 
  
            
Profesa Kitila Mkumbo
WASIFU
Umri: 44
Elimu: Shahada ya Sayansi ya Elimu (BSC Education), Shahada ya Uzamili (M.A) Saikolojia na Shahada ya Uzamivu (PhD) Saikolojia.
Kazi: Profesa Mshiriki Shule ya Elimu (Duce).
Historia yake
Profesa Kitila Mkumbo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu 
cha Dar es Salaam na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa. Alizaliwa Juni
 21, 1971 katika Kijiji cha Mgela wilayani Iramba, Singida. (Atatimiza 
miaka 44 Juni 2015). Profesa Mkumbo hakuwa na bahati ya kulelewa na 
wazazi, hivyo alisomeshwa kwa misaada ya ndugu na wasamaria wema.
Alisoma katika Shule ya Msingi Mgela iliyoko 
wilaya ya Iramba kati ya mwaka 1981-1987 kisha akajiunga Shule ya 
Sekondari Mwenge (Singida) na kusoma kidato cha kwanza hadi cha tano 
mwaka 1988-1991 na elimu ya Juu ya Sekondari akaipata pale Shule ya 
Sekondari Pugu kati ya mwaka 1992-1994 akijikita katika mchepuo wa PCB 
(Fizikia, Kemia na Bailojia).
Baada ya kuhitimu kidato cha sita alifanya kazi ya
 kuvua samaki katika Bwawa la Mtera huko Iringa kwa sababu ya kuwa na 
hali mbaya ya kiuchumi na baadaye alipata nafasi ya kwenda kujiunga na 
mafunzo ya polisi kwenye Chuo cha Polisi (CCP) Moshi kwa muda wa miezi 
miwili lakini alikatisha mafunzo baada ya kuchaguliwa kujiunga Chuo 
Kikuu.
Profesa Mkumbo alihitimu shahada yake ya kwanza 
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1999 akisomea Sayansi ya Elimu
 na kupata daraja la kwanza, akaanza kazi hapo hapo Chuo Kikuu kama 
Ofisa Utawala, aliifanya kazi hiyo kwa miaka minne (1999 – 2003) na 
wakati anafanya kazi aliendelea kusoma shahada ya uzamili (M.A) akibobea
 katika Saikolojia, alihitimu shahada hiyo mwaka 2002.
Mkumbo ni mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri 
katika shahada ya uzamili na baada ya kufundisha Chuo Kikuu kwa miaka 
michache alipewa udahili katika Chuo Kikuu cha Southampton kilichoko 
nchini Uingereza ambako alitunukiwa shahada ya uzamivu akibobea pia 
katika saikolojia, hii ilikuwa ni mwaka 2008.
Mwaka 2010 hadi 2012 amekuwa Makamu Mwenyekiti wa 
Udasa (Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na 
Mwenyekiti wa Udasa Oktoba 2014 hadi sasa.
Pia amekuwa mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia 
na masomo ya Mtaala katika UDSM 2009 – 2012, Mhadhiri Mwandamizi kuanzia
 2011 – 2014,
 Mkuu wa Kitivo cha Elimu Duce na hatimaye Profesa Mshiriki kuanzia Julai 2014.
Mkumbo alianza siasa kama mwanachama wa CCM, 
baadaye alijiunga Chadema kawa mshauri muhimu wa chama hicho, pia akiwa 
mjumbe wa Kamati Kuu. Mwaka jana (2014), Profesa Mkumbo alitangaza 
kukihama chama chake cha zamani na kujiunga na chama kipya, ACT – 
Wazalendo, akiwa na rafiki yake wa siku nyingi, Zitto Kabwe. Hata katika
 chama hiki kipya yeye amekuwa mshauri mkuu. Watu nilioongea nao kutoka 
ndani ya ACT wanasisitiza kuwa Mkumbo ana mchango mkubwa na unaoonekana 
anapokuwa katika taasisi yoyote ile.
Profesa Mkumbo amekwishafanya tafiti zaidi ya 18 
na zimechapishwa katika majarida ya kitaaluma ya kimataifa, 
amekwishaandika vitabu takribani vitatu, ameoa na ana watoto watatu.
Mbio za ubunge
Profesa Mkumbo hakuwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote hapa
 Tanzania, muda wake mwingi amejikita katika masuala ya kitaaluma na 
ushauri wa mikakati ya kisiasa. Japokuwa alipokuwa mwanachama hai wa 
Chadema alifanya harakati nyingi katika jimbo la Iramba (jimbo 
linaloongozwa na Mwigulu Nchemba wa CCM) na amewahi kuingia kwenye 
misukosuko mingi na hata kufunguliwa kesi ya kisiasa kwa sababu ya 
harakati zake.
Mtu yeyote yule anatambua kuwa harakati zile za 
Mkumbo jimboni Iramba (ambazo sina hakika kama amezisitisha kutokana 
kuhamia ACT) lazima zilikuwa na nia ya kugombea ubunge kwenye uchaguzi 
mkuu wa mwaka huu au labda miaka mingine mitano ijayo. Ninachoamini ni 
kuwa, Mkumbo nadhani anajiandaa kuwa mbunge miaka ya mbele na huwenda 
bado ndoto hizo ziko kwenye damu yake.
Mbio za urais
Profesa Mkumbo hajatangaza nia ya kutaka urais wa 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ila sehemu kubwa ya wanachama wa ACT 
nilioongea nao walimtaja kama mmoja wa wanachama wa ACT wenye sifa zote 
muhimu za kuwa Rais wa nchi ikiwa chama hicho kitaamua kuweka mgombea 
urais katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Nilipomuuliza yeye mwenyewe aliniambia kuwa ana 
mipango ya muda mrefu sana ya kisiasa na kwamba ataitekeleza kwa kadri 
alivyoipanga bila kufuata mipango na matakwa ya watoa maoni juu yake. 
Kwa hiyo, Profesa Mkumbo naye anachambuliwa kwa sababu ana sifa, vigezo 
na uwezo wa kuwa rais wa nchi, hata kama yeye mwenyewe hana mipango hiyo
 maana hatujui nini huwatokea viongozi mbalimbali na wakaweza 
kubadilisha mipango yao muda wowote mbele ya safari.
Nguvu zake
Sifa na nguvu ya kwanza ya Profesa Mkumbo ni kuwa 
kijana na msomi mahiri. Pamoja na kuwa wasomi wengi wanapewa madaraka na
 wanavurunda kama vile hawakwenda shule, bado mataifa yote duniani 
hayakwepi wala kukimbia dhana ya kuongozwa na watu walioelimika maana 
kuna wasomi wengi tu ambao ni waadilifu katika kazi zao, mmoja wao ni 
Profesa Mkumbo.
Ukiniuliza, mmoja kati ya wasomi wanaojua majukumu
 yao na wanayasimamia sana, nitakwambia Profesa Mkumbo ni mmoja wao. 
Nguvu na sifa vina maana kubwa sana kwa mtu ambaye anafikiri au 
anafikiriwa kuwa rais wa nchi.
Lakini jambo la pili, yeye ni mwanademokrasia 
thabiti na anayependa demokrasia iwe katika vitendo. Msomi huyu ni mmoja
 wa watu wanaoamini katika kujenga hoja na wanaopenda hoja 
zishindanishwe na zijadiliwe kwa uwazi na kisha hoja yenye mashiko ndiyo
 ipitishwe.
Ukitembelea ukurasa wake wa “Facebook” utaona watu
 wanaandika jambo lolote na humuoni akigombana nao, anapingwa waziwazi 
na wakati mwingine anatukanwa lakini anaacha uhuru wa wanaompinga na 
kumtukana uendelee. (Mimi binafsi nimekuwa sipendi mtu anitukane au 
anidhalilishe kwenye mitandao, napenda kupingwa kwa hoja na si kutukanwa
 na nakumbuka kila aliyenitukana niliishia kumuondoa miongoni mwa 
marafiki).
Jambo la tatu ambalo ni nguvu na sifa ya Profesa 
Mkumbo ni kubahatika kuwa kiongozi kila alipokaa, kusoma, kufanya kazi 
n.k. Amebahatika kuwa kiongozi tangu akiwa mdogo, nidhamu na kuwajali 
wenzake viliwavuta watu waliomzunguka kumtumia yeye awe mwakilishi wao. 
Amekuwa “kiranja” tokea akiwa Shule ya Msingi, Sekondari na Sekondari ya
 Juu. Uwezo huu wa kiuongozi uliendelea hata alipokuwa Chuo Kikuu (UDSM)
 kwani alichaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso) kati ya 
mwaka 1998 – 1999.
Watu nilioongea nao kuhusu uongozi wa Mkumbo 
alipokuwa Daruso wameniambia alikuwa na karama za kipekee. Mmoja ambaye 
hivi sasa ni kiongozi mkubwa CCM na aliwahi kumpinga Mkumbo walipokuwa 
Chuo Kikuu, amenieleza kuwa Mkumbo alikuwa na ushawishi mkubwa kila 
akisimama mbele ya wanafunzi  na mmoja wa marais wa Daruso waliovuka 
vikwazo vya kupinduliwa.
Udhaifu wake
Nini kinaweza kumfanya asipitishwe
Nini kinaweza kumwangusha?
Udhaifu wake
Moja ya mambo ambayo nayatazama kama udhaifu 
mkubwa wa Profesa Mkumbo ni uthubutu unaopita kiasi. Binadamu 
waliofanikiwa huthubutu kufanya mambo kadha wa kwadha lakini uthubutu 
kwa kiwango kisicholeta madhara kulingana na mahali walipo. Jambo hili 
halifanywi na Mkumbo na mara kadhaa amethubutu kufanya mambo 
yaliyowagutusha wenzie.
Mathalani, alipokuwa mwanachama wa Chadema alikiri
 kuhusika katika kuandaa waraka uliopewa jina maarufu la “waraka wa 
mapinduzi ndani ya Chadema”. Waraka ule ulikuwa ni moja ya mikakati ya 
msomi huyu kumpigia chapuo rafiki yake wa siku nyingi “Zitto Kabwe” ili 
ajiandae kuongoza chama hicho kupitia kwenye uchaguzi uliokuwa ukifuata.
 Waraka wa Kitila na wenzake ulitafsiriwa kama njama za mapinduzi ndani 
ya chama, usaliti na “kitu kisichofaa”.
Uthubutu huu wa Kitila ungewezekana sana kama 
angekuwa anafanya kazi katika vyama vikubwa mno duniani, siyo hapa 
Afrika Mashariki, tena nchini Tanzania. Lazima tukubali kuwa vyama vya 
kiafrika vimejijenga katika mifumo migumu sana kuingilika kidemokrasia 
na mara nyingi vina shida kwenye eneo hilo, ndiyo maana nilishtushwa na 
kujua kwamba Kitila amekubali kuhusika na waraka ule wakati anatambua 
kuwa yuko Afrika ambako demokrasia inapiganiwa kwa matakwa ya walioko 
madarakani kwa wakati husika.
Kwa siasa za Afrika, hata huko ACT ambako Kitila 
ni mwanachama leo hii, ukijaribu kuandaa waraka kama ule wa Chadema, 
nako anaweza kuonekana kama msaliti, mfanya mapinduzi, mhaini n.k. Ndiyo
 maana nasisitiza kuwa uthubutu huu unaopitiliza ni tatizo kubwa sana 
kwake na kwa watu waliomzunguka na tamaduni zao. Hata akiwa rais wa nchi
 atazungukwa na watu mbalimbali, aliowakuta na watakaomkuta, atakuwa na 
jukumu la kufanya mambo kwa uthubutu wa viwango vinavyokubalika ndani ya
 taasisi aliyomo kuliko “kuthubutu kulikovuka mipaka” ambako kunatazamwa
 kama uhaini kwa tamadani na demokrasia ya Afrika.
Lakini kuthubutu huku kulikopitiliza ndiko pia 
kumemfanya Mkumbo mara kadhaa atofautiane sana na menejimenti ya Chuo 
Kikuu cha Dar es Salaam kwenye mambo kadha wa kadha. Ubishi na 
kutokukubali mambo kirahisi au kutokukubaliana na mazingira na tamaduni 
za mahali ulipo, ni mambo ambayo yanamgharimu sana na nayatazama kama 
udhaifu utakaoendelea kutishia ustawi wake kisiasa.
Nini kinaweza kumfanya asipitishwe
Moja ya masuala yanayoweza kumfanya Profesa Mkumbo
 apitishwe na ACT kugombea urais wa Tanzania ni kwa sababu ya 
“umashuhuri”. Umaarufu wa Mkumbo umetokana na nafasi na fursa ya 
kuonekana mara kwa mara katika shughuli za kitaifa za Chadema (wakati 
akiwa mwanachama), pia  yeye ni mmoja wa Watanzania waliowahi kushiriki 
katika mijadala mingi ya kitaifa na ambayo imekuwa ikioneshwa moja kwa 
moja katika vyombo vya habari kwa hisani ya Udasa na vyombo binafsi.
Sehemu kubwa ya Watanzania wanaofuatilia habari 
wanaweza kuwa wanamfahamu Mkumbo kwa namna moja au nyingine. Kwa sababu 
ACT ni chama kipya na kinahitaji kujikuza na kwenda juu kisiasa, nadhani
 kitahitaji mtu wa namna yake ambaye akipelekwa kwa wananchi, 
hawatauliza huyu ni nani, katokea wapi n.k.
Lakini pia, Mkumbo anaweza kupitishwa na ACT 
kugombea urais kwa sababu ya uzoefu wake wa kumudu mazingira magumu na 
majukumu mengi, achilia mbali uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja 
majukwaani. Mkumbo amemudu mambo mengi tangu akiwa chuo kikuu, kwa mfano
 kumudu kuongoza Daruso na kisha akapata daraja la kwanza katika shahada
 yake siyo jambo dogo. Mimi nimekuwa kiongozi wa Daruso na sikudhani 
kama kiongozi wa Daruso anaweza kupata “First Class”, Uongozi ule ni 
kushughulikia matatizo ya wanafunzi kila kukicha huku vikao vya 
menejimenti vya chuo vinavyoamua masuala ya wanafunzi vikiendelea kila 
kona na unapaswa kuwapo kote huko. Pia kuongoza Udasa, Duce, na timu za 
kiushauri katika mipango na mikakati ya Chadema na baadaye ACT. Mtu 
anayemudu majukumu mengi namna hii ndani ya ACT anaweza kuwa Profesa 
Kitila pekee na huenda chama hicho kikahitaji mgombea urais anayemudu 
kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
Nini kinaweza kumwangusha?
Ikiwa ACT itakuwa na mwanachama mwingine ambaye 
ana sifa kumshinda Profesa Kitila (si kwa maana ya elimu tu), anaweza 
kabisa kupewa nafasi hii ya kugombea urais na Mkumbo akasaidia katika 
masuala mengine ya mikakati. Hii ndiyo sababu pekee ambayo inaweza 
kuzorotesha ndoto ambayo Mkumbo anaotewa, kwamba ana sifa, uwezo na 
vigezo vya kuongoza Tanzania.
Mipango mingine iwapo hatachaguliwa
Hitimisho
Mipango mingine iwapo hatachaguliwa
Mipango mitatu hivi inaweza kufuatwa na Profesa Mkumbo ikiwa hatapewa kazi ya kupeperusha bendera ya ACT kwenye urais mwaka huu:
Mpango wa kwanza ni kuendelea kuwa mhadhiri wa 
Chuo Kikuu, kazi ambayo anaifanya hadi sasa kwani yeye ni mmoja wa 
wataalamu wachache waliobobea na wenye uwezo mkubwa katika eneo la Elimu
 ya Saikolojia hapa nchini.
Mpango wa pili ni kuendelea kusaidia vitengo vya 
upangaji mikakati ndani ya chama kipya cha ACT Wazalendo ambacho naamini
 kwa uchanga wake kinahitaji wapanga mikakati wazoefu ili kukifanya 
kisidumae na labda kufa.
Na mpango wa tatu ni kuendeleza mchango wa ukuzaji
 wa fikra katika jamii ya Watanzania ambayo ina matatizo makubwa katika 
kufanya siasa za kuvumiliana na kukubali changamoto mpya.
Hitimisho
Safari ya kisiasa ya Profesa Mkumbo inaweza 
kuathiriwa na ukuaji au uzorotaji wa Chadema na Ukawa. Kwa sababu ni 
mwanachama wa ACT na kwa kusema ukweli, ukuaji wa ACT kwa kiasi kikubwa 
utategemea sana na uzorotaji wa Chadema, ndiyo kusema kuwa ukuaji wa 
Chadema kwa kasi yoyote unaweza kuathiri safari ya kisiasa ya ACT na 
Prof Kitila mwenyewe.
Kwa mfano, hata kama ikitokea Profesa Mkumbo 
akagombea urais wa Tanzania, ikiwa mgombea wa Ukawa atakuwa na nguvu 
kubwa kwa wananchi, Mkumbo na ACT hawatakuwa na fursa nzuri tena, labda 
mpaka uchaguzi mwingine.
Pamoja na yote hayo, namtakia kila la heri “rafiki
 yangu” Profesa Kitila Mkumbo katika kufikia safari yake kisiasa na kiu 
ya mabadiliko ya Tanzania afikiriayo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment