Ukunga ni taaluma muhimu katika kujenga maisha bora ya jamii kwa sababu
ndiyo inayohakikisha usalama wa mama na mtoto kuanzia anapobeba mimba,
kujifungua na kuelimisha juu ya lishe, chanjo na uzazi wa mpango.
Jumanne wiki hii ilikuwa Siku ya Ukunga Duniani.
Ni siku ambayo wakunga wa Tanzania waliungana na wenzao duniani
kutafakari juu ya kazi zao. Ni tafakari ambayo pia iliihusisha jamii
nzima kwa sababu inahusika.
Mkunga ni mwanataaluma mwenye elimu ya kuhakikisha
mama anajifungua salama na wote wanaendelea na afya njema.Kwa kawaida
mkunga ndiye hasa anayeshuhudia dakika ya kwanza ya maisha ya mtoto
mchanga anapotoka duniani. Kwa maana hiyo mkunga anafanya kazi ngumu sana ya kuhakikisha maisha ya mtoto mchanga yanakuwa bora.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Wakunga
Nchini, Agenes Mtawa anasema kuwa wamekuwa wakisherehekea siku hiyo Mei
5, kila mwaka. Anasema hapa nchini ilikuwa ni siku ya wakunga
kukaa pamoja na kutafakari hali halisi ya kazi zao, wako wapi na
wanakwenda wapi katika kuhakikisha wanapunguza vifo vya mama na watoto
vinavyotokana na matatizo ya uzazi.
Mtawa anasema kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Mkunga kwa maisha mazuri ya baadaye.”
Anasema uzito wa kauli hii ni kwamba mtoto
akizaliwa akiwa na afya njema, mama akijifungua kwa kupata huduma
stahiki za mkunga mwenye weledi, inategemewa mtoto huyo awe kiongozi wa
baadaye. Lakini mtoto akizaliwa bila ya kupata huduma stahiki kutoka
kwa mkunga mwenye weledi, anaweza kupata matatizo ya kuchelewa kulia au
kutopumua vyema. Siyo hivyo pekee, anakuwa na matatizo baadaye kwa hiyo
kauli mbiu inaangalia utoaji mzuri wa huduma ili kuweza kuendeleza
kizazi kizuri chenye akili timamu hapo baadaye na ndiyo malengo ya
kaulimbiu.
Anasema kauli mbiu pamoja na siku ya wakunga
imeanza mwaka 1991 kwa kukaa wakunga na kutafakari vifo vya watoto
wachanga na wajawazito, vimepungua au vimeongezeka na kwa nini. Ni mwaka
wa 14 kwa sasa wakunga wanasherekea siku yao. “Tumekuwa tukisherehekea
siku yetu kila mwaka na kuna kuwa na kauli mbiu tofautitofauti na
hulenga katika afya ya mama na mtoto.
“Kumekuwa na mabadiliko kiasi katika kupunguza
vifo na kuboresha huduma bora ya afya ya mama na mtoto, ili kuweza
kupunguza vifo vya kinamama na watoto,” alisema Mtawa.
Mtawa alisema kuwa, kwa sasa kuna changamoto kubwa
ya kuwa na wakunga wachache kwa sababu mjamzito akifika kupima ujauzito
ana huduma nyingi kama kuzuia Virusi Vya Ukimwi (VVU), chanjo ya
tetanasi, huduma za afya, kupimwa magonjwa ya kuambukiza, sukari, wingi
wa damu, ukuaji wa mtoto tumboni na mapigo ya moyo.
Mchakato wote huo wa upimaji unamkuta mkunga yuko
peke yake, hawezi kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na kwa haraka ili aweze
kumhudumia mjamzito mwingine.
Anasema kunatakiwa kuwana wakunga zaidi ya watano katika vituo vya afya.
Wajawazito ni wengi
Lugha chafu
Wajawazito ni wengi
Halimu Juma ni mkazi wa Mbagala Charambe. Yeye ana
ujauzito wa miezi saba. Anasema kuwa anafika katika hospitali ya
Mbagala Zakhem saa 2:00 asubuhi anapanga foleni ya kusubiri huduma mpaka
saa 8:00 mchana.
Mkunga Mkuu katika Hospitali ya Zakhem, Mbagala,
Marina Lumambo anakiri kuwa wajawazito wanaofika kwa siku ni wengi sana
ukilinganisha na idadi ya wakunga waliopo pamoja na vifaa vya upimaji.
“Kwa siku tunapokea wajawazito 150 hadi 200
wanaohitaji huduma ya upimaji. Kwa upande wa kujifungua kwa siku
tunapokea wajawazito 30 hadi 40 na bajeti ya hospitali ni kuhudumia
wajawazito 30 tu kwa siku.
Lugha chafu
Mara kadhaa yamekuwepo madai kwamba baadhi ya
wakunga huwa na lugha chafu kwa wajawazito wanapoenda kujifungua na hata
wakati mwingine hudiriki hata kuwapiga.
Kuhusu suala la wakunga kutumia lugha chafu Mtawa
anaanza kwa kujitetea mwenyewe akisema amefanya kazi hiyo kwa miaka 24
laki hata siku moja hajawahi kutumia lugha ya matusi kwa mjamzito. Anasema kufanya kazi hiyo ya ukunga kwa ufasaha bila ya kutumia lugha ya matusi unapata baraka kwa Mungu.
Isitoshe anasema kwa sasa kuna sheria ya uuguzi na
ukunga ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kinagaubaga juu ya kutumia lugha
ya matusi kwa mkunga akiwa kazini kwa kumwambia mteja.
Mratibu wa Chama cha Wakunga Tanzania (Tama),
Martha Rimoy anakiri yamekuwapo mara kadhaa madai ya wakunga kufanya
vitendo kinyume na maadili wakati wanahudumia mjamzito.
Hata hivyo, anasema suala la namna hiyo huhitaji
uchunguzi wa kina ili kupata uthibitisho ili mhusika achukuliwe hatua.
Hata hivyo anasema kuwa yawezekana vikatokea lakini hii itatokana na
aliyejihusisha na utovu huo wa nidhamu kuwa na elimu ndogo ya ukunga.
Anasema mkunga halisi, aliyesomea taaluma hiyo,
huipenda kazi yake na wala siyo kuichafua. Hivyo humshughulikia mama
anayejifungua kwa umakini ili kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama.
Ahmed Makuwani ni daktari anayefanya kazi ya ukunga ni ya watu wenye moyo wa kuipenda kazi yao.
“Ukitaka kazi ya ukunga lazima ukubali kukesha kwa
sababu wajawazito walio wengi hujifungua usiku. Ndiyo maana wakunga
wengi ni wanawake na wanaume ni wachache kwa sababu wanaogopa kukesha
kuwazalisha wajawazito,” anasema Makuwani.
Dk Makuwani alisema kuwa, hatasahau katika maisha
yake mwaka huu, aliwafanyia upasuaji wajawazito tisa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kwa usiku mmoja na anafurahi kwa sababu wote wana
afya njema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment