WASIFU
Umri: Miaka 67
Elimu: Shahada ya Sheria (LLB) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kazi: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Historia yake
Mizengo Pinda alizaliwa Agosti 12, 1948 mkoani
Rukwa (atafikisha miaka 67 Agosti mwaka huu). Pinda ni Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2008.
Wazazi wa Mizengo Pinda wote walikuwa wakulima kwa
hiyo kijana pia alifuata nyayo hizo huku akifanya jitihada kubwa kwenye
masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shule ya msingi na sekondari,
akifaulu vizuri kila alikopita.
Baada ya masomo yake ya sekondari, Pinda alijiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea Shahada ya Sheria (LLB) mwaka
1971 hadi 1974. Baada ya kuhitimu, alijiunga katika utumishi kwenye
Wizara ya Sheria akiwa Mwanasheria wa Serikali na alikaa katika utumishi
huo tangu mwaka 1974 hadi 1978.
Mwaka 1978, alifanya kazi akiwa “Ofisa Usalama wa
Taifa” akiwa Ikulu hadi mwaka 1982, Rais wakati huo, Mwalimu Julius
Nyerere alipomteua kuwa katibu wake binafsi (Katibu wa Rais) nafasi
aliyoishikilia hadi mwaka 1985.
Baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka na kuikabidhi
nchi kwa Ali Hassan Mwinyi, Pinda alitakiwa kubaki kuendelea kumsaidia
Mzee Mwinyi na alikubali wito huo. Akaendelea kuitumikia Ikulu chini ya
utawala wa Mwinyi hadi mwaka 1992.
Mnamo mwaka 1995, Pinda alijaribu kugombea ubunge
katika Jimbo la Mpanda Mashariki lakini alishindwa katika hatua ya kura
za maoni na ikampasa kurejea kwenye kazi yake ya awali Ikulu.
Baada ya Mkapa kuteuliwa kurithi Ikulu mwaka 1995,
alimteua Pinda kuwa karani wa Baraza la Mawaziri. Wadhifa alioushikilia
kuanzia mwaka 1996 hadi 2000.
Pinda amemuoa Tunu na wamepata watoto wanne; Janet, Jenifer, Hardwick na Narusi.
Mbio za ubunge
Mwaka 2000, Pinda aliachana na utumishi ndani ya
Serikali na Ikulu akajitupa jimboni Katavi kusaka ubunge kwa mara
nyingine, safari hii alipita ndani ya kura za maoni za CCM akafanikiwa
kuwashinda wapinzani na kuwa mbunge.
Nyota ya Pinda ilizidi kung’ara mwaka 2001, pale
Rais Mkapa alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi) akifanya kazi chini ya waziri wake, Brigedia
Jenerali Hassan Ngwilizi, hadi mwaka 2005.
Mbio za urais
Nguvu yake
Mwaka 2005, Pinda aliwashinda Sebastian Bedastus wa TLP na
Albert Damian wa CUF na kuchaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa
Katavi na aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa waziri kamili wa Tamisemi.
Bahati ya Pinda kisiasa iliruka angani wakati wa
“ajali ya kisiasa” ya Edward Lowassa iliyoacha nafasi ya uwaziri mkuu
wazi kutokana na kashfa ya Richmond, Rais Kikwete alimteua Pinda kuwa
Waziri Mkuu.
Jimboni Katavi mwaka 2010, Mizengo Pinda alishinda
uchaguzi kwa “kupita bila kupingwa” na aliteuliwa tena na Rais Kikwete
kushika wadhifa wa Waziri Mkuu hadi sasa.
Mbio za urais
Pinda ni mwanasiasa aliyeamua kwa dhati kuachana
na mambo ya ubunge na kujitosa miguu miwili kwenye kinyang’anyiro cha
urais. Wanasiasa wengi hujaribu kugombea urais huku wakiwa wanautaka
ubunge, hutupa ndoano kwenye urais lakini wanapiga hesabu za ubunge
ikiwa watakosa ridhaa ya uteuzi, hawa ni aina ya watu ambao huamini kuwa
wanapaswa kusalia madarakani kwa njia yoyote ile, Pinda si mmoja wao.
Hivi ninapoandika, Pinda amekwishawaaga wana
Katavi tangu mwaka jana na amekuwa akijiweka hadharani na kuendelea na
mikakati ya chini kwa chini ya kuingia Ikulu.
Hata hivyo, kutangaza nia kwake kumekuwa na maoni
tofauti kutoka kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wanamfahamu
vizuri kwa uimara na udhaifu wake na kila mmoja ana sababu yake.
Oktoba, 2014 akiwa nchini Uingereza alieleza kuwa
amejitokeza kugombea urais ili pamoja na wenzake walioanza harakati,
Watanzania wapate muda wa kuwapima.
Mwandishi wa BBC alipomhoji kama na yeye ni
miongoni mwa watu wanaotaka kuvaa viatu vya Kikwete alisema, “… umesikia
kama nimo? … basi tukubali hilo na yeye Waziri Mkuu yumo. Hao wote
waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu aliyejitokeza ni katika jitihada za
kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au hapana?”
Nguvu yake
Pinda ana nguvu ya asili, ni kiongozi mtulivu na
msikivu. Mawaziri wakuu wengi waliopita hapa nchini si watu wa
‘chapchap’, Pinda yuko tofauti, ukimpigia simu muda wowote ambao yuko
karibu nayo atapokea na atakusikiliza nini unasema, atakushauri hatua
zipi zichukuliwe au atakuomba muda afuatilie suala husika kwa mawaziri
wake. Mara nyingi husikiliza zaidi kuliko kuongea, hii ni sifa muhimu
mno kwa kiongozi yeyote yule anayehitaji madaraka makubwa.
Jambo la pili linalompa nguvu ni kutojikweza.
Pinda si mtu wa makuu wala mbwembwe, ni mtu asiyejikweza na kila mara
anaishi maisha ya kawaida tofauti na mawaziri wakuu wengi duniani na
hata baadhi ya waliopita hapa Tanzania. Yeye mwenyewe hujiita “mtoto wa
mkulima” na aina ya maisha anayoishi yanafanana na “ukulima”.
Udhaifu wake
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Jambo la tatu ni “usafi wa kisiasa”. Ukiondoa kashfa ya Escrow
ambayo almanusura imuondoe katika wadhifa alionao hivi sasa, Pinda
hakuwahi kutuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wowote ule serikalini. Hata
Escrow kwa kiasi kikubwa tuhuma zilimwendea kwa sababu tu ya nafasi yake
ya Waziri Mkuu lakini si kwa sababu alishiriki kukwapua fedha hizo.
Pinda ana nguvu ya asili ndani ya CCM, kwa sababu
ni waziri mkuu anayemaliza muda wake, siyo jambo la ajabu kuwa ana watu
wengi wanaomuunga mkono ndani ya chama hicho.
Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa wa Pinda ni kufanya uamuzi.
Kiongozi yeyote huhitaji kuwa na uwezo mzuri wa kufanya uamuzi thabiti
na kwa wakati, Pinda si miongoni mwao. Pamoja na kujua aina ya Rais
anayefanya naye kazi, bado hakuchukua jukumu la kuwa thabiti nyakati
zote na kufanya uamuzi mgumu kila inapowezekana.
Mwanya huo umeifanya Serikali ya Awamu ya Nne
ionekane ina ombwe kubwa, ikizingatia kuwa mkuu wa nchi pia ana upungufu
ambao ungeweza kuzibwa na waziri mkuu wake ambaye naye hatendi
inavyopaswa. Uongozi mara zote ni kufanya uamuzi, siyo kutafakari mwaka
mzima. Pinda amefeli katika eneo hili.
Si hivyo tu, Pinda pia ana udhaifu mkubwa mambo
yakimzidia, anakata tamaa na kuona hakuna suluhisho. Mwaka 2013,
alipoulizwa bungeni kuhusu tabia ya vyombo vya dola kuzuia maandamano ya
wananchi na kuwapiga wanaoandamana bila sababu, aliishia kusisitiza
kuwa “watu hao lazima waendelee kupigwa”, Pinda alisisitiza kuwa
amechoshwa na maandamano na migomo na kwamba wanaofanya hivyo
kilichobakia ni “kuendelea kupigwa tu”. Kwa mtu anayejua uongozi, hii ni
kauli ya kukata tamaa kutolewa na kiongozi mkubwa wa nchi wakati ambao
alipaswa kuonyesha uongozi wake unapanua demokrasia katika masuala ya
msingi.
Hasira na pupa katika uamuzi na kukata tamaa kwake
vilionekana pia wakati alipokuwa akitoa kauli ya Serikali juu ya mauaji
ya albino. Pinda alijikuta ametamka kuwa wanaofanya hivyo nao “wauawe
tu”. Hii ni kauli ya hatari. Kiongozi ni mtu wa kusaka utatuzi wa kudumu
wa matatizo siyo kushadidia matatizo yatatuliwe kwa kuvunja sheria,
kuongeza matatizo mengine na kuchukua uhai wa watu wengine. Hizi ni
dalili za kiongozi anayekata tamaa.
Upole kupita kiasi ni udhaifu mwingine wa Waziri
Mkuu anayemaliza muda wake. Pinda ni mpole mno kiasi kwamba duru za
ndani ya Serikali zinasema kuna baadhi ya mawaziri wanatumia upole huo
kumruka na kujifanyia mambo yao bila kibali chake na hata mara nyingine
kumshauri ndivyo sivyo kwa kutumia udhaifu wake huo. Upole uliopitiliza
wa Pinda ni kati ya mambo ambayo yameiumiza Serikali ya CCM katika awamu
inayokwisha.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama Pinda atapitishwa kugombea urais kwa tiketi
ya CCM, basi uzoefu wa uongozi wa Serikali ngazi za chini hadi juu ni
jambo litakalombeba. Pinda ameitumikia Serikali hii kama mtumishi wa
ngazi ya chini na amepanda ngazi moja baada ya nyingine hadi amekuwa
waziri mkuu. Hakuna shaka kuwa amekuwa mtumishi wa Watanzania tangu
mwaka 1974 – 2015 (miaka 41).
Kukaa serikalini muda mrefu kumemfanya aijue nchi
hii na matatizo yake. Ikiwa chama chake kitakuja na ilani
inayotekelezeka na yenye majibu ya matatizo ya wananchi, mtu aliyekaa
serikalini miaka 41 si wa kumchukulia “poa”, huyu ni hazina kubwa na
huenda CCM ikaliona jambo hilo.
Sababu nyingine inayoweza kumpa Pinda nafasi ni
uadilifu. Kama nilivyosisitiza awali, Pinda hana kashfa yoyote kubwa
inayomgusa moja kwa moja na CCM inajua kuwa inahitaji watu kama yeye
iwapo itawekeza nguvu kumtafuta rais asiye na madoa lukuki. Ni mara
chache kukuta mtu amekaa serikalini miaka 40 halafu hana “rundo la
kashfa” lililomzunguka. Hii ni bahati kubwa.
Nini kinaweza kumwangusha?
Asipopitishwa (Mpango B)
Hitimisho
Sifa nyingine itakayombeba Pinda ni kutokuwa na makundi ya muda
mrefu. Kama kuna jambo lililomsaidia kuukwaa uwaziri mkuu mwaka 2008 ni
hili na huenda likamsaidia tena katika kusaka tiketi ya urais kupitia
CCM.
Tofauti na wanasiasa wengi ndani ya CCM, Pinda
hakuwahi kuwa na makundi ya kudumu na hata hii majuzi alipoonyesha kuwa
ataingia kwenye kinyang’anyiro cha urais watu wengi wanamchukulia kama
mtu mtulivu na asiye na papara, lakini anaaminika kwa kuendelea na kasi
kubwa ya mipango ya chini kwa chini kwa maandalizi. Ikiwa CCM itahitaji
mtu “neutral” wa kuivusha katika uchaguzi mgumu kama huu, basi Pinda
atakuwa moja ya karata za chama hicho.
Nini kinaweza kumwangusha?
Kama kuna jambo moja kubwa litakalokwamisha safari
ya Pinda kwenye mchujo wa CCM ni makosa mengi yaliyofanywa na Serikali
inayomaliza muda wake ambayo yeye alikuwa kiongozi wa juu kabisa.
Inawezekana CCM ikamuona Pinda kama sehemu ya
udhaifu wa Serikali ya Kikwete na ikaona si mtu wa msaada tena kwa
wakati huu hasa ikiwa kazi aliyoifanya kwa miaka saba (uwaziri mkuu)
itatafsiriwa kuwa haikuwa ya mafanikio. Jambo hili linaweza kumtupa nje.
Kitu kingine kinachoweza kumwangusha ni kasumba ya
“waziri mkuu anayemaliza muda wake hawezi kuwa Rais katika Serikali
inayofuata hapa Tanzania”. Kasumba hii imekuwapo tangu enzi za uhuru
hadi leo. Mawaziri wakuu wote tangu uhuru walipojaribu kuomba ridhaa ya
urais ndani ya CCM katika Serikali iliyofuatia waliangushwa na jambo
hili limezoeleka ndani ya CCM. Ikiwa kasumba hii itaendelea, ina maana
yale yaliyowakuta mawaziri wakuu wengine wote yatamkuta pia mtoto wa
mkulima.
Jingine linaloweza kumuondoa Pinda kwenye
kinyang’anyiro ni kuchokwa na wana mabadiliko ndani ya CCM. Ikumbukwe
kwamba kuna viongozi wengi ndani ya CCM wanahitaji mabadiliko makubwa ya
kimfumo ndani ya chama chao na ili kuyafanya, kunahitajika watu wenye
historia za kusimamia mabadiliko makubwa kitu ambacho Pinda hakiwezi.
Ndani ya CCM, Pinda anaendelea kuonekana kama kiongozi asiye na mbinu
mpya za kufanya uongozi wa kisasa na hivyo hatoweza kubeba matarajio ya
wana mabadiliko waliomo ndani ya chama hicho kikongwe.
Pinda anaweza kuwa tishio kwa wasaka urais ndani
ya CCM lakini katika jamii pana anatazamwa kama mtu wa kawaida sana
ambaye hana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa serikalini. Pinda
amekuwa serikalini akiwa waziri mkuu kwa miaka sana na hakujawa na
“maajabu” makubwa yaliyotendeka humo serikalini.
Asipopitishwa (Mpango B)
Kwa maoni yangu, ikiwa Pinda hatachaguliwa na
chama chake kugombea urais, ataungana na msururu wa mawaziri wakuu
wastaafu wengine kurudi ‘mtaani’ kulijenga taifa hili akiwa mshauri na
mtu muhimu.
Mwenyewe mara kadhaa amesikika akisema kuwa
akistaafu siasa atajikita katika “ukulima” kazi ambayo ameizoea tangu
akiwa kijana mdogo. Pinda atakuwa mmoja wa mawaziri wakuu ambaye
hataumizwa kukosa nafasi ya chama chake kugombea urais, hali hii
inasaidiwa na tabia yake ya kutokuwa na tamaa na kupapatikia mambo
makubwa ambayo hayawezekani.
Hitimisho
Serikali ya awamu ya nne inamaliza muda wake huku ikiwa na
upungufu mwingi na yeye amekuwa sehemu ya historia hiyo. Nadhani CCM
itapaswa kupiga hesabu za kutosha kabla ya kumfikiria Pinda, itaipasa
ipige hesabu za aina ya mgombea ambaye atasimamishwa na vyama vya Ukawa
na kupima kuona kama Pinda anauzika kiasi cha kumshinda mgombea bora wa
upinzani ikiwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki au la.
Namuona Pinda kama mshauri mzuri wa CCM siku za
mbele lakini si kama mgombea urais bora sana, japokuwa kama nilivyosema
awali, nguvu yake na mtandao wake ndani ya CCM vinawatisha wagombea
wengine na huenda vikambeba. Mzee huyu “mtoto wa mkulima” tunamtakia
kila la heri katika kuvuka vizingiti vinavyomkabili.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment