
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwasili kwenye Uwanja wa Extended
mjini Urambo mkoani Tabora katika moja ya mikutano yake ya kisiasa.
Historia
Freeman Mbowe ni Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Jina lake la kwanza “Freeman”
waliwahi kupewa vijana wengi tu waliozaliwa mwaka ambao Tanganyika
ilipata uhuru. Mbowe alizaliwa Septemba 14, 1961 hapahapa Tanzania.
(atafikisha miaka 54 Septemba). Baba yake, Mzee Aikael Mbowe, ni
miongoni mwa wapigania uhuru wa Tanganyika walioshirikiana vyema na
Mwalimu Julius Nyerere kabla na baada ya uhuru.
Wasomaji wataniwia radhi kwa sababu taarifa za
elimu ya kiongozi huyu na mambo mengine muhimu yanayohusu wasifu wake na
mtiririko wake haviko katika tovuti ya Bunge. Lakini pia ofisi yake
haikutoa ushirikiano ili kupata taarifa hizo na hata viongozi wa juu na
waandamizi wa chama hicho (ambao wengine ni marafiki zangu) waliahidi
kukamilisha wasifu huo na kunipa lakini baadaye wakanieleza kuwa
hawawezi kuutoa kwa sababu Mbowe siyo mgombea urais, pamoja na kuwa
nilishawajulisha kuwa anachambuliwa kwa sababu anatajwa na wananchi kuwa
ana sifa na vigezo.
Watu wa karibu na kiongozi huyu wamenijulisha kuwa
amewahi kuwa mfanyakazi wa muda mrefu katika sekta ya fedha hapa nchini
na nchi jirani na nimeambiwa kwamba amewahi kuwa mfanyakazi wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kipindi kirefu.
Mbowe ni mmoja wa waasisi muhimu wa Chadema tangu
mwaka 1992 na ndiye alikuwa muasisi kijana zaidi kuliko wote
walioanzisha chama hicho. Baada ya kuasisiwa, alipewa jukumu la kuongoza
kurugenzi ya vijana kwa miaka kadhaa lakini pia akiwa mtu muhimu katika
utekelezaji wa masuala ya michakato ya ujenzi wa chama na ushauri wa
usimamizi wa fedha.
Baada ya kukitumikia chama chake kati ya mwaka
1992 – 2003, Mbowe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa mwaka 2004,
akichukua nafasi ya Bob Makani (sasa marehemu) na ameendelea kuongoza
chama hicho kwa miaka zaidi ya 10 hadi sasa.
Pamoja na kuongoza chama, Mbowe ni Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), aliianza nafasi hiyo mwaka 2010
akichukua nafasi ya Hamad Rashid wa CUF, amemuoa Dk Lilian Mtei na wana
watoto.
Mbio za ubunge
Mbowe, “Kamanda wa anga” alianza harakati za
ubunge mwaka 1995 katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi katika Jimbo la
Hai Mkoa wa Kilimanjaro. Hata hivyo, katika uchaguzi huo mgumu, mshindi
alikuwa ni Mwinyihamisi Mushi wa NCCR – Mageuzi ambaye alipata kura
29,046 (52.0%), Mbowe alipata kura 15,995 (28.6%) na kushika nafasi ya
pili.
Juhudi zake alizozianza mwaka 1995, zilizaa
matunda katika uchaguzi wa mwaka 2000. Safari hii akiwa amejizatiti
ipasavyo, aliwashinda wagombea wa vyama vingine akiwamo wa CCM wakati
NCCR ilionekana kudhoofu kutokana na migogoro. Alipata asilimia 64.5 ya
kura zote.
Baada ya kukaa nje ya siasa za ushindani za moja
kwa moja kwa miaka mitano, Mbowe alirejea tena mwaka 2010. Aliingia
katika kinyang’anyiro kupambana na CCM iliyokuwa imemsimamisha Godwin
Kimbita aliyeibwaga Chadema mwaka 2005. Mbowe alilirejesha jimbo hilo
kwa kura 28,545 (51.63%) dhidi ya 23,349 (42.17%) za Kimbita.
Mbio za urais
Mbowe siyo mgeni katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya nchi.
Walau ana uzoefu wa kuisaka nafasi hiyo mara moja, na hii ilikuwa mwaka
2005. Katika uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika Oktoba 39, 2005,
Chadema ilimpa fursa ya kutafuta kura za urais ili kuunda Serikali.
Lakini kabla ya siku ya uchaguzi, mgombea mwenza
wa Chadema, Jumbe Rajab Jumbe (kutoka Zanzibar) alifariki dunia na hivyo
uchaguzi ukaahirishwa hadi 14 Desemba mwaka huo ili kukipa chama hicho
muda wa kupata mgombea mwingine. Aliyejaza nafasi hiyo alikuwa Maulidah
Komu.
Baada ya matokeo kutangazwa, Mbowe aliibuka katika
nafasi ya tatu akitanguliwa na Jakaya Kikwete wa CCM aliyekuwa na
ushindi wa asilimia 80.28, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF aliyepata
asilimia 11.68. Mbowe aliwapita wagombea wengine kama vile Augustine
Mrema wa TLP na Dk Sengondo Mvungi (marehemu) wa NCCR.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mbowe
hajatangaza kugombea urais na wasaidizi wake wa karibu wameniambia
huenda hana kabisa mipango hiyo, lakini anaingia kwenye orodha ya
wanasiasa wanaochambuliwa katika safu hii kwa sababu jamii inamtazama
kama “presidential material” na kwamba anafikia sifa, uwezo, vigezo na
kila mambo muhimu yanayoweza kumfanya mwanasiasa yeyote afae kuvaa viatu
vya urais.
Nguvu yake
Nguvu na sifa ya kwanza ya Mbowe kwa siasa za sasa
ni kuwa “Kiongozi wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni”. Katika mabunge
yote duniani, huu ni wadhifa mkubwa na mara nyingi watu wanaopitia
wadhifa husika huwa wanatazamwa kama “marais wanaosubiri kuingia ikulu.”
Ameifanya kazi hii ya kuongoza upinzani kwa mafanikio makubwa na
yanaonekana ndani na nje ya Bunge. Sifa hii ni nguvu muhimu kwake kama
anataka kwenda Ikulu.
Sifa na nguvu ya pili ya Mbowe iko kwenye ujasiri.
Yeye ni mmoja wa viongozi wenye ujasiri mkubwa katika masuala
wanayoyafanya na anajua ni muda gani aongoze mapambano dhidi ya Serikali
kwa ukali na muda gani atumie lugha nyepesi. Aina ya siasa za Mbowe
ndiyo pia ilimsaidia kuwavuta vijana wengi katika chama hicho, ambao
wanaendelea kufanya vizuri kwenye ulingo huo nchini. Sifa hii nadhani
inamsaidia pale itakapotokea anaongoza nchi.
Tatu, Mbowe ni mtu mwenye msimamo na anayetaka
mambo yafanyike na kuonekana kwa haraka, naweza kusema kuwa ni mmoja wa
viongozi wanaohitaji matokeo ndani ya muda mfupi na staili yake ya
uongozi imemsaidia katika maeneo kadhaa, mathalan; amekuwa Mbunge wa Hai
kati ya mwaka 2000 – 2005 na katika wakati wake alihimiza kazi kubwa ya
ujenzi wa sekondari za kata. Serikali ilipokuja na mkakati wa kujenga
shule za kata nchi nzima, Wilaya ya Hai haikuwa na kazi hii tena. Huu ni
mfano wa uongozi wenye matokeo.
Mwisho, tabia ya Mbowe inamtofautisha na viongozi
wengi Tanzania. Yeye ni mtu wa kawaida naweza kusema. Akiongea na
makundi ya kijamii hutumia lugha ambazo makundi hayo yangependa
kuzitumia na hii ni sifa muhimu kwa viongozi waliofanikiwa duniani.
Ndiyo maana mwandishi mkongwe hapa nchini, Samson Mwigamba, aliwahi
kumuelelezea Mbowe kwenye gazeti moja la kila wiki, kama “…mtu wa watu
“social”, anayeweza kuongea hata na walinzi na wahudumu wa chini kabisa
na kutaniana nao, lakini asiyetaka mchezo kwenye kutekeleza wajibu wake.
Huweza kujishusha sana kiasi kwamba wakati mwingine utamkuta akitoa
“photocopy” za nyaraka za chama na hata kubana karatasi pamoja
(stepling)”. Tabia za Mbowe zinamfanya awe na uhuru wa kujichanganya
mahali popote na kufanya jambo lolote na sifa hii ni kubwa na muhimu.
Mwisho ni ubunifu na uwezo wa kufanya siasa za
kisasa. Kati ya Watanzania waliotoa mchango mkubwa katika kubadilisha
mazingira ya kisiasa kutoka zile za kizamani na kuanza kufanya za kisasa
ni pamoja na Mbowe. Ndani ya chama chake mathalan, amefanikiwa
kusimamia uanzishwaji wa mambo kadhaa ambayo baadaye yalikuwa maarufu
kwa Watanzania, moja ya masuala hayo ni “kubuni vazi la kombati kwa
chama chake” lakini pili ni kuanza utaratibu wa kutumia helikopta ili
kuwafikia wapigakura haraka na kwa ufanisi. Jambo hili sasa linafanywa
na vyama karibu vyote vyenye uwezo, kila vinapoona inafaa. Sifa hii ya
ubunifu na uwezo wa kufanya siasa za kisasa ni mambo muhimu pia kwa mtu
anayetaka kuongoza dola.
Udhaifu wake
Nayatizama mambo matatu kama udhaifu wa Mbowe:
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Nini kinaweza kumwangusha?
Asipochaguliwa (Mpango B)
Hitimisho
Jambo la kwanza ni tabia ya kutangaza uamuzi mgumu na wakati
mwingine asiweze kuutekeleza na au bila kuwa amekubaliana na wenzake.
Mara kadhaa amewahi kusikia akitangaza maandamano makubwa au akitoa
masharti makubwa kwa Serikali na kuna wakati haikuyatekeleza na
hakuchukua hatua zaidi. Wepesi huu wa kutangaza maazimio kadhaa bila
kufanya mashauriano ya kina, mapana na ya kimkakati na wadau wote wa
ndani na nje ya chama chake – vinampunguzia uwezo wa kiutendaji ambao
amekuwa akizoeleka nao.
Udhaifu wa pili ni katika kufanya uamuzi. Watu
waliofanya kazi na Mbowe ndani ya Chadema kwa muda mrefu, wameniambia
kuwa ana tabia ya kufanya uamuzi kwa haraka mno na ana tabia ya kuamini
taarifa za watu anaowaamini, hataki hakuzichuja vizuri. Staili hii ya
uamuzi na tafakuri ya mambo ni upungufu ambao unaweza kumwangusha
kiongozi yeyote. Mara kadhaa nimesisitiza kuwa kiongozi mzuri hupaswa
kufanya uamuzi, lakini hupaswa kuyafanya kwa utaratibu na akijipa muda
wa kutosha wa kupima athari zake ziwe za muda mfupi na muda mrefu.
Tatu, Mbowe kwa kipindi kirefu amekuwa akihimili
siasa za kiuhamasishaji na harakati na kuna wakati amewahi kusikika
kwenye chombo kimoja cha habari akisisitiza kuwa chama chake kinaachana
na siasa za harakati. Kwa umri wa vyama kama Chadema, si sahihi kufanya
harakati hadi hivi sasa. Kimeshakomaa na kinahitaji kujipanga
kushirikiana na vyama vingine vilivyokomaa kupewa ridhaa ya uongozi
nchi. Siasa za kiuhamasishaji za Mbowe pamoja na ufanyaji harakati pana
vinaweza kuwa udhaifu mwingine ambao bado ameendelea kuushikilia, pamoja
na kuwa chama chake kinakwenda mbele zaidi, kikianza kuhimili kasi ya
siasa za kitaifa, za kupigania nchi na siyo harakati za kawaida au
masuala madogo.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Mambo mawili makubwa yanaweza kabisa kumvusha Mbowe na akawa mgombea urais wa Chadema na labda baadaye Ukawa:
Moja, yeye ni mhimili muhimu wa ukuaji wa Chadema.
Chini ya uongozi wake, ndipo kwa mara ya kwanza Chadema kilipata
wabunge wenye ujasiri mkubwa, kina Zitto Kabwe, Halima Mdee na wengineo
na kwa wakati huo chama hicho kilikuwa na wabunge wengi kuliko vingine
vya upinzani Tanzania Bara. Lakini pia, chini ya uongozi wake ndipo
kiliruka kutoka kuwa na wabunge 11 kwa ujumla katika Bunge la Muungano
mwaka 2005 hadi kuwa na wabunge zaidi ya 40 mwaka 2010. Mafanikio haya
yametokea chini ya usimamizi wake na huenda yakawa moja ya sababu za
kumpitisha kugombea urais ili aweze kusimamia mabadiliko makubwa ya
nchi.
Lakini jambo la pili ni uzoefu wa muda mrefu ndani
ya siasa za upinzani. Tofauti na wanasiasa kadhaa wakubwa ambao tangu
mwaka 1992 hadi leo wamekuwa kwenye vyama vitatu au vinne, Mbowe amekaa
Chadema muda wote huo na amekijua vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa mbunge
na hata mgombea urais kwenye kipindi kimoja. Uzoefu huu unaweza kuifanya
Chadema pia imuone kama mtu muhimu katika nafasi ya urais.
Nini kinaweza kumwangusha?
Mambo mawili makubwa yanaweza kumwangusha katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya Chadema:
Jambo la kwanza ni umaarufu na ukuu ambao Katibu
Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa, ameujenga kwa Watanzania. Pamoja na kwamba
Mbowe alikabidhiwa uenyekiti wa Chadema na Dk Slaa akiwa Katibu Mkuu
wake miaka 10 iliyopita, lakini kwenye Bunge la mwaka 2005 – 2010 ambalo
Mbowe hakuwemo, Dk Slaa, Zitto na Mdee walikuwa miongoni mwa watu
waliofanya kazi kubwa ya kujenga taswira ya Chadema. Baada ya hapo Dk
Slaa aligombea urais mwaka 2010 na kupata kura nyingi kiasi cha
kuitikisa CCM. Ikiwa Dk Slaa atahitaji kugombea nafasi hiyo tena mwaka
huu, huenda chama hicho kikampa nafasi kubwa zaidi na hivyo Mbowe
akasubiri wakati mwingine.
Jambo la pili ambalo ni la moja kwa moja, ni ikiwa
Chadema haitatoa mgombea Rais. Sielewi viongozi wa Ukawa wanapanga
kutumia utaratibu gani kumpata mgombea urais, lakini ikitokea nafasi
hiyo inakabidhiwa kwa chama kimoja na chama hicho kisiwe Chadema, moja
kwa moja Mbowe atapaswa kujipanga kwa majukumu mengine zaidi.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Mbowe anaweza kuwa na mipango mitatu ikiwa hatapitishwa kugombea urais:
Moja ni kugombea ubunge katika Jimbo la Hai –
Kilimanjaro. Tukumbuke kuwa yeye ni mbunge wa jimbo hilo hadi sasa na
sijaambiwa ikiwa hatagombea na mara nyingi ameonekana akizidi
kujiimarisha mno kisiasa katika jimbo hilo. Nadhani atakuwa na fursa ya
kugombea kipindi kingine, ikiwa hatagombea urais.
Pili, nadhani Mbowe atakuwa na kazi ya kuendelea
kuijenga Chadema. Ni mwenyekiti wa chama kwa sasa na nadhani bado
anaweza kugombea tena uenyekiti kwa sababu kwa siasa za Afrika kugombea
uongozi mara nyingi ni utamaduni wa kawaida na unatokana na sababu ya
watu madhubuti kuendelea kuhitajika katika taasisi ili ziwe imara zaidi
kabla ya kuwaachia wengine.
Mwisho ni kuendelea na biashara. Mbowe ni
mfanyabiashara na anamiliki miradi na kampuni kadhaa. Ikiwa hatagombea
urais na labda kuipata nafasi hiyo, naona akiwa na muda mzuri wa
kuendelea na usimamizi wa biashara zake.
Hitimisho
Mbowe ni mmoja wa viongozi watakaokumbukwa kama
vinara wa mageuzi na demokrasia ya vyama vingi katika nchi. Kiongozi
huyu amesimamia mbadiliko mengi ya kidemokrasia ndani ya nchi na
ameshiriki kwa vitendo. Naamini bado anapaswa kuwa na mchango mkubwa kwa
Taifa kama letu ambalo ndiyo kwanza linajikongoja kuelekea kwenye
maendeleo. Sehemu kubwa ya masuala anayoyasimamia yana tija kubwa na
huwezi kuyabeza kirahisi. Namtakia kila la heri katika harakati za
kuitafuta Tanzania ambayo inasubiriwa na wengi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment