Askofu Mkuu wa Kanisa la GMCL-Mbeya, Nabii David Mpanji (kulia)
akimuombea Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alipohudhuria ibada
maalumu ya harambee ya kuchangia vifaa vya redio ya kanisa hilo jijini
Mbeya juzi.
Askofu Mkuu wa Kanisa la General Mission
Center Limited (GMCL) la jijini hapa, Nabii David Mpanji juzi
alimkabidhi mafuta ya upako, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba
kwa ajili ya kung’arisha nyota yake katika harakati zake za kuwania
urais.
Nabii Mpanji alisema mafuta hayo yanaashiria
ufalme na utawala na kusisitiza kwamba kitendo hicho ni kudhihirisha
kuwa Nchemba, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, anafaa kuliongoza
Taifa.
Tukio hilo lilifanyika kwenye ibada maalumu
iliyoambatana na harambee ya kuchangia vifaa vya redio ya kanisa hilo
iliyoendeshwa na Nchemba na Sh53 milioni zilipatikana.
Alimtaka Nchemba kutamka nia yake ya kugombea
urais mbele za watu, huku akisisitiza kuwa Taifa linahitaji mtu
anayeweza kusimamia wananchi wenye kipato cha chini na kumtaja mbunge
huyo wa Iramba Magharibi kuwa amethubutu kufanya hivyo.
“Mimi nasema wazee wasikuumize kichwa, hata Biblia
inasema fahari ya wazee ni mvi zao lakini fahari ya vijana ni nguvu
zao. Tunahitaji Watanzania wazalendo na jasiri ambao wanaweza kusema
bila kuogopa kama wewe (Nchemba),” alisema. Akizungumza katika ibada hiyo, Nchemba
aliwashukuru Watanzania wenye imani naye na kubainisha kuwa muda ukifika
atasema nia yake.
“Imebaki kitambo kidogo nitasema kwani mimi ni
kiongozi wa chama, hivyo natakiwa kufuata taratibu na kanuni cha chama,
nawaomba mvute subira kidogo nitasema tu,” alisema.
Nchemba alisema upako huo ni dalili tosha za
Watanzania kutambua mchango wake katika kuwatumikia na yeye
hatawaangusha... “Tutavuka mto tukifika mtoni.”
Mwigulu ambaye aliongozana na waimbaji maarufu wa
nyimbo za Injili akiwamo Boniface Mwaitege na Moses Makondeko, alisema
katika suala hilo (la urais) anamtegemea sana Mungu.
Aliwataka wananchi kuwa na uchungu na nchi yao kwa
kutanguliza uzalendo kwani ni vigumu kupata kiongozi mzalendo katika
Watanzania wasio kuwa na uzalendo.
Akisoma risala mchungaji wa kanisa hilo, Aquina
Mhanze alisema mahitaji ya kanisa hilo ni Sh200 milioni kwa ajili ya
kukamilisha vifaa vya redio na ofisi na kwamba kwa sasa kuna Sh15
milioni.
Alisema kuwa kati ya fedha hizo, Sh150 milioni ni
kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya redio na Sh50 milioni kwa ajili ya
ununuzi wa vifaa vya redio.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment