Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (kushoto) akichangia bungeni mjadala
 wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
 Utawara Bora na Uhusiano na Uratibu kwa mwaka wa fedha 2015/2016, 
mjini Dodoma jana.
Mjadala wa bajeti mwaka
 2015/16 umegeuka mwiba mchungu kwa Ofisi ya Rais baada ya mawaziri 
watatu waliopo katika ofisi hiyo kubanwa na wabunge wa upinzani hasa 
wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakisema “njaa 
imeanzia Ikulu na Ofisi ya Rais inayosimamia Taasisi ya Kuzuia na 
Kupambana na Rushwa (Takukuru) haina utashi wa kupambana na rushwa.”
Mawaziri hao jana walitakiwa kueleza sababu za 
ofisi hiyo kushindwa kutokomeza rushwa, mikakati ya Serikali kuiwezesha 
Takukuru na kuipa meno ya kuwashtaki moja kwa moja watuhumiwa wa rushwa.
Kambi hiyo imeilipua Taasisi ya Wanawake na 
Maendeleo (Wama) inayoongozwa na mke wa Rais, mama Salma Kikwete 
wakitaka ifutwe kwa maelezo kuwa imekiuka sheria za nchi.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Muhambwe 
(NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliibua malumbano makali kati yake na 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na 
Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o, baada ya kudai kuwa Ikulu na 
Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kupambana na rushwa licha ya kuwa 
chini ya Rais.
Alivyochafua hali ya hewa
Katika mjadala huo, Mkosamali alihoji; “kama 
Takukuru, Mkurabita na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) ziko
 chini ya Ofisi ya Rais na bado zinalia njaa, kwa nini watumishi wa umma
 kama wauguzi na walimu wawe chini ya ofisi hii badala ya kuwa katika 
Ofisi ya Waziri Mkuu au Tamisemi?
“Yaani njaa imeanzia Ikulu. Tumeiweka Takukuru 
Ikulu tukidhani kuwa Rais ataweza kupambana na rushwa, sasa ukiona 
taasisi hiyo imefeli tambua kuwa Rais hana utashi wa kisiasa wa 
kupambana na rushwa
“Watu wanajua Takukuru ikiwatuhumu katika kesi 
kubwa zitafutwa. Taasisi hii kufeli kufanya kazi maana yake ni kuwa 
Serikali imefeli katika miaka yote minane, hata Rais hakuwa na nia ya 
kupambana na rushwa,” alisema na kusisitiza jinsi Bunge la Katiba 
lilivyoshindwa kuipa meno Takukuru kupitia Katiba Inayopendekezwa.
Alihoji, “Tasaf wameomba Sh18 bilioni mwaka jana 
na mpaka sasa wamepewa Sh3 bilioni na sasa hivi mnaomba tena mabilioni 
ya shilingi. Hivi mnataka wakurugenzi wa Tasaf na wafanyakazi 
wawachukuliaje?”
Alihoji taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais 
kutopewa fedha za bajeti kama ilivyoidhinishwa mwaka jana na kusema 
kitendo cha mwaka huu wizara tatu za Ofisi ya Rais kuja na bajeti 
nyingine wakiomba mabilioni ya fedha ni fedheha.
“Kama taasisi zilizopo Ikulu zina njaa, hivi 
nyinyi huko katika halmashauri si ndiyo mtakufa! Rais ambaye taasisi 
hizi zipo ofisini kwake anashindwa kuzihudumia atawakumbuka watu wa 
Kibondo? Hii Serikali imechoka kabisa na imechakaa,” alisema.
Kauli hiyo ilimnyanyua Mkuchika na kuomba kutoa 
taarifa, jambo ambalo lilipingwa na Mkosamali akidai kuwa awali aliomba 
kutoa taarifa kwa mwenyekiti na kunyimwa.
Wabunge wasisitiza
Wama yalipuliwa
Mafanikio ya Takukuru
Mishahara
“Mwenyekiti usiendeshe Bunge namna hii, nieleze umetumia kanuni 
gani ya kunizuia nisitoe taarifa na kumruhusu Mkuchika. Umetumia kifungu
 kipi, kwani huyu (Mkuchika) si mbunge kama mimi,” alihoji Mkosamali na 
kujibiwa na Mng’ong’o kuwa Mkuchika ni waziri.
Huku akiwa amesimama, Mkosamali aliendelea kuzungumza licha ya kuzimiwa kipaza sauti.
Katika taarifa yake Mkuchika alisoma Kanuni ya ya 
Bunge 64 (d) inayosema; Hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika 
mjadala au kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kuamua jambo 
lolote kwa namna fulani. “Mkosamali wakati anachangia ameeleza Rais hana 
nia ya kupambana na rushwa. Namtaka afute kauli hiyo kwa sababu 
amekwenda kinyume na kanuni za majadiliano. Ila mchana nikimjibu 
nitamweleza alichokifanya Rais katika kupambana na rushwa,” alisema 
Mkuchika.
Taarifa hiyo ilikataliwa na Mkosamali akisema: 
“Nitafutaje wakati ndiyo hali halisi. Juzi, Katibu Mkuu Kiongozi (Balozi
 Ombeni) Sefue kawasafisha wala rushwa. Kesi kubwa zote mmezifuta na 
suala la kuiongezea meno Takukuru lililokuwa katika rasimu ya (Jaji 
Joseph) Warioba mmeshindwa kuliweka katika Katiba Inayopendekezwa.”
Licha ya kutakiwa na Mng’ong’o kufuta kauli ya 
‘Rais kashindwa kupambana na rushwa’, Mkosamali alisisitiza, “Nimesema 
Takukuru wakituhumu kesi 4,000 wanashinda kesi 40 hadi 50, sasa huo ni 
uongo, kweli wana nia ya kupambana na rushwa?”
Wabunge wasisitiza
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Karagwe (CCM), 
Gosbert Blandes alisema Sheria ya Kupambana na Rushwa inatakiwa 
kubadilishwa ili kuiwezesha Takukuru kumshtaki moja kwa moja mtuhumiwa 
wa rushwa, badala ya kumchunguza tu na kupeleka faili kwa DPP.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine 
alisema: “Takukuru inatakiwa ipewe fedha kwa wakati na watumishi wa 
kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Tunatakiwa tuwe na 
sheria kali ili watakaokamatwa kwa rushwa wanyongwe au kupigwa risasi 
kabisa.”
Aliongeza, “Viongozi wote wanatakiwa kuchunguzwa 
kwa sababu wanapata maendeleo ndani ya muda mfupi tangu kuwa viongozi, 
iweje ndani ya mwaka tu mtu awe na nyumba ya ghorofa na magari?”
Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati 
alisema: “Rushwa imekithiri kwa kiasi kikubwa ninaitaka Serikali ieleze 
kwa nini haichunguzi mali za viongozi. Wapo viongozi wanaotumia ofisi za
 umma kwa masilahi yao binafsi kwani ndani ya muda mfupi wanakuwa 
matajiri wa kutupwa.”
Wama yalipuliwa
Akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu matumizi ya 
Ofisi ya Rais na Uratibu, msemaji wa kambi hiyo wa Ofisi ya Rais, Ester 
Matiko alisema, Wama inatakiwa ifutwe kwa sababu imekiuka sheria za 
nchi.
“Iweje Waziri (Simba) awe mjumbe wa Bodi ya Wama 
wakati ni wizara yake ndiyo inasimamia taasisi zisizokuwa za Serikali? 
Ikiwa Serikali imeamua kuyasafisha mashirika yasiyo ya kiserikali 
isisahau kuifutia Wama usajili,” alisema.
Katika hotuba yake, Matiko pia alisema Usalama wa 
Taifa umeshindwa kazi kutokana na nchi kuwa na matukio mengi ya ufisadi,
 mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na rushwa... “Ni jambo la 
kushangaza kuwa na Usalama wa Taifa unaoshindwa kutoa taarifa za 
kiintelejensia kuhusu ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi wasiozidi 
hata 200,000. Hii ni aibu kubwa kwa utawala wa CCM na Rais Kikwete.”
Mafanikio ya Takukuru
Awali, akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina 
Kombani alisema Takukuru imefanikiwa kurejesha zaidi ya Sh623 milioni 
baada ya kuchukua hatua mbalimbali za kupambana na rushwa.
“Kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa 
katika jitihada za kupambana na rushwa, wahusika waliopatikana na hatia 
walirejesha Sh623,941,408,” alisema Kombani.
Alisema katika kipindi cha kati ya Julai mwaka 
jana hadi Machi, majalada 50 yaliyohusu tuhuma za rushwa kubwa 
yalifikishwa kwa DPP, kati ya hayo 27 yamepata kibali na watuhumiwa 
wamefikishwa mahakamani.
Kombani alisema kesi  856 za rushwa ziliendeshwa 
mahakamani zikiwamo mpya 192. Alisema kati ya kesi hizo, 664 zilitolewa 
uamuzi na watuhumiwa 73 walipatikana na hatia na kuadhibiwa.
“Kesi 24 ziliondolewa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali na kesi 123 watuhumiwa wake waliachiwa huru,” alisema.
Katika mwaka wa fedha 2015/ 2016, Kombani alisema Takukuru itaendelea kuchunguza tuhuma 2,776 zilizopo na mpya zitakazojitokeza.
Mishahara
Akizungumzia mishahara, Kombani alisema katika 
mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali imeongeza kima cha chini cha mshahara
 kutoka Sh240,000 hadi Sh265,000 kwa mwezi. “Vibali vya ajira mpya 58,483 kati ya 68,138 vilivyoidhinishwa katika bajeti ya 2014/2015 vilitolewa,” alisema.
                
              
Majibu
Alisema mwaka 2015/2016 Serikali inatarajia 
kuajiri watumishi wapya 71,496 na kipaumbele kitakuwa katika sekta za 
elimu, afya, kilimo na mifugo.
Majibu
Akijibu hoja za wabunge hao, Waziri wa Nchi, Ofisi
 ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya alimshutumu mmoja wa 
kiongozi wa upinzani kwa kushindwa kuwa mzalendo.
Alisema kiongozi huyo akiwa Marekani, alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikikiuka haki za binadamu kwa kuwapiga wapinzani. Alisema kiongozi huyo alipigiwa makofi bila 
kufahamu waliokuwa wakifanya hivyo walikuwa wakimshangaa kwa kitendo 
chake cha kutokuwa mzalendo kwa nchi yake.
Alisema kiongozi huyo alifika mbali na kusema kuwa
 wataleta wanasheria na kuipeleka Serikali katika Mahakama ya Kimataifa 
ya Makosa ya Jinai ya The Hague. “Huwezi kumkuta Mmarekani akiisemea vibaya nchi 
yake na hii ni kwa nchi yoyote duniani. Mimi niliposikia nilishangaa 
kwelikweli,” alisema.
Aliwaomba wabunge wa upinzani kumpa heshima yake Rais na kuacha kumzungumza kama wanavyomzungumzia mbunge mwingine. “Huwezi kumzungumzia Rais kama unavyomzungumzia 
Mbunge wa Rungwe. Mimi mnaweza kuzungumza hata mkitaka kunitukana sawa, 
lakini mnapomzunguzia Rais lazima tuseme,” alisema.
Profesa Mwandosya alitumia fursa hiyo kuaga 
akisema hatagombea tena ubunge katika Uchaguzi Mkuu. “Miaka 15 
niliyopita bila kupingwa inatosha labda unaweza kuwa ndiyo mwanzo wa 
kulitumikia Taifa katika ngazi nyingine,” alisema.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, 
Sophia Simba alisema ni shirika lisilo la kiserikali moja tu la Sisi kwa
 Sisi lililofutiwa usajili kutokana na kujihusisha na ushoga.
Kuhusu Wama alisema imesajiliwa na Brela na inaendeshwa kwa kufuata taratibu za kisheria.
Katika majibu yake, Mkuchika alisema hakuna 
mkutano wowote ulioitwa na Ikulu kwa ajili ya kuwasafisha mawaziri na 
viongozi waliohusika na sakata la Tegeta Escrow wala Operesheni 
Tokomeza.
Juu ya Rais Kikwete kutokuwa na dhamira ya 
kupambana na rushwa, alisema Rais, Serikali na chama kupitia ilani yake 
ya uchaguzi wana dhamira ya dhati ya kupambana na tatizo hilo.
Alitaja mambo yanayoonyesha kuwa Serikali ina 
dhamira ya dhati kuwa ni pamoja na kujenga makao makuu ya Takukuru, 
kujenga ofisi saba za chombo hicho na kuongeza raslimali watu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment