Social Icons

Pages

Wednesday, May 13, 2015

UKAWA SAFI, LAKINI HUU NI MWISHO WA CUF, NCCR


Tangu Februari mwaka 2014, siasa za Tanzania zimekuwa na mwelekeo chanya kwa vyama vya upinzani kushirikiana, tofauti na  wakati wowote tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe nchini.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeweza kuunganisha vyama vitatu vikubwa na chama kimoja kidogo, na kitendo cha umoja huo kuendelea kuwapo ni mafanikio makubwa.
Haya ni mafanikio makubwa kwa  vyama vya siasa vyenye utamaduni wa kisiasa na itikadi tofauti. Ukawa umewafanya wananchi waamini kabisa kuwa mwisho wa CCM umefikia, kwani kwa muda mrefu  wananchi wamekuwa wakitamani vyama vya siasa kushirikiana.
Ukawa ni umoja ulioundwa kwa ajili ya kushinikiza kupatikana kwa katiba inayotokana na maoni ya wananchi walio wengi, kama ilivyoonyeshwa katika taarifa ya Tume ya Marekebisho ya Katiba. Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Jaji Joseph Warioba pamoja na mambo mengine, ilipendekeza kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano yenye serikali tatu.
Tafiti mbalimbali zilikuwa zinaonyesha kuwa huu ndio msimamo wa wananchi  wengi. Hata hivyo, CCM walifanikiwa kwa kutumia nguvu kubwa kuzuia mfumo huo kuanzishwa na hivyo kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa, yenye mfumo wa sasa na iliyoondoa maeneo mengi yenye kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini.
Ukawa ilijiandaa kushawishi wananchi kutojitokeza kupiga kura ya maoni ya Katiba, lakini  hiyo imeahirishwa na hivyo Ukawa kubakia na ajenda kubwa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Ukawa imepanga kuweka wagombea wa ubunge, udiwani na urais kwa kushirikiana. Wakifanikiwa hilo itakuwa ni hatua kubwa ya kimaendeleo katika siasa za Tanzania.
Kwa mujibu wa Ukawa inayoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chadema, kila  chama kitaachiwa maeneo kadhaa ya kugombea nafasi za ubunge na udiwani. Pia chama kimojawapo katika vyama hivi kitatoa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa kiti cha urais Zanzibar.

Wasiwasi
Baadhi ya watu wana shaka kubwa na uwezo wa vyama hivi kuendelea kukaa pamoja, kwa sababu ya maslahi binafsi ya vyama vyao. Chama cha siasa chochote kina melengo ya kushika dola ili kiweze kutekeleza sera na mipango yake. Hata hivyo, kwenye demokrasia kuna uwezekano wa chama zaidi ya kimoja kushika dola kwa kushirikiana, ama kwa makubaliano ya baada ya uchaguzi au kabla ya uchaguzi.
Mwaka 2010 huko Uingereza, vyama viwili vya siasa viliunda serikali ya pamoja baada ya matokeo kuonyesha kuwa hakuna chama kilichoweza kuunda serikali peke yake. Vyama vikubwa nchini humo, yaani  Conservatives na Labour  vyote havikuwa na idadi ya wabunge inayotosha kuunda Serikali.
Hivyo chama cha tatu kwa idadi ya wabunge bungeni kikaungana na Conservatives kuunda serikali ambayo ilidumu mpaka mwaka 2015. Safari hii Chama cha Conservatives kimeunda serikali peke yake. Huu ni mfano wa ushirikiano wa vyama baada ya uchaguzi.
Mwaka 2002 nchini Kenya kuliundwa ushirikiano wa vyama ili kukishinda chama cha Kanu na kuunda Serikali. Ushirikiano huo uliitwa NARC na ulihusisha wanasiasa wote wakubwa wa nchi hiyo. Umoja ule kimsingi ulikuwa ni ‘Umoja dhidi ya Moi’
Uchaguzi uliofuata kila chama kiliingia serikalini kivyake na kwa muundo mwingine kabisa wa vyama. Madhara ya umoja ule wa mwaka 2002 yalikuwa makubwa mno, kwani vurugu za mwaka 2007 zilitokana hasa na chuki za kikabila kati ya makabila makubwa kulingana na wanasiasa waliowaunga mkono.
Hapa Afrika mifano mingi ya ushirikiano baada ya uchaguzi inatokana na vurugu na uchaguzi kuibwa na yote iliishia na matokeo mabaya kwa vyama vya upinzani. MDC ya Zimbabwe ilitupwa nje na kukataliwa na wananchi baada ya kukaa madarakani na Robert Mugabe kwa miaka mitano.
Chama hicho sasa kimevunjikavunjika katika pande nne na hakina tena ushawishi. ODM ilipoteza madaraka nchini Kenya kwani ilikuwa ni rahisi  kwa wananchi na wachambuzi wa kisiasa kuhusisha masuala mabaya serikalini na uwepo wa Raila Odinga katika serikali hiyo. Pia uchaguzi wa 2013 nchini humo ukajengeka kwenye ukabila zaidi na makabili yenye watu wengi yakashinda uchaguzi huo.

Ukawa ijifunze haya
Mifano hii ndio ambayo Ukawa inapaswa kuitazama na kuichambua inapoelekea kuunda umoja kabla ya uchaguzi. Chama cha Wananchi (CUF) chenye nafasi kubwa ya kushinda huko Zanzibar kiasi cha kutohitaji kabisa Ukawa kinaweza kufutika kabisa upande wa Bara, kama hakitakuwa makini katika namna ya mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi na nafasi gani watachukua baada ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, CUF itaachiwa majimbo takribani 100, na nusu ya majimbo haya yapo Zanzibar. Hata hivyo, kwa uamuzi huu CUF itapoteza nafasi kubwa sana ya kupata kura kwa ajili ya mgawo wa wabunge wa viti maalumu na ruzuku za kuendesha chama chao.
Kwa mujibu wa Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara, chama cha siasa hupata ruzuku kutokana na moja Idadi ya kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi mkuu wa wabunge; pili  idadi ya wabunge wa majimbo.
Sifa ya kwanza ni lazima kwanza chama kipate zaidi ya asilimia  tano ya kura zote ambazo zimepigwa katika uchaguzi huo.
Hii ndiyo sifa pia ya kupata wabunge wa viti maalumu. CUF wameachiwa majimbo ya Zanzibar ambayo idadi ya wapiga kura wake hawazidi wapiga kuwa wa wilaya ya Kahama na pia imeachiwa majimbo ya Pwani ( Tanga, Lindi, Pwani na Mtwara) ambayo yana wapiga kura wachache kulinganisha na mshirika wake Chadema.
Hivyo CUF wanaweza kumaliza uchaguzi wa mwaka 2015 wakiwa na wabunge wachache zaidi wa viti maalumu kuliko wakati wowote ule na pia wakiwa hawana fedha za kuendesha chama chao.
Kwa Chadema, chama ambacho kimetumia miaka mitano kujijenga na kusambaa kila kona ya Tanzania, ushirikiano huu una faida kubwa kwa maana ya kuondoa propaganda ya udini na ukabila. Hata hivyo, kukua kwa kasi kwa chama kipya cha ACT-Wazalendo kutanyofoa kura nyingi kutoka Chadema.
Kitendo cha Chadema kutoweka wagombea nchi nzima na ikitokea ACT-Wazalendo wakaweka wagombea nchi nzima na hivyo kuwa chama kikubwa cha pili kwa idadi ya wagombea ubunge na kuweza kuokota kura nchini nzima, kunaweza kuifanya kuwa chama cha tatu kwa idadi ya kura hata kama kitapata wabunge wengi zaidi ya ACT- Wazalendo.
Hii maana yake itasababisha Chadema kuwa na wabunge wachache wa viti maalumu na vilevile ruzuku ndogo. Chama cha NCCR Mageuzi kitaendelea kuwa chama kinachosindikiza kutokana na ukweli kuwa kwa mgawanyo wa majimbo ulivyo hawatapata zaidi ya asilimia tatu ya kura. NCCR  Mageuzi inaweza kubakia na wabunge wawili tu baada ya uchaguzi mkuu. Hiki ni chama ambacho Ukawa utakifuta katika ramani ya siasa.
Hata hivyo, kwa ajili ya malengo ya nchi na kuiondoa CCM madarakani Ukawa bado ni umoja ambao ni muhimu kwa nchi. Kuendelea kuwepo kwake au la kutatokana na iwapo viongozi wa vyama watakubali madhara yaliyoainishwa katika makala haya.
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Ukawa ikiunda  serikali au la, vyama hivyo vitagombana na uchaguzi wa mwaka 2020 utakuwa na ‘hesabu’  tofauti kabisa za kisiasa. Chama kitakachotoa Rais mwaka 2015, ndicho kitakachodumu kutokana na kuwa na dola, kwa kuwa ndiyo chombo muhimu katika nchi za Kiafrika.
Mwai Kibaki wa Kenya ni mfano tosha kabisa. Ukitaka mfano nje ya Afrika, tazama nchini Uingereza ambapo chama cha Liberal Democrats kimefutika kutoka wabunge 58 mpaka wabunge wanane tu ndani ya miaka mitano. CUF wasome zaidi alama hizi kuliko chama kingine chochote.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: