Wabunge wa Bunge la Tanzania
Mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu mwaka 2015/16 katika kikao cha pili cha mkutano wa 20 wa
Bunge la 10, umetekwa na kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao, huku wabunge
kutoka vyama vya upinzani wakihakikisha wanatumia neno “Serikali
imechoka” kila wanaposimama kuchangia, huku wa CCM wakiitetea na kutamba
kuibuka na ushindi wa kishindo.
Hotuba hiyo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda
iliyozungumzia mafanikio katika kipindi cha miaka 10, ni ya kwanza kwa
Bunge la Bajeti ambalo litahitimisha shughuli za chombo hicho cha
kutunga sheria cha Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya Uchaguzi Mkuu ambao
kikatiba unatakiwa ufanyike wiki ya mwisho ya Oktoba.
Hali hiyo ya kumalizika kwa muda wa Serikali ya
Awamu ya Nne ilijionyesha dhahiri kwenye michango ya wabunge, kiasi
kwamba kila hoja ya kutetea au kubeza mafanikio ilichagizwa na maneno ya
kuponda upinzani au kuiponda Serikali kuwa imechoka, neno lililotumiwa
kwa mara ya kwanza juzi na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
Lissu.
Katika kujadili hotuba hiyo jana, kati ya wabunge
22 waliochangia mjadala wa bajeti ya ofisi hiyo hadi jana mchana, 12
walijikita zaidi katika kujipigia kampeni wao na vyama vyao, hususan CCM
na Ukawa, pamoja na kuwapiga vijembe wenzao kutoka vyama vingine.
Wengine 10 walichangia bajeti hiyo huku
‘wakichomeka’ masuala ya uchaguzi huo wa Oktoba na kutaka Serikali
itekeleze ahadi ilizotoa katika majimbo yao.
“Bunge limeanza vibaya kutokana na wabunge kuanza
kushambuliana,” alisema mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua
Nassari alipoulizwa kuhusu mwenendo huo wa mjadala.
“Wabunge warudi kwenye bajeti, waache kujadili watu na vyama,” alisema Nassari.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk Pudensiana
Kikwembe alisema, “Wabunge wanataka kujihami na majimbo yao lakini watu
watapima ni maendeleo gani yamefanyika katika kipindi cha uongozi wa
wao.”
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses
Machali alikuwa na kauli kama hiyo alipofuatwa nje ya Bunge kuzungumzia
mwenendo wa mmjadala.
“Sidhani kama ni sahihi (kujikita kwenye
kampeni),” alisema Machali ambaye alikiri kuwa mabunge mengi hutawaliwa
na hali kama hiyo wakati uchaguzi unapokaribia. “Tunachotakiwa kufanya
ni kuzungumza mambo ambayo yanahusu bajeti hii ili kuweza kuishauri
serikali mambo ya msingi ya kuzingatia.”
Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi alionya kuwa hali hiyo haiwezi kubadilisha kitu kwa kuwa uchaguzi lazima upo.
“Hakuna sababu ya kuendelea kupiga kelele kuhusu uchaguzi kwa sababu uko pale pale kwa mujibu wa Katiba,” alisema Arfi.
Mjadala huo ulitawaliwa na vijembe, mifano ya kuchekesha na hoja
za nguvu zilizoishia kwa kupondana kisiasa na kushauri wananchi wasiipe
tena fursa CCM kuongoza nchi, huku wabunge wa chama hicho tawala
wakiponda kuwa wapinzani hawataambulia kitu.
Mjadala
Mjadala huo jana ulianza kwa mbunge wa Sikonge
(CCM), Said Nkumba kuiponda Ukawa kuwa ndiyo dhaifu kwa sababu imeundwa
na vyama vinne ili kuking’oa chama kimoja, jambo ambalo alisema haliwezi
kufanikiwa. “Huwezi kwenda Ikulu wakati hujashinda uchaguzi wa
serikali za mitaa. CCM imeshinda kwa asilimia 70. Huwezi kupewa nchi
wakati hujui maendeleo yaliyopatikana kwa miaka 50 tangu nchi ipate
uhuru,” alisema Nkumba huku akiponda kuwa kauli za wapinzani kuwa Rais
Jakaya Kikwete atajiongezea muda inaonyesha jinsi walivyo na hofu.
Paulina Gekul
Mbunge wa viti maalum (Chadema), Pauline Gekul
alisema wapinzani wanavyosema serikali imechoka wana maana kuwa viongozi
wa Serikali wamechoka kufikiri, hawawezi tena kuongoza na wanatakiwa
kupumzika.
Gekul alitaja mambo saba ambayo CCM itakumbukwa
kuwa ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na
wakulima, wanakijiji na hifadhi za utalii; mauaji ya albino, unyanyasaji
katika Operesheni Tokomeza, utengaji wa bajeti hewa za maendeleo,
kushindwa kutengeneza fursa za ajira kwa vijana, kulimbikiza madeni ya
wakulima na kutopima vijiji licha ya nchi kupata uhuru miaka 50
iliyopita.
“Msiibeze Ukawa, maana Watanzania wanajua
wanachotaka. Tunaposema Serikali imechoka mnaruka tu katika viti.
Tunamaanisha kuwa mmechoka kiakili, si kimwili,” alisema.
Mbunge huyo alisema kuwa kitendo cha Serikali
kupeleka Tamisemi asilimia 17 ya fedha zilizotengwa kwa wizara hiyo,
kinaonyesha ni kwa jinsi gani Serikali haiwezi kutekeleza majukumu yake.
Mchungaji Msigwa
Mjadala huo ulifikia hatua ya uongozi wa Serikali kuelezewa kuwa ni dhaifu kiasi cha kuhatarisha hata usalama wa taifa. “Heri mhalifu kuliko kiongozi dhaifu,” alisema mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Livingistone Lusinde
Assumpter Mshama
Hamad Rashid Mohamed
Mbunge huyo alisema namba moja wa Usalama wa Taifa
nchini ni Serikali ya CCM na ili Taifa liwe salama lazima kuing’oa
madarakani. “Hii Serikali ya ajabu kabisa imechoka na tutaendelea kusema
tu. Taifa hili ni kubwa kuliko kitu chochote, mnabadilisha mawaziri
lakini kila siku mambo ni yaleyale ndio maana tunasema mmechoka.
Wananchi wajiandikishe katika Daftari la Wapigakura ili kukiondoa chama
hiki,” alisema Msigwa.
Mchungaji Msigwa alisema haiwezekani ndani ya mwaka mmoja Serikali ikataka kufanya mambo makubwa mengi wakati haina fedha, akitaja mambo hayo kuwa ni kusimamia Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitambulisho vya Taifa na kuendesha Kura ya Maoni.
Mchungaji Msigwa alisema haiwezekani ndani ya mwaka mmoja Serikali ikataka kufanya mambo makubwa mengi wakati haina fedha, akitaja mambo hayo kuwa ni kusimamia Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitambulisho vya Taifa na kuendesha Kura ya Maoni.
Livingistone Lusinde
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliamua kujibu mapigo akitumia muda wake kumrushia madongo Msigwa na kuuponda Ukawa. “Msigwa anashangaa Deni la Taifa kupaa sasa mbona
wabunge hapa tunakopa, kipi cha ajabu. Uchaguzi Mkuu ukisogezwa mbele
nchi haiwezi kulipuka kama wanavyosema Ukawa, mbona alivyokufa Rajab
Jumbe (mgombea mwenza wa Chadema 2005) uchaguzi ulisogezwa mbele na nchi
haikulipuka,” alisema Lusinde.
Assumpter Mshama
Mbunge wa Nkenge (CCM), Assumpter Mshama alijikita
zaidi katika mifano ya mambo yaliyofanywa na serikali ya Awamu ya Nne
huku akiwaponda wapinzani kuwa wanazungumza mambo wasiyoyajua.
Hamad Rashid Mohamed
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed
alilitangazia Bunge kuwa hatagombea tena ubunge, badala yake atagombea
urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ADC.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment