Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Bunge la Bajeti linaendelea tena mjini hapa leo,
baada ya mapumziko mafupi ya mwishoni mwa wiki, ikiwa ni zamu ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) kuwasilisha hotuba ya makadirio ya
bajeti ya wizara yake.Masuala kadhaa ya utawala bora ikiwamo hatua ya Ikulu kuwasafisa
baadhi ya vigogo waliotajwa katika kashfa ya fedha za akaunti ya Tegeta
Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huenda yakazua mjadala mkali. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema), alipinga kauli ya
Waziri Mkuu Mizengo Pinda kudai kuwa Ikulu haijawasafisha baadhi ya
vigogo akisema inazua maswali mengi magumu.
“Nimeomba kuchangia wizara hii, hususan, masuala ya utawala bora, inaonekana wengi hawafahamu umuhimu wa jambo hili. “Utawala bora unahusika na utu, maadili, haki za binadamu, maisha ya kesho ya Mtanzania, maisha ya mtumishi wa umma.
“Sidhani kama serikali inafahamu utawala bora wenye maadili, hekima
na utawala wenye upendo…tuna tatizo kubwa hapa la rushwa, ufisadi
unaofanywa na viongozi wa umma,” alisema na kutaja mfano wa fedha
zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta iliyofunguliwa BoT ambapo zaidi ya
Sh. bilioni 300 zilichotwa.
Alisema pamoja na baadhi ya mawaziri, wabunge na watendaji wengine
kuwajibika kutokana na kashfa hiyo, wahusika waliochota fedha hizo
kwenye akaunti iliyofunguliwa benki ya Stanbic bado hawajatajwa. Alisema waliochukuliwa hatua ni wale waliopewa mgawo wa fedha hizo,
lakini wale/yule aliyeidhinisha fedha hizo zitolewe BoT hajachukuliwa
hatua yo yote. “Huo sio utawala bora,” alisema.
Baadhi ya wabunge walishangaa kutochukuliwa hatua ya kusimamishwa
mnikulu wa Ikulu Shaban Gurumo ambaye naye alifikishwa mbele ya Baraza
la Sekretarieti la Maadili ya Viongozi wa Umma akikabiliwa na kosa la
kukiuka maadili kwa kupokea Sh. 80, 850,000.
Mwanasheria wa sekretarieti hiyo, Hassan Mayunga, alidai Gurumo
anatuhumiwa kukiuka vifungu mbalimbali vya Sheria ya Maadili ya Viongozi
wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kama ilivyorekebishwa mwaka 2001. Gurumo ambaye alikuwa Naibu Katibu wa Rais, aliteuliwa kuwa mnikulu
Machi 9, 2011 kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Rajab Kianda
aliyefariki Februari 7, 2010.
Masuala ya usawa katika ugawaji wa raslimali za umma na
ushughulikiaji wa tatizo la rushwa, muundo na mfumo wa utawala wa sheria
na demokrasia, ushirikishwaji, uwakilishi na uwajibikaji yanaweza kuwa
moja ya mambo yanayoweza kuzua mjadala mkali baada ya waziri mwenye
dhamana, George Mkuchika (pichani) kuwasilisha makadirio ya bajeti kwa
mwaka 2015/16.
Katika siku za hivi karibuni, wananchi wengi wameonyesha
kutoridhishwa na utendaji katika Jeshi la Polisi na mamlaka za kisheria,
masuala kama ya rushwa na ucheleweshaji wa kesi na hata masuala ya
kubambikiwa kesi na wanyonge kutopata haki yalijitokeza kwa kiasi
kikubwa.
Wiki iliyopita katika hotuba ya makadirio ya bajeti ya ofisi ya
Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge, wabunge hususani wa upinzani waliibana
serikali kwa kushindwa kumpeleka fedha za kutosha kwenye miradi ya
maendeleo. Suala la uchaguzi mkuu pia lilipata nafasi kubwa baada ya wabunge
wa upinzani kuishinikiza serikali kutothubutu kuahirisha uchaguzi mkuu
Oktoba mwaka huu.
Mjadala kuhusu hotuba hiyo kama ambavyo itakuwa katika wizara
zingine utachukua siku mbili kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari, Elimu
kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment