
Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania
katika nchi za nje wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano wa siku tatu
ulioanza, Dar es Salaam juzi.
Rais Jakaya
Kikwete amewaaga rasmi mabalozi 36 wa Tanzania katika mataifa mbalimbali
akiwaeleza kuwa hatakuwa madarakani baada ya Oktoba.
Rais aliwaaga mabalozi hao jana wakati akifungua
mkutano wa siku tatu utakaohitimishwa leo, ambao pamoja na mambo
mengine, utajadili ‘Diplomasia ya Tanzania Kuelekea Dira ya Taifa 2025.’ “Huu ni mkutano wangu wa mwisho kuzungumza nanyi.
Mmenisaidia vizuri katika kipindi chote cha utawala wangu na niwaahidi
tu kuwa nitaondoka Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema Rais
Kikwete.
Pamoja na kuaga, aliwaachia mambo manne ya
kuzingatia ili kuifanya Tanzania iendelee kuheshimika kimataifa. Mambo
hayo yanajumuisha; kuwasaidia wawekezaji wa Kitanzania kupata fursa
katika nchi wanazoziwakilisha; kuwasaidia Watanzania walioko katika nchi
wanakowakilisha kuunda umoja wao; kuzishawishi asasi za kiraia za
kimataifa kuja kuwekeza nchini pamoja na kutengeneza marafiki wa Taifa
kwa ujumla.
Rais alieleza kuwa wakati Serikali ikitekeleza
mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025,
tayari kuna wananchi wenye uwezo wa kiuchumi ambao wameshaanza kuwekeza
katika baadhi ya nchi Afrika na hata nchi za Magharibi, hivyo ni vyema
wakapewa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma zao.
“Niwakumbushe tu kuwa mahitaji yamebadilika nanyi
pia badilikeni. Kwa sasa ni vyema vipaumbele vyenu vikawa uwezo wa
kuleta mitaji nchini, kiasi cha misaada ya maendeleo mlichochangia,
masoko kwa bidhaa zetu mliyoyabainisha na wawekezaji wa nje
mliowashawishi kuja kuwekeza,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Achaneni na ripoti zenu za kila mwisho wa mwezi
mnazoleta za malalamiko mara eeeh wanataka mabadiliko kwenye cyber crime
(Sheria ya Makosa ya Mtandaoni) au Sheria ya Takwimu. Hayo masharti
wanayotoa ndiyo maana ilifikia hatua nikasema kuwa kama hatuwezi kupata
mikopo bila masharti ni bora tusipewe tu.”
Rais pia aliwataka mabalozi hao kuzihoji serikali
za nchi waliko juu ya mchango wao katika kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi ambayo athari zake zinaziathiri sana nchi zinazoendelea kama
Tanzania.
Alifafanua kuwa kama jotoridi la dunia litaendelea
kuongezeka upo uwezekano mkubwa ifikapo mwaka 2030 Mlima Kilimanjaro
usiwe na theluji iliyopo sasa, hali itakayopunguza mvuto wake na hivyo
kuathiri utalii. Alisema: “Ukame umeongezeka… mwaka jana hatukupata
mvua kabisa za vuli. Mazao yamekauka na ipo dalili kuwa kutakuwa na
upungufu mkubwa wa chakula mwaka huu.”
Aliongeza kuwa aliingia madarakani nchi ikiwa
haina adui na anaondoka nchi ikiwa hivyo pia na kuwakumbusha kuwa ni
vyema kila mmoja akajitahidi katika hilo.
Akimkaribisha Rais kufungua mkutano huo, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kwa
kipindi cha miaka 10 iliyopita nchi imeshirikiana vyema na mataifa mengi
ulimwenguni jambo lililowezesha kufunguliwa kwa Ubalozi wa The Hague
pamoja na kufutiwa madeni na ongezeko la misaada ya maendeleo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mussa Azzan Zungu alimweleza Rais kuwa kamati yake imekuwa ikishirikiana vyema na wizara kuifanya Tanzania iendelee kuwa na uhusiano mwema wa kidiplomasia.
CHANZO: MWANANCHI
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mussa Azzan Zungu alimweleza Rais kuwa kamati yake imekuwa ikishirikiana vyema na wizara kuifanya Tanzania iendelee kuwa na uhusiano mwema wa kidiplomasia.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment