
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Baadhi ya wabunge wamemtaka Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, kuwa mkweli kuhusu kuwasafisha viongozi watuhumiwa wa Escrow na
Operesheni Tokomeza, badala ya ‘kuhadaa’ kuwa wanaendelea kuchunguzwa.Waziri Mkuu akihitimisha mjadala wa bajeti yake juzi mjini Dodoma,
alisema Ikulu haijawasafisha viongozi hao kwa vile wanaendelea
kuchunguzwa. Akichambua maelezo ya Pinda, Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi),
Felix Mkosamali, alisema Watanzania wanatakiwa kumshangaa kiongozi huyo
kwa kutolieleza taifa ukweli.
Waliosafishwa na Ikulu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Profesa
Sospeter Muhongo. Wengine ni mawaziri waliowajibika kutokana na kashfa ya Tokomeza,
Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani); Balozi Khamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa).
Wabunge hao waliwajibishwa na Bunge kwa kushindwa kusimamia
operesheni hiyo na kutaka wawajibike kwani ilisababisha vifo,
udhalilishaji, mateso kwa watu na uharibifu wa mali. Mwingine aliyelazimika kujiuzulu katika sakata hilo ni Dk. David
Mathayo David (Mifugo na Uvuvi), ingawa Bunge halikumuwajibisha.
Mkosamali alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, vyote viko
chini ya Ofisi ya Rais (Ikulu), haviwezi kufanya kazi kwa kupingana. “Kama Ikulu imetoa ripoti kuwa ni wasafi, hakuna cha kuwachunguza
zaidi kwa vile taasisi hizi zinafanya kazi pamoja na bosi wao ni Ikulu,”
alisema na kuongeza: “Inabidi kushangaa maelezo haya yanayotolewa ya kulipotosha Taifa.
Sheria inaelekeza kuwa Sekretarieti ya Maadili ikiwahoji viongozi,
ipeleke ripoti na mapendekezo yake Ikulu, na yamepelekwa.Wameonekana ni
safi, unasemaje wanachunguza zaidi.”
Alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitoa taarifa
ya kamati ya uchunguzi kwa niaba ya Rais, hivyo kusema kuwa kuna taasisi
nyingine ndani ya Ikulu zinaendelea na uchunguzi, ni jambo la
kushangaza. “Tungeelezwa na Ikulu maoni na mapendekezo ya Sekretarieti ya
Maadili, kwa vile hatujaambiwa kilichoko kwenye ripoti yake. Lakini
Sefue pia awafahamishe wananchi, hicho alisema ni cha Kamati ya Rais na
ya Makatibu Wakuu, mapendekezo ya sekretarieti hiyo yako wapi?”
Mkosamali alishauri kuwa kwa vile hizi ni zama za uwazi, sheria
zifanyiwe marekebisho ili zitoe muda maalum kwa Rais kutangaza ripoti na
mapendekezo ya sekreterieti ili kuongeza uwazi.
GODBLESS LEMA
Akizungumzia hatua ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Arusha Mjini
(Chadema), Godbless Lema, alisema wamesafishwa kwa vile anachosema Sefue
ndizo taarifa za Ikulu. “Ukisema hajawasafisha unategemea nani mwingine azungumzie habari
na ripoti za tume hizo zilizoteuliwa na Rais na kupeleka mapendekezo
Ikulu. “Ni Sefue ndiye Ikulu na Ikulu ndiyo yeye,” alisema.
Alisema Maswi amesafishwa kwa kuwa ndiye aliyeandika barua fedha
zitolewe kutoka Benki Kuu (BoT), ukisema anachunguzwa zaidi na nani
mbona kila kitu alichofanya kinafahamika? Ikulu inawafahamu wote
waliochota fedha kwenye Benki ya Stanbic na kwingineko mbona
hawajatajwa?” alihoji na kuendelea: “Kusema wanaendelea kuchunguzwa ni mchezo wa kisiasa na kufunika kombe mwanaharamu apite au kumaliza mambo kimya kimya.”
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment