
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeonya kuwa,
uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu ukiahirishwa nchi
itawaka moto.Kambi hiyo imeituhumu serikali kuchelewesha kukamilisha usajili wa
watu kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura licha ya tarehe ya kupiga
kura kufahamika. Kiongozi wa Kambi hiyo, Freeman Mbowe, alisema bungeni jana kuwa,
kitendo hicho kina malengo na nia mbaya ya kutaka kuongezea muda wa
utawala wa Rais Jakaya Kikwete, kwa kisingizio kuwa uchaguzi mkuu
hauwezi kufanyika kwani daftari hilo bado halijakamilika kuboreshwa.
Alisema ucheleweshaji huo umefanywa na serikali kwa kuchelewesha fedha za kuanza mchakato. “Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imeanzisha mchakato wa kuandikisha
wapiga kura bila kutengewa fedha za kutosha za kununulia vifaa, kuajiri
na kuwapa mafunzo wafanyakazi wanaohusika na kutoa elimu kwa umma,”
alisema.
Alisema hivi sasa inaonekana serikali ina matatizo makubwa ya fedha
baada ya wahisani kusitisha kutoa fedha za msaada wa bajeti kwa sababu
ya ufisadi wa kutisha wa Akaunti ya Tegeta Escrow. Alisema pamoja na ukweli kwamba Sheria ya Taifa ya Uchaguzi
inahitaji tume kuboresha daftari hilo mara mbili kati ya uchaguzi mkuu
na unaofuata; kwa makusudi serikali iliamua kuivunja Sheria ya Kuboresha
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Alisema kambi hiyo inataka kupata majibu kutoka serikali hii ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhusu lini mashine za BVR zitawasili nchini
kwa ukamilifu wake. Pia alisema inataka kujua lini Nec itamaliza kuwaandikisha
Watanzania wote wenye sifa ya kuwa wapiga kura katika Daftari la Wapiga
Kura.
“Ni lini Watanzania ambao watakuwa wameandishiwa kwenye daftari
hilo watapata fursa ya kuhakiki Daftari la Wapiga Kura kwa mujibu wa
sheria na zoezi hili litachukua muda gani. “Je, ni lini itafanya maandalizi mengine ya kina ya uchaguzi mkuu
na ikizingatiwa kuwa muda wote itakuwa inaendelea kuandikisha wapiga
kura,” alihoji.
Alihoji ni lini tume itaweka hadharani mpango mzima na ratiba za
utekelezaji kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015 ambao kwa mujibu wa
sheria zimebaki siku pungufu ya 100 kwa kampeni za uchaguzi kwanza.
AFICHUA MPANGO HARAMU
Alisema kukosekana kwa muda na vifaa vya kutosha kwa ajili ya
kuandikisha wapiga kura wote wenye sifa kwa mfumo wa BVR, tume
imeshaamua kwa makusudi kutokuwaandikisha wapiga kura zaidi ya milioni
2.9 katika uandikishaji unaoendelea. Alisema hiyo ni kwa mujibu wa taarifa rasmi za tume iliyoko kwenye randama yake.
SERIKALI YAJIANDAA KUPAMBANA
Mbowe alisema wakati serikali ikishindwa kuipatia fedha Tume ya
Uchaguzi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2015,
ili ufanyike katika mazingira ya amani, haki na utulivu, serikali
imeamua kuwekeza na kujiandaa kupambana na wananchi wake.
“Hii inatokana na ukweli kuwa wakati tume inakosa fedha za kulipia
vifaa kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura na kufanya maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu, tuna taarifa kuwa Serikali imeamua kuagiza zaidi ya
magari 777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi,” alisema.
Alisema magari hayo ni kuanzia yale ya maji ya kuwasha, doria na shughuli za ukaguzi katika mwaka huu wa fedha. “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inajiuliza kwamba hivi ni nini
kipaumbele chetu kama taifa kwa sasa? Je, ni kuandaa mazingira ya
kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwa hali ya haki, amani na utulivu?...au ni
kujiandaa kuuvuruga uchaguzi huo?. Ndiyo maana tunashuhudia jitihada
hizi za kujiandaa kupambana na wananchi wakati uchaguzi mkuu
utakaposhindikana kufanyika kwa sababu ya kukosekana kwa maandalizi
thabiti na ya kina ya kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi huo,” alisema.
Alisema hizo ndiyo sababu za serikali kukataa kufanya maandalizi ya
kina kwa ajili ya uchaguzi mkuu na kuwekeza katika mapambano.
LISSU ANGA’AKA
Mbunge Iramba Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alitikisa Bunge na
kuoinya serikali kuwa kama ina mpango wa kuahirisha uchaguzi
haitawezekana kwa vile ni vita pekee inayokubalika kikatiba kuahirisha
uchaguzi.
Akizungumza kwa kauli kali wakati akichangia hotuba ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, aliishambulisha serikali kwa akiita ya kichovu na dhaifu,
alisema ibara ya 44 (4) ya Katiba ya Tanzania inasema hakuna namna ya
kuahirisha uchaguzi ila tu kama taifa liko vitani.
Alisema serikali chovu imeshindwa kukamilisha kura ya maoni,
kadhalika hadi sasa imebakia miezi mitano imeshindwa kusajili wapiga
kura. “Taarifa ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 2010 inasema kuwa katika
uchaguzi wa 2010 uandikishaji wa wapiga kura ulikuwa umekamilika
Septemba 2009 leo ni mikoa miwili pekee? Serikali ieleze sababu,”
alifoka.
“Tunahitaji serikali mpya, utaratibu mpya siyo hawa walioshindwa kuandaa kura ya maoni, kusajili wapiga kura.” Aliiponda serikali akidai imepitisha katiba pendekezwa kwa kutumia
kura za marehemu, wagonjwa waliolazwa India na mahujaji na kuhoji kuwa
safari hii hakuna ujanja wa kuahirisha uchaguzi wala kuchakachua.
MHAGAMA ATIBUKA
Baada ya kuiponda serikali kuwa ni chovu na kudai kuwa kura za
marehemu zilitumika kuidhinisha kura pendekezwa walipigiwa, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Jenister Mhagama,
alimtaka kuacha lugha ya kuudhi na kupotosha kuwa marehemu walipigishwa
kura.
Hata hivyo, Lissu alimpinga na kumuonya asijibu hotuba yake, wala kutoa maelezo ya michango yake.
“Anaomba nini? Anataka utaratibu au anajibu hotuba yangu, akae
chini” Lissu alisema kabla ya Spika Anne Makinda kumruhusu Mhagama
kuendelea kutoa maelezo.
Pinda alipopewa tena nafasi aliendelea kuiita serikali chovu ambayo
licha ya watu kuuliwa, mifugo kuuawa na mali kuharibiwa kwenye
Operesheni Tokomeza, imewasafisha mawaziri na watendaji kuwa hawana
lawama.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment