umiliki wa ardhi, uuzwaji wa benki ya NBC, ununuzi wa mgodi wa makaa ya mawe ya Kiwira na sakata la Meremeta.
Kuhusu masuala hayo, alisema Watanzania wanapaswa kutofautisha uamuzi wa serikali na wizi na sehemu kubwa ya mambo hayo yalikuwa ni uamuzi wa Serikali na chama, hasa sera ya ubinafsishaji.
“Nilishawahi kuyatolea maelezo yote haya. Suala la rada lilikuwa muhimu sana. Ukumbuke nchi ilikuwa haina chombo cha kuongozea ndege…ilikuwa ni hatari kwa usalama wa nchi na sekta ya anga,” alisema Sumaye akizungumzia suala hilo la ununuzi wa rada kwa bei ya juu kulinganisha nay a sokoni. “Mashirika makubwa ya ndege yalishaanza kukataakutua nchini. Hata jeshi halikuwa na rada. Hali ilikuwa mbaya. Suala la ununuzi lilihusisha wataalamu hata mimi sikuiona inafananaje na hata Mzee Mkapa haijui ikoje. “Kama mtu aliiba ni jambo jingine. Kama mtu amebainika aliiba, Serikali imchukulie hatua.”
Katika sakata hilo, Bunge la Uingereza lilihoji sababu za nchi maskini kama Tanzania kununua rada kwa bei kubwa na baadaye kuagiza uchunguzi ambao ulibaini kuwapo ufisadi wa kupandisha bei kwa hila. Iliagizwa fedha hizo zirejeshwe nchini.

Asisitiza dhamira ya kuihama CCM
Alipoulizwa iwapo ataendelea na msimamo wake wa kukihama chama hicho kama ambavyo amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari kwamba kama CCM itamteua mgombea mla rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Sumaye alisema “hawezi kushirikiana na wala rushwa”. “Nitatoka CCM, ndiyo…kama huwezi kuungana nao utabakiaje? Ila naamini chama changu hakitamchagua mla rushwa na ndiyo maana sitegemei kutoka kwa sababu hawatachagua mla rushwa,” alisema.
Kuhusu ubinafsishaji wa mashirika ya umma ambao ni moja ya masuala ambayo Serikali yake na rais Mkapa ilinyooshewa vidole, Sumaye alisema alikuta sera zilizopitishwa na CCM na Serikali, hivyo hatakiwi kulaumiwa kwa kutekeleza yalikuyokubaliwa na mfumo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: