Jaji Augustino Ramadhani, akipiga kinanda wakati wa Ibada katika kanisa kuu la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam
Historia yake
Jaji Augustino Ramadhani alizaliwa Desemba 28,
1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya wanane
waliozaliwa kwa wazazi wake. Baba yake ni Mathew Douglas Ramadhani, raia
wa Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1962.
Watu wengi hushangaa “mkongwe” huyu kuwa na majina
mawili ya dini tofauti. Augustino (jina la Kikristo) na Ramadhani (jina
la Kiislamu). Lakini ukweli wa mambo ni kuwa yeye ni Mkristo wa dhehebu
la Anglikana na ni mchungaji wa kanisa hilo.
Elimu ya msingi aliianzia wilayani Mpwapwa Mkoa wa
Dodoma katika Shule ya Msingi Mpwapwa mwaka 1952 -1953 darasa la kwanza
na la pili. Baadaye alihamia mkoani Tabora na kusoma darasa la tatu na
la nne katika Shule ya Mingi “Town School” mwaka 1954 – 1956. Mwaka 1957
– 1958 alisoma darasa la la sita na la saba katika Shule ya Msingi
Kazel Hill (sasa inaitwa Shule ya Msingi Itetemia), kabla ya kurudi
Mpwapwa ambako alikamilisha darasa la nane mwaka 1959.
Aijiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora
mwaka 1960-1965 kwa ajili ya elimu ya kidato cha kwanza na nne pamoja na
elimu ya kidato cha tano na sita. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari
alipata fursa ya kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akianza
kusomea Sheria. Shahada hii nyeti aliisoma kuanzia mwaka 1966 hadi
alipohitimu Machi 1970.
Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu alijiunga
na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria na aliajiriwa katika
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kufanya kazi za uanasheria.
Kwa mtu mwenye shahada ya chuo kikuu enzi za miaka
ya 1970, kupanda vyeo kilikuwa kitu cha lazima. Jeshi halikuwa na
wasomi wengi kama ilivyokuwa katika sekta nyingine na kila aliyekuwa na
elimu kubwa alikuwa mtu muhimu. Ndiyo maana haikushangaza kwamba mwaka 1971 tayari
alikuwa Luteni (nyota mbili) akiwa kambi ya Mgulani na miaka sita
baadaye akahamishiwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora wakati huo akiwa
tayari ni Meja.
Kwa kuwa nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa wasomi
wa sheria, Rais wa Zanzibar wakati huo, Aboud Jumbe Mwinyi, alimwomba
na kumwondoa jeshini Jaji Ramadhani na kumteua kuwa Naibu Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), mwaka 1978.
Oktoba 1978 aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Mabadiliko mengine yakatokea tena Machi 1979 alirudishwa jeshini,
ambako hakukaa muda mrefu; akahamishiwa vitani Uganda kuendesha mahakama
za kijeshi (akiwa tayari na cheo cha Luteni Kanali).
Baada ya vita alirejea Zanzibar na kurudishwa
kwenye utumishi wa kiraia ambako Januari 1980 aliapishwa kuwa Jaji Mkuu
wa Zanzibar. Miaka tisa baadaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya
Rufaa ya Tanzania.
Alidumu katika ujaji wa Mahakama ya Rufaa kwa
miaka minne hadi alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) mwaka 1993. Alikaa NEC hadi Oktoba 2002 alipohamishiwa
Zanzibar kufanya kazi kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC) hadi Oktoba 2007.
Kati ya Novemba 2001 hadi Novemba 2007 aliteuliwa kuwa Jaji wa
Mahakama ya Afrika Mashariki. Mwaka 2007 alifikia wadhifa wa juu kabisa
kwa wanasheria wa Tanzania, alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania hadi
alipostaafu mwaka 2010. Septemba 2014 aliteuliwa na Mahakama ya Afrika
ya Haki za Binadamu yenye makao yake jijini Arusha kuwa rais wa
mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.
Nguli huyu wa taaluma ya sheria amemuoa mwanajeshi
wa ngazi ya juu, Luteni Kanali Saada Mbarouk na wamepata watoto wanne
(wawili wanafanya kazi kama wafamasia nchini Uingereza, mmoja ni
mwanasheria huko huko Uingereza na mmoja ni mwandishi wa habari hapa
Tanzania).
Mbio za urais
Jaji Ramadhani hajatangaza kuwa atagombea urais
lakini anatajwa sana ndani ya majukwaa ya kisiasa nchini. Na ile kauli
ya Rais Jakaya Kikwete kuwa wagombea wazuri hawajajitangaza inamfanya
ahisiwe kuwa mmoja wa “wagombea hao wazuri”.
Vyama vikongwe duniani vinapozidiwa na “mazonge”
ya kiutawala na vikahitaji kurekebisha mifumo yao, huwatumia watu wenye
sifa thabiti ilimradi hawatokei katika vyama hasimu. Jaji Ramadhani
aliyetumikia nchi hii tangu enzi za Tanu na CCM bila shaka alikuwa mwana
Tanu mzuri enzi hizo japokuwa kazi yake ya ujaji ilimweka kando kidogo
na kushabikia chama anachokipenda.
Lakini pia, kutumikia Serikali na Jeshi kumemfanya
awe karibu mno na CCM na mfumo wa nchi na hata nyadhifa nyingi
alizopitia katika fani ya sheria hadi kuwa Jaji Mkuu zinataka uteuliwe
na Amiri Jeshi Mkuu ambaye hadi leo ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Nguvu yake
Kati ya watu wote wanaopigiwa chapuo na kutajwa
kuwania urais kupitia CCM, ni Jaji Ramadhani pekee unayeweza kusema hana
shutuma za kukosa uadilifu na uaminifu kazini. Amefanya kazi ya ujaji
kwa mafanikio na hatukuwahi kusikia amehongwa au ametuhumiwa kuhongwa.
Sifa hii inaweza kuleta aina ya rais mstaarabu, imara, anayejiamini na
anayeweza kuchukua hatua bila kuhofia kuwa machafu yake yatamsuta.
Moja ya matatizo makuu ya Watanzania ni “ukosefu
wa haki” katika nyanja zote za maisha yao na bila shaka Jaji Ramadhani
amekuwa mtu anayesimamia utoaji na utendaji wa haki kwa kipindi kirefu.
Huyu anaweza kuwa aina ya watu wanaoyafahamu matatizo ya Watanzania kwa
kina na akiwa mara nyingi sana amekerwa nayo lakini akiwa hayuko katika
nafasi za kuyachukulia hatua sahihi kwa sababu, labda yalipaswa
kushughulikiwa na mihimili mingine ya dola. Kwa hiyo, anaweza kusimama
na kusema kwa uwazi kuwa akipewa uongozi wa nchi anajua wapi pa kuanzia.
Jambo la tatu ni kuheshimika kwa watu wa kada ya
kati. Jaji Ramadhani ni mtu anayeheshimika sana kutokana na kazi zake,
kada ya wasomi na wanazuoni inafahamu mengi kumhusu na inaweza kutumika
kupasha habari zake nzuri kwa wananchi wa chini bila kuulizwa maswali
yasiyo na majibu.
Huyu ni mtu anayeaminiwa na wafanyakazi na makundi
ya kidini. Wafanyakazi wanamwamini kwa sababu amekuwa mfanyakazi
mwenzao mahakamani na jeshini, lakini ni mfanyakazi ambaye hakuwa na
madoa mengi na hakuonesha mifano mibaya. Pia, yeye ni mchungaji wa
kanisa la Anglikana; madhehebu ya dini yanaweza kuona nchi inahitaji
kiongozi mnyenyekevu na mwenye hofu ya “Mungu” kwa dhati na hiyo inaweza
kumwongezea uungwaji mkono.
Udhaifu wake
Jambo moja linalomharibia ni kutokaa ndani ya mfumo wa CCM.
Nilieleza hapo juu kwamba Jaji Ramadhani amekuwa zaidi serikalini kuliko
ndani ya chama na nikasema inawezekana hali hiyo pia ilimsaidia, kwa
kiasi fulani, kuwa karibu na viongozi wa CCM. Lakini ukaribu huo
haukuwahi kumfanya awe mtendaji ndani ya CCM, hili ni eneo la kwanza
linalompa udhaifu wa utambulisho ndani ya chama.
Pili, yeye hafahamiki sana kwa wananchi wa
kawaida. Pamoja na kwamba amekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa miaka
minne, na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, kwa miaka mingi,
watu wanaweza kukosa kumbukumbu ya maamuzi mazito aliyowahi kufanya.
Kwamba “umewahi kuwa Jaji Mkuu lakini watu wakisaka kwenye rekodi ni
nini kikubwa hasa ulikisimamia na kulinda mhimili huo” hawakioni. Huu ni
udhaifu kwa mtu ambaye anatarajia kuwa kiongozi wa nchi.
Tatu, katika utumishi wake wa miaka minne kama
Mkuu wa Mahakama Tanzania hakuonekana kama mpambanaji mkubwa wa rushwa.
Mwalimu Nyerere alikuwa “hachukui rushwa na alipambana na rushwa kufa na
kupona”, Jaji Ramadhani naye “hakuwahi kuchukua rushwa lakini
hakupambana na rushwa kufa na kupona”. Unaweza kujionea tofauti hiyo.
Tumeshuhudia mahakama zetu zikiendelea kuwa
“sehemu ya kutoa na kupokea rushwa”, wananchi wanalalamika na
kumwandikia Jaji Mkuu kila kukicha juu ya mienendo ya majaji na mahakimu
lakini wakati wake hakuna uchunguzi mkubwa uliowahi kufanywa juu ya
mienendo hiyo na hatua thabiti kuchukuliwa. Rushwa haiondolewi kwa
kuchukiwa kwa maneno matupu bali kwa vitendo; katika uongozi wake
hatukupata kuona yeye na majaji wenzake wenye dhamana wakipambana na
rushwa kwa vitendo.
Eneo jingine la udhaifu wake mkubwa linaweza
kuangaliwa wakati akihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa NEC kati ya mwaka
1993 – 2002. Chini ya uongozi wake na wenzake kulifanyika chaguzi mbili,
ule wa mwaka 1995 na ule wa mwaka 2000 zote akishinda Rais Benjamin
William Mkapa.
Baadhi ya waangalizi wa ndani na nje ya nchi
walitoa tathmini zao zikionyesha kuwa chaguzi zile hazikuwa huru na za
haki na kwamba vyombo vya dola vilitumika waziwazi kuisaidia CCM na
viliizidi nguvu NEC. Hii ina maana kuwa Jaji Ramadhani amewahi
kushuhudia demokrasia ikikandamizwa wakati ana dhamana kubwa ya
kusimamia uchaguzi na hakuchukua hatua zozote wala kuonyesha msimamo wa
kutenda haki.
Kwa upande mwingine, yeye mwenyewe, kwa mikono
yake, amewahi kushiriki katika ukandamizaji wa demokrasia (si kutazama
tu, alishiriki!). Hukumu ya Mahakama ya Rufani dhidi ya mgombea binafsi
(hoja na kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila) ililaumiwa sana na
wapigania haki wengi, mashirika binafsi na hata majukwaa ya kidini na
baadhi ya wanasheria waliishangaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ikitoa
hukumu ambayo inaifanya mahakama kukwepa wajibu wake wa kusimamia haki
hadi ionekane inatendeka.
Katika hukumu hiyo, Jaji Ramadhani na wenzake
walijaribu kuzunguka mbuyu wakikwepa kuiudhi Serikali. Sehemu ya
hitimisho la hukumu hiyo (tafsiri ni yangu) ilisema: “….Kwa upande wetu,
tunasema kwamba suala la mgombea binafsi linapaswa kushughulikiwa na
Bunge ambalo lina mamlaka ya kubadilisha Katiba (na uwezo huo) siyo wa
mahakama ambazo, kama tulivyoeleza, hazina mamlaka hayo. Uamuzi wa
kuanzisha au kutoanzisha mgombea binafsi unategemea mahitaji ya kijamii
ya kila taifa kutokana na hali halisi ya historia yake. Kwa hiyo, suala
la mgombea binafsi ni la kisiasa na si la kisheria……..”
Hadi sasa baadhi ya wanasheria nguli, nilioongea
nao, wanasisitiza kuwa, walau Jaji Ramadhani na wenzake hata kama
wangekuwa wanajikosha kwa serikali, wangeweza kuuma na kupuliza na
kuhitimisha kuwa “suala la mgombea binafsi ni haki ya kikatiba na kwamba
wanaiamuru Serikali isimamie utekelezaji wake”, na kisha Serikali ndiyo
ingetumia taratibu zake kuliarifu Bunge lifanye kazi yake.
Katika dunia ya sasa ambapo mihimili ya dola
inafanya kazi yake, mahakama yoyote ina wajibu wa kuhakikisha sheria
zote zinazowanyima haki wananchi zinabatilishwa. Haiwezekani nchi
inakuwa na sheria inayokiuka haki za raia halafu mahakama inatoa hukumu
ya kusema Bunge liamue litakavyo “hata kwa jambo linalovunja haki za
raia”. Hii ni rekodi nyingine inayoonesha kuwa taswira ya Jaji Ramadhani
imewahi pia kutumika vibaya kwa kufanya maamuzi ambayo yanakinzana na
uzito wa dhamana aliyowahi kupewa.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Jaji Ramadhani anaweza kupitishwa kwa sababu ya
taswira yake ya uadilifu, usafi na kuchukia rushwa. CCM ya sasa,
iliyochofuka sana, inahitaji mgombea msafi asiye na madoa mengi ili awe
na uwezo wa kuwashughulikia bila haya wale wote wanaotumia ofisi za umma
kujinufaisha, ikiwa atapigiwa kura na kuwa Rais. Ikumbukwe kuwa huyu ni
mwanataaluma nguli na askari mstaafu wa cheo cha juu jeshini na anao
uwezo wa kusimamia mambo, labda aamue kushindwa kimakusudi.
Lakini, pia, mtu wa namna hii atajenga taswira safi na kupitia
upya malengo na mustakabali wa chama hicho kuona kama anaweza
kukirudisha katika malengo yake ya miaka ya 1970, ya kuwatetea wakulima
na wafanyakazi ambayo kwa sasa yamekufa.
Kwa sababu hana makundi ndani ya CCM, hili
linaweza kumbeba. Kwamba CCM inatafuta mtu ambaye atayafanya makundi
makubwa yanayogombana ndani ya chama hicho yamheshimu; ikikosea kumpata
mtu huyo itaparaganyika na kama mtu huyo atakuwa ni Jaji Augustino
Ramadhani maana yake makundi hayo yatatishwa na heshima/uadilifu wake na
kuanza kumuunga mkono mara moja.
Nini kinaweza kumwangusha?
Kitisho kikubwa kwa wahafidhina ndani ya CCM ni
“ugeni” wa Jaji Ramadhani katika chama chao. Pamoja na kuwa kwake karibu
na Serikali, jeshi na hata kufahamiana na viongozi wengi wa CCM,
hakuwahi kuwa mmoja wa wahafidhina na wale wanaojidai “CCM ni mali yao”.
Ikiwa hawa wenye chama watamwekea ngumu, ataanguka.
Jambo jingine ni kwamba ikiwa uongozi wa juu wa
CCM utaona yeye ni chaguo la chama hicho, yeye na uongozi wanaweza
kukumbana na kisiki kikubwa cha makundi yenye pesa kutumia kila mbinu
ili aenguliwe. Watu wa namna yake wanaweza kuonekana kama “watakaotia
mchanga kwenye kitumbua cha mabosi, kilichoandaliwa muda mrefu” na dawa
yake ni kumpiga fitina kwa nguvu za pesa na kila ushawishi hadi
andolewe.
Asipopitishwa (Mpango B)
Jaji Ramadhani amekwishastaafu mbio za utendaji wa
umma, lakini yeye ni mmoja wa wachungaji muhimu wa kanisa la Anglikana.
Nilipoongea na ofisa mmoja wa juu wa kanisa hilo alinijulisha kuwa
huenda miaka michache ijayo mkongwe huyu akatawazwa pia kuwa askofu
kwenye moja ya dayosisi za kanisa hilo. Kwa hivyo, kama hatateuliwa
kuwania urais naona ana kazi ya kudumu ya “kuchunga kondoo wa Bwana
wasipotee”!
Hitimisho
Aina ya watu kama Jaji Ramadhani ni kitisho
kikubwa kwa makundi yaliyojitangaza muda mrefu na kujisuka vilivyo
kunasa tiketi ya urais kupitia CCM. Mtu mwadilifu, mwenye rekodi nzuri
kiutendaji, aliyepitia jeshini, aliyekuwa jaji wa mahakama kuu hadi jaji
mkuu na ambaye sasa anatajwa kugombea urais, lazima tu atatisha.
Atatisha kwa sababu ya rekodi zake za kuvutia na kukosa mawaa na kashfa
wakati anafanya kazi kwenye sekta ambayo kama angependa angekula rushwa
kila siku, lakini alikataa.
Hakika, mzee huyu asidharauliwe hata kidogo.
Huenda watu wa namna yake ndiyo kimbilio la CCM kwa sasa, katika wakati
ambao chama hicho kinapaswa kufanya maamuzi magumu ili walau kiokoe
sehemu iliyobaki katika nyumba inayoungua.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment