Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi akiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya
Kikwete akiwasalimia wakazi wa Dar es Salaam waliojitokeza kumlaki
katika Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam jana. Rais Nyusi yuko nchini kwa
ziara rasmi ya siku tatu.
Ziara ya kwanza
ya Rais wa Msumbiji, Filipe Nyussi nchini imefanikisha kusainiwa kwa
mkataba wa kuondoa malipo ya viza kwa wanadiplomasia, wafanyabiashara na
wananchi baina ya nchi hizo mbili.
Mkataba huo mpya ulisainiwa jana kati ya Waziri wa
Mambo ya Ndani wa Msumbiji, Jaime Basilio Monteiro na Waziri wa Mambo
ya Ndani wa Tanzania aliyewakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo kati ya Rais Nyussi na mwenyeji wake, Jakaya Kikwete, Ikulu jijini hapa.
Akizungumza kuhusu makubaliano hayo, Membe alisema
kuanzia sasa wananchi wa pande zote mbili watafaidika na uhusiano mwema
uliojengwa kwa muda mrefu na fursa za biashara kutoka nchi hizi. “Hakutakuwa tena na viza kwa Watanzania
wanaokwenda Msumbiji. Awali, walilazimika kulipa Dola za Marekani 900
(zaidi ya Sh1.8 milioni) kwa muda wa siku 30 wakati wao walikuwa
wanalipa Sh10,000 kwa siku 90. Baada ya mkataba huu, hakutokuwa tena na
malipo hayo,” alisema Membe.
Waziri Membe alifafanua kuwa mkataba huo umeondoa
pia malipo ya viza kwa muda huo kwa wafanyabiashara, wanadiplomasia
pamoja na wananchi wa kawaida lakini wanafunzi wamepewa kipaumbele cha
pekee kwani hawatotakiwa kulipa kwa muda wote wa masomo yao.
Alisema uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi mbili
hizi, umechangia kwa kiasi kikubwa kufikia uamuzi huo na katika siku
zijazo, wanatarajia kufanya mazingira ya kuvuka mipaka yasiwe kikwazo
kwa maendeleo ya wananchi wake.
Rais Nyussi aliwasili nchini jana na atafanya
ziara ya siku tatu itakayomfikisha pia Zanzibar ambako atazungumza na
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohammed Shein
kabla ya kuelekea Dodoma ambako atatembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom)
kabla ya kulihutubia Bunge.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment