Pages

Monday, May 04, 2015

WASIRA AWAPIGA KIJEMBE WANAOTAMBIA SHULE ZA KATA

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (kushoto) akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake Dar es Salaam.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira amewakosoa baadhi ya vigogo wanaojinasibu kuanzisha programu ya shule za sekondari za kata nchini akisema ni ujinga kusema hivyo kwa kuwa miradi yote hufanywa na Serikali na siyo mtu binafsi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake juzi, Wasira alisema wazo la kujenga sekondari kila kata ni ahadi ya CCM katika ilani ya mwaka 2005 na si wazo la mtu mmoja kama inavyodaiwa. Huku akitumia nadharia ya uendeshaji Serikali, Wasira alisema miradi yote ya maendeleo inafanywa kwa pamoja na kwamba kama ni kuihusianisha na mtu mmoja, basi mwenye sifa hiyo ni Rais.
Kauli ya Wasira ilikuja baada ya kuulizwa juu ya changamoto mbalimbali zinavyoikabili nchi na masuala ambayo rais ajaye anatakiwa kufanya ili kuiletea nchi maendeleo.
“Mtu anayesema alijenga sekondari za kata anawadanganya Watanzania. Ile kitu ipo kwenye ilani ya CCM… jitihada na sifa za kujenga sekondari huwezi kuzihamisha kutoka kwa rais anayeongoza nchi na kusema waziri mmoja tu ndiyo anahusika, nakataa kabisa na yeyote anaweza kuninunia kwa hilo,” alisema Wasira huku akisisitiza anazungumzia masuala (issues) na siyo kumshambulia mtu.
Alisema Serikali inapoamua kufanya mradi ni jambo la pamoja na huendeshwa kama familia, hivyo hakuna mtu mmoja katika baraza anaweza kusema ni la pekee yake kutokana na kuangukia katika wizara yake.
“Mimi ni waziri wa kilimo, sisi tumeanzisha mambo mengi ikiwamo kuishauri Serikali ianzishe benki ya wakulima inayoanza Julai mwaka huu lakini siwezi kusema bila mimi kusingekuwa na benki au ruzuku kwa wakulima… sasa kila mtu akichukua sifa hizo Rais atachukua sifa ipi?” alihoji.
Ingawa Wasira hakutaja jina la mtu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amekuwa akihusishwa kusema mara kwa mara kuwa alikuwa kiungo muhimu katika uanzishwaji wa mpango wa shule za kata nchini.

Ukawa si tishio
Katika mahojiano hayo ya takriban saa 1.30, Wasira alipuuza nguvu ya Ukawa kisiasa kwa sasa akisema umoja huo wa Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, hauinyimi usingizi CCM kwa kuwa vyama vya upinzani havina maono ya maendeleo kama ilivyo kwa chama tawala.
Alisema anajua Ukawa ina mbinu na sera zake lakini siyo tishio kwa sababu CCM itakwenda kwa wananchi kwa hoja. “Wenzetu ukiwauliza wana mikakati gani hawana… huwezi kwenda kwa wananchi kwa kelele tu wakakuchagua… lazima uonyeshe mwelekeo, unataka kuipeleka nchi yao wapi, kwenye maandamano?
“Nimekaa na vyama hivi sijapata kusikia jambo la msingi la maendeleo au dira ya maendeleo ya vyama vyao. Hata ukimkamata Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman) leo ukimuuliza wewe unataka kuongoza nchi, utafanya nini... hana lolote la kukwambia,” alisema.
Alisema vyama hivyo vinaongoza kwa kulalamika badala ya kutafuta majibu ya matatizo yanayowakabili wananchi na kusema, ifikie kipindi viongozi waache kuwatengeneza wananchi kuwa jamii ya kulalamika mara kwa mara isipokuwa tu pale Serikali inapotokea kushindwa kabisa.
Wasira aliyekuwa makini kujibu maswali hayo, alipoulizwa CCM imejiandaaje kisaikolojia iwapo itashindwa Uchaguzi Mkuu ujao, alisema imejiandaa kushinda na siyo kushindwa na ikitokea ikashindwa itajulikana mbele kwa mbele.
Alisema CCM ni chama tawala kilichofanikiwa mambo mengi ya maendeleo hivyo hakijiandai kushindwa na kwamba ikitokea mtu anakwenda kugombea akijua atashindwa, basi hana akili. “Unavyokwenda kugombea unakuwa umeshafanya utafiti kuwa utashinda na hiyo ndiyo nguvu inayowapeleka, lakini kushindwa ni kama ajali ambayo huwezi kuipanga… sisi tunapanga kushinda, tena siyo kidogo, bali kwa kishindo na uwezo tunao, nia tunayo na sababu zipo nyingi,” alisema huku akicheka.

Serikali za Mitaa
Pamoja na kwamba CCM ilipoteza viti vingi kwa upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana, Wasira alisema hilo si tishio na bado anaona kwamba vyama hivyo bado ni dhaifu. Alisema katika uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa kishindo kwa asilimia 80 na kwamba asilimia za upinzani ni halali kuongezeka kwa kuwa vyama hivyo pia vinakua.

CCM na uteuzi
Akizungumzia kuchelewa kwa kipenga cha kuruhusu makada wa CCM kuanza mchakato wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, Wasira alisema kunatokana na kubadilika kwa taratibu za kichama ambazo si sheria lakini lazima zifuatwe. “Kuna vyama 22 nchini kwa nini watu wanasema CCM imechelewa... imechelewa nini mbona hata wanaojiita Ukawa nao kwani wamemaliza? Kwanza CCM ina watu wengi wanaojulikana hata ukimteua leo mmoja wao, wananchi watasema ni huyu lakini vyama vingine hata hawajulikani sana, sasa tatizo lipo wapi?” alihoji Wasira.
Alipoulizwa iwapo kuchelewa huko ni mbinu za kutegeana na Ukawa kusimamisha wagombea kama inavyodaiwa na wachambuzi wa mambo, alisema CCM haiwezi kutegea chama chochote. “CCM haina mapatano na chama chochote wala haiwezi kungojea chama kingine wala kutegea, hatujafika huko. Sisi ni chama kikubwa tukae tunategea Ukawa hadi lini lakini mkumbuke zile kanuni zinategemea nafasi.
“Kulikuwa na mambo mengi hapo mbele kama Kura ya Maoni Aprili na mambo mengine yaliyotakiwa yapeane nafasi lakini Tume (NEC), imeamua lipelekwe mbele kwa sababu haijamaliza kuandikisha wapigakura… sasa ni uamuzi wa chama!

Uhusiano na uratibu
Alipotakiwa kuelezea iwapo kusuasua kwa uhusiano baina ya Serikali na baadhi ya wadau wengine kama taasisi za kidini kulisababishwa na yeye kwa kutomshauri vizuri Rais akiwa Wazira wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Wasira alijibu: “Hilo utaamua mwenyewe.”
Ila alibainisha kuwa kwa miaka yote ya nyuma kumekuwa na uhusiano mzuri tangu Rais Kikwete aingie madarakani lakini mambo yamebadilika baada ya kuanza mchakato wa Katiba kutokana na kuwapo maoni tofauti. “Mahusiano ni mchakato, hakuna kipindi ukasema yametosha kwa sababu kila siku mambo mapya yanaibuka na huwezi kuzuia yasije. Ukumbuke mwaka 2010 mambo yalikuwa mazuri lakini baada ya Katiba vyama vikaja na ajenda zao, taasisi za dini nazo… hivyo Serikali haina mgogoro wowote na wadau wake,” alisema.

Kugombea urais
Wasira ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kugombea urais mwaka huu na tayari alishapigwa adhabu ya mwaka mmoja kwa kuanza kampeni mapema akiwa na vigogo wengine watano wa chama hicho.
Hata hivyo, juzi alipotakiwa kueleza akiwa rais anatakiwa kufanya nini, alisema asingependa kuzungumza kama mgombea, bali alisema kwa ujumla kiongozi ajaye anatakiwa kuendeleza mikakati ya maendeleo ikiwamo dira ya maendeleo ya miaka mitano baada ya ile sasa kumalizika mwakani.
Alisema japo hamfahamu, alisema rais huyo, anatakiwa awekeze katika ukuzaji wa kilimo na viwanda ikiwa ni mwendelezo wa dira iliyopo iliyojikita katika kuondoa vikwazo vya kiuchumi na biashara kwa kuwekeza kwenye miundombinu.
Alisema Rais Kikwete imefanya mambo mengi mazuri ya maendeleo yakiwamo kukuza elimu ikiwamo ujenzi wa sekondari za kata, miundombinu lakini tatizo Watanzania hawataki kuangalia mema. “Hakuna mtu anayeweza kuthibitisha kuwa akiwapo Rais mwingine hakutakuwa na matatizo. Hata hizo shule za kata wanazokosoa bado zinasaidia sana na wanafunzi takriban milioni 1.5 wanasoma. “Kama mchumi nafahamu mkiharakisha sana hatua za maendeleo, kuna wakati mnashusha ubora ila baada ya hapo mnachukua hatua,” alisema Wasira.

Uchaguzi Mkuu
Mbunge huyo wa Bunda (CCM) naye hakuacha kuwananga wale wanaonyesha wasiwasi kuwa Uchaguzi Mkuu huenda usifanyike mwaka huu akidai ni vigumu kuahirisha shughuli kwa kuwa ipo kikatiba na haiwezi kutokea katika hali ya kawaida.
Alisema kama alivyosema Rais Kikwete wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi, uchaguzi huo utakuwapo na hakuna haja ya watu kuanza kulalamika wakati bado ni mapema. “Haiwezekani kubadilisha Katiba kirahisi na hakuna mwenye mamlaka hayo zaidi ya Bunge na kuahirisha siyo jambo la kawaida labda kuwe na vita. Sasa hao wanaosema utaahirishwa wamepata wapi hayo maneno? Wanazidi kuwafanya wananchi kuwa watu wa kulalamika.”

Ilani ya CCM
Wasira ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kuandaa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho mwaka 2015 - 2020, alisema wanaendelea vizuri shughuli hiyo huku akikataa kueleza mambo ya msingi yatakayozingatiwa.
Baada ya kukamilisha rasimu ya hiyo, alisema watapeleka kwa mamlaka zilizowaagiza ambazo ni Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa maboresho zaidi na kuipitisha tayari kwa ushindi wa kishindo.
Hata hivyo, Wasira alipotakiwa kueleza iwapo kuchaguliwa kwake katika kamati hiyo kuna lengo la kupunguza nia yake ya kugombea urais, alijibu kuwa hakuna kitu kama hicho na kwamba yeye ni mjumbe wa NEC hivyo ana sifa ya kufanya hivyo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment