
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba,
ameishangaa serikali kumsafisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,
Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliyesimamishwa
kazi, Eliakim Maswi, dhidi ya tuhuma za kuhusika katika kashfa ya
kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti
ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku watuhumiwa
wengine wakiachwa kusafishwa.Alisema hayo alipokuwa akichangia hotuba ya mwelekeo wa kazi za
serikali, makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Bunge kwa mwaka 2015/16 iliyowasilishwa na Mizengo Pinda, bungeni juzi. Serukamba alisema inashangaza kusikia kamati iliyochunguza tuhuma
dhidi ya Maswi na Prof. Muhongo kwamba, imebaini kuwa ni wasafi na
muamala uliofanywa katika akaunti hiyo ulikuwa safi.
Alisema hakubaliani jinsi suala hilo lilivyoshughulikiwa na kutoa
taarifa kuwa licha ya suala la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
kusimamiwa na wizara hiyo, viongozi wake wanasafishwa kuwa hawana hatia.
Alihoji inakuwaje watu wengine wafikishwe mahakamani, waondolewe kwenye
nyadhifa na wengine wakiwa bado maofisini. “…hao ni wachafu? Maswi na Muhongo ndiyo wasafi?” alihoji Serukamba.
Aliongeza: “Kama wao ni wasafi na muamala wa Escrow ulikuwa safi,
kwanini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna
Tibaijuka, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, nao wasisafishwe?
au ni wachafu?”
Alimtaka Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kutangaza kuwa
wengine waliotuhumiwa kuwa ni wachafu kama Prof. Tibaijuka, Chenge,
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kuwa nao
pia hawana hatia. “Nashangaa wengine wamesafishwa. Mbona William Ngeleja na Victor
Mwambalaswa, waliondolewa kwenye nafasi za uenyeviti? Nao wasafishwe,”
alisema Serukamba.
Ngeleja alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala wakati Mwambalaswa alikuwa anaongoza Kamati ya Nishati na
Madini. Ngeleja alitajwa kupokea Sh. milioni 40 kutoka kwa mmiliki wa
kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, wakati
Mwambalaswa alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Tanesco iliyotajwa kuhusika katika
kashfa ya akaunti hiyo.
Serukamba alitaka Bunge liambiwe kama kuna wasafi, wachafu ni wepi na Katibu Mkuu Kiongozi aeleze usafi wao ni nini?
WALIOTIMULIWA WAREJEE
Alisema iwapo ni wasafi na muamala ni safi, basi waliojiuzulu warejeshwe kwenye nafasi zao. Alitoa mfano wa Kenya kuwa katika kashfa ya Goldenburg, ilidaiwa
kuwa Waziri wa Fedha, Amos Kimunya, alihusika kuuza hoteli ya Grand
Regency, naye alijiuzulu, lakini baada ya uchunguzi wa tume ya mahakama,
alibainika kuwa hana hatia.
Alisema hatua iliyofuata alirudishiwa wadhifa wake akateuliwa kuwa
waziri wa viwanda. Alitaka hatua hizo zichukuliwe kwa waliotuhumiwa kuwa
wana hatia ambao sasa wameonekana kuwa wasafi. Alishauri tume ya
uchunguzi ya mahakama iundwe kuwachunguza mawaziri waliojiuzulu kutokana
na kashfa mbalimbali kama ile ya Richmond.
Aliwataja waliokuwa mawaziri waliojiuzulu kuwa ni Ezekiel Maige
(Maliasili na Utalii), Ngeleja na aliyekuwa Naibu Waziri Nishati na
Madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa,
wachunguzwe na wasafishwe.
TOKOMEZA
Akizungumzia pia taarifa kuwa watuhumiwa waliosimamia Operesheni
Tokomeza ni safi, alisema ina mengi ya kushangaza. Alisema japo wabunge
wanataka kuona ripoti ya Operesheni Tokomeza, Ikulu haiwapi, badala yake
wanawasilisha taarifa nusu nusu tena ile wanayotaka ifahamike.
Alitahadharisha kuwa kudai watuhumiwa hao kuwa ni wasafi na wengine ni
wachafu, hilo halikubaliki na kwamba, ni ubaguzi. “Huu ni ubaguzi. Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema huu ni ubaguzi,” alisema.
BUNGE LIDAI
Alitaka serikali iache undumilakuwili na kusisitiza Bunge lidai
serikali iwasafishe wengine wote waliotuhumiwa katika kashfa ya akaunti
hiyo na ile ya Operesheni Tokomeza kwa kigezo kuwa muamala ni safi na
waliohusika ni wasafi.
MWAMBALASWA AJIBU
Akizungumzia sakata la kutajwa na Serukamba kuwa naye asafishwe,
Mwambalaswa alisema hapingani na azimio wala maamuzi ya Bunge
yaliyomuondoa kwenye wadhifa wa Uenyekiti wa Kamati ya Bunge. Alisema hahitaji kutetewa, kujitetea wala kusafishwa kwa vile hana tope na aliwajibika kisiasa.
Alitoa utetezi wake wakati akichangia hoja kwenye hotuba hiyo wala
hakusimama kuomba kiti kutoa taarifa. Alisema aliwajibika kwa vile
alikuwa mjumbe wa bodi hiyo, lakini akaeleza kuwa siku kilipofanyika
kikao kilichokuwa na ajenda kuhusu akaunti ya muamla wa Tegeta Escrow
hakuhudhuria. Serukamba anakuwa mbunge wa pili kuzungumzia Tokomeza na
Escrow akitanguliwa na Lissu, ambaye pia juzi alikosoa kuwasafisha
watuhumiwa waliohusika na kashfa hizo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment