
Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo, akitangaza nia ya kuwania
urais kupitia CCM katika mkutano uliofanyika Mjini Musoma jana.
Mbunge wa
kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo ameeleza jinsi atakavyoondoa
umaskini nchini kwa kutumia uchumi wa gesi endapo atapitishwa na Chama
cha Mapinduzi (CCM), kuwania urais.
Akitangaza nia ya kuwania nafasi hiyo mjini Musoma
jana, Profesa alisema: “Nitafuta umaskini kwa kutumia uchumi wa gesi
ambao utakuwa unamilikiwa na Watanzania wenyewe… gesi nimesomea kwa hiyo
ninafahamu mambo haya vizuri.
“Tena kutokana na juhudi zangu za kuhamasisha
vijana wapelekwe nje kusoma masomo ya gesi, nategemea mwakani tutakuwa
na wataalamu wengi zaidi watakaoweza kufanya kazi kwenye sekta hii.
Lakini pia hata baadhi ya vyuo vikuu nchini kama Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na Dodoma vimeanzisha shahada za masuala ya gesi kwa hiyo kadri
tunavyoendelea, tutakuwa na wataalamu wa kutosha.”
Profesa Muhungo aliyekuwa ameongozana na mkewe,
Bertha Mamuya alisema ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, kutakuwa na
mfuko maalumu kwa ajili ya kutunza fedha za gesi... “Matumizi ya mapato
ya gesi yatakuwaje?” alihoji na kuendelea kutoa ufafanuzi wake kwa
makini.
“Mapato ya gesi hayatakwenda Hazina. Tutafungua
mfuko maalumu kwa ajili ya kutunza fedha hizo. Kama ikitokea kiasi
fulani kinahitajika kwa ajili ya matumizi fedha zitakuwa hazitoki
hivihivi tu.
“Kila mwaka Bunge litakuwa linajadili tutoe kiasi
gani kwenye mfuko ili kiweze kusaidia kwenye matumizi hayo. Lakini kabla
ya kutolewa, pia kwenye mfuko huo nitakaouanzisha, kwa mara ya kwanza,
lazima ridhaa hiyo itoke kwa Watanzania wenyewe.”
Profesa Muhongo ambaye alitumia kaulimbiu ya
‘Tukuze uchumi, tuondoe umasikini’, alisema: “Mfuko huo kwa mara ya
kwanza utatumika kutoa mikopo nafuu ya riba ndogo kwa Watanzania
wanaofanya shughuli zao kwenye sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji na
michezo. Watakuwa wanapata mkopo wa riba ya asilimia mbili… haya yote
yatakuwa yanapitishwa na wabunge kwa ridhaa ya wananchi.
“Tutatunga sheria kwa ajili ya kusimamia mipango
yote hii tutageuza uchumi wetu kupitia uvuvi, kilimo, michezo na
ufugaji kutoka asilimia saba hadi asilimia15 ifikapo 2025.” Profesa
Muhongo alisema uchumi wa gesi utaongeza uzalishaji wa umeme zaidi
tofauti na unaozalishwa sasa kwa ajili ya matumizi ya viwanda na
majumbani ambao ni Megawati 1,500 tu. “Gesi itasaidia kuongeza uzalishaji wa umeme utakaokuwa unatumika viwandani. Uzalishaji huo utaongeza ajira kwa vijana pia.”
Mbali na gesi, katika hotuba yake ya saa 1.05,
Profesa Muhongo alisema, amefanya utafiti katika maeneo mbalimbali na
kubaini kuwa Tanzania bado ina hazina kubwa ya madini ambayo
hayajachimbwa. “Nafahamu sidhani kama kuna mtu mwingine
anafahamu kama mimi. Mkinipa ridhaa yenu wanaCCM, nitahakikisha
tunatumia vyema fursa hizo kwa ajili ya manufaa ya uchumi wa Taifa
hili,” alisema.
Kuongoza kisomi
Profesa Muhongo alisisitiza kuwa akipewa dhamana, ataunda
Serikali ya kisomi ambayo itatekeleza majukumu yake kwa kutegemea tafiti
mbalimbali za kisayansi. Alisema Serikali zote katika nchi
zilizoendelea zinafanya hivyo.
Alisema nchi inayoongoza kwa kuwa na watafiti
wengi duniani ni Finland, ambayo ina watafiti 7,707 katika watu milioni
moja. Alisema utafiti ndiyo umeufanya uchumi wa nchi hiyo kuwa imara.
Alisema Tanzania haiwezi kujenga uchumi kama
hakuna wataalamu wa kutosha watakaojua rasilimali zilizopo nchini na
kuelewa namna ya kuzitumia ili ziwanufaishe Watanzania wote. “Mtu wa kufanya yote haya ndani ya CCM ni mimi,
mnanijua vizuri, sina ubabaishaji kwenye mambo muhimu ya maendeleo.
Naomba kupewa dhamana hii ili kukuza uchumi wa nchi yetu na mtu
mmojammoja,” alisema Profesa Muhongo.
Moja ya mipango yake ya kutokomeza umaskini ni
kuwekeza katika elimu. Katika eneo hili alisema, atahakikisha vifaa vya
elimu vinapatikana shuleni na masilahi ya walimu yanaboreshwa. Alitolea
mfano wa nchi ya Finland kwamba inawalipa walimu mishahara sawa na
madaktari.
Profesa Muhongo alisisitiza kuwa utafiti ni jambo
muhimu katika utawala na biashara za kawaida. Alisema mfanyabiashara
anaweza kufanya utafiti mdogo wa kutaka kujua bidhaa gani inanunuliwa
zaidi sehemu fulani ili kuifanya kwa ufanisi.
“(Said) Bakhresa anauza sana kwa sababu anafanya
utafiti, kabla ya kutengeneza bidhaa. Nchi ikiendeshwa kwa tafiti
tutapata maendeleo kwa haraka na kufikia lengo la kuwa nchi yenye uchumi
wa kati miaka 10 ijayo,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza: “Mfanyabiashara anayepanga lazima ajue nchi ina
watu wangapi na dunia ina watu wangapi ili ajue auze huko kiasi gani cha
korosho, pamba au kahawa anayozalisha. Wote wakifanya hivyo, uchumi
wetu utakua kwa kasi.”
Changamoto
Profesa Muhongo alisema tangu nchi inapata uhuru,
ilikuwa na maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi, wakati
huo ikiwa na watu milioni tisa, lakini kufikia Mei, kuna watu milioni
49.5 na matatizo hayo bado ni sugu.
Alisema ongezeko hilo la watu limesababisha
changamoto nyingine ambazo atakabiliana nazo. Alizitaja kuwa ni rushwa,
ukosefu wa ajira kwa vijana, siasa kila mahali, uonevu na dhuluma.
Changamoto nyingine alizitaja kuwa ni kutojiamini
kwa Watanzania, uvivu na utegemezi, kutopatikana kwa takwimu sahihi na
kupungua kwa amani, utulivu, upendo na usalama wa Taifa. Alijigamba kuwa
kwa elimu yake, anajiamini na ana uwezo wa kufanya hayo.
Hali iliyokuwa
Atangaza nia
Usomi wake
“Kiongozi lazima awe na maono na kujua namna ya kutekeleza maono
yake. Vipaumbele vyangu ni kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuondoa
umaskini. Hakuna mtu mwingine anayeweza kufanya haya ndani ya CCM, ni
mimi tu,” alisema Profesa Muhongo, huku akishangiliwa na mashabiki wake
waliohudhuria hafla hiyo.
Hali iliyokuwa
Watu wa hali ya kawaida mjini Musoma ndiyo
waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza Profesa Muhongo. Walioonekana kuwa
na uwezo walitumia pikipiki kufika eneo alilotangazia nia.
Waendesha pikipiki, maarufu bodaboda, walifaidi
matunda ya mkutano huo kutokana na kupata abiria wengi kutoka viunga vya
mji wa Musoma kuwapeleka wananchi katika Ukumbi wa MCC ilikofanyika
shughuli hiyo.
Hata hivyo, shughuli hiyo ya Waziri wa zamani wa
Nishati na Madini, iliingia doa baada ya umeme kukatika saa sita mchana
na kusababisha malalamiko kwa baadhi ya wananchi, baadhi wakidai kwamba
ni hujuma ya washindani wake. “Nchi hii ni hatari wameona anatangaza jembe
wakakata umeme ili tusimshuhudie,” alisikika mtu mmoja akilalamika eneo
la Bohari Kantini.
Umeme huo ulirejea saa 9.15 alasiri kwa dakika
kadhaa na kukatika tena ilipotimu saa 9.33 alasiri. Baadaye saa 9.55
alasiri ulirejea.
Hali hiyo ilionekana dhahiri kumkera Profesa
Muhongo ambaye kwenye hotuba yake alisema alipokuwa waziri wa wizara
hiyo, wananchi walisahau kukatika kwa umeme.
Hata hivyo, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) Mkoa wa Mara, Henry Byabato alisema umeme ulikatika mikoa ya
Kanda ya Ziwa kutokana na hitilafu hiyo iliyotokea kwenye Gridi ya
Taifa.
Profesa Muhongo ambaye aliingia ukumbini akiwa
ameongozana mkewe, Bertha na mfanyabiashara maarufu mjini hapa, Dora
Jama na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Daud Misango huku
akishangiliwa, alisema muda huu siyo wa kutukanana au kulaumiana kwa
sababu mambo hayo hayaondoi umaskini wa Watanzania.
Kama kawaida yake, alikuwa na vibwagizo,
kimojawapo kikiwa ni juu ya wasifu wake akisema hana haja ya kuelezea
kiwango chake cha elimu, kwani anaweza kutumia muda mrefu, bali kama ni
kusoma amesoma na utaalamu wake umefikia hatua ya mwisho.
Atangaza nia
Akitangaza nia yake hiyo, Profesa Muhongo alitaja vipaumbele
vyake kuwa ni pamoja na mtazamo mpya, maono ya mbali, mabadiliko,
msimamo usioyumbishwa, uzoefu na mafanikio.
Alisema ana uhakika wa kuyasimamia hayo kwa kuwa
ni mchapakazi mwenye kuaminika aliye na utaalamu na ujuzi wa hali ya
juu, mzoefu wa kimataifa, mkweli, mwaminifu, mwadilifu, mzalendo wa
kweli, mtu wa uamuzi wa busara na mwenye uwezo wa kusimamia ilani.
“Nia yangu ni kuomba ridhaa ya wanaCCM, tusifanye
sherehe, sikuja hapa kumsema mtu kwa sababu hata ukimsema umaskini wa
watu wetu bado upo palepale mimi nimekuja na suluhisho la kuwaondolea
umaskini Watanzania,” alisema Profesa Muhongo.
Kama kawaida yake anapokutana na watu, aliwataka
wananchi wenye kalamu na karatasi kuanza kuandika takwimu kwa sababu
hazungumzi bila utafiti... “Nilikata kadi ya Tanu mwaka 1975 nikiwa JKT
(Jeshi la Kujenga Taifa) na mwaka 1977 nikakata ya CCM na risiti zote
ninazo hizi hapa (huku akizionyesha kwa wananchi), hivyo ni mwasisi wa
CCM, kama naweza kutunza hivi, basi mimi ndiyo nafaa kutunza rasilimali
zenu.” Alisema hafanyi kampeni za urais, bali anachohitaji ni kupewa
ridhaa ya chama ili kupeperusha bendera yake, huku akikataa kuahidi
chochote kwa sababu hawezi kuahidi kujenga shule au kupandisha mishahara
bila kukuza uchumi ambao ndiyo kazi yake kuu.
Profesa Muhongo alisema Watanzania pia
wanakabiliwa na tatizo la kupungukiwa ushindani kuanzia katika michezo,
ajira na soko la kimataifa kutokana na kutojiamini hata kwa mambo
wanayoyajua na kuyamudu vyema.
“Ajira za ndani na nje tunalalamika tu ooh..fulani
anatuchukulia kazi zetu na hata kwenye masoko tuko nyuma sana kama
Taifa. Anayetaka kuongoza Tanzania lazima ajue mambo haya na awe na
maono ya kukuza ya uchumi, kuondoa umaskini, kuongeza uzalishaji na
kuongeza uwezo wa kujitegemea wa watu binafsi na Taifa,” alisema.
Usomi wake
“Itoshe tu kusema kama ni kusoma nimesoma hadi
mwisho wa kisomo kinapoishia. Nikieleza utaalamu ambao unaanza baada ya
kisomo pia nimefika hadi mwisho wa utaalamu unapofikia,” alisema
mtaalamu wa Jiolojia.
Alisema katika maisha yake ya utaalamu, amefanya
utafiti na wataalamu wa Ujerumani kwa miaka 30 na wenzake wa Uingereza
kwa zaidi ya miaka 20 huku akifanikiwa kupanda ngazi ya juu katika vyama
vya wataalamu wa jiolojia Marekani, China na Uingereza.
Alijigamba kwamba hata mkewe Bertha
aliyemtambulisha kwenye mkutano huo, ni mwanasayansi ya Kemia na iwapo
atafanikiwa kuwa rais, Taifa hili litaongozwa kwa mara ya kwanza na
wanasayansi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment