Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alipokuwa akiwasili kwenye viwanja vya
Bunge mjini Dodoma mwaka jana kuwasilisha bajeti ya mwaka 2014/2015.
Bunge la Bajeti ya Serikali ya
2015/16 linaanza leo mjini Dodoma kwa mwendo wa mchakamchaka kutokana na
kuongezwa saa mbili kila siku ili limalizike Juni 27. Saa za mjadala katika vikao zimeongezwa ili kuziba
pengo la siku 12 zinazopungua na kutoa fursa kwa wabunge kuchangia
bajeti za wizara na Bajeti Kuu ya Serikali ndani ya siku 44
ikilinganishwa na siku 56 zilizotumika kupitisha bajeti ya mwaka 2014/15
na miaka ya nyuma.
Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wa bajeti,
wachumi na wanasiasa wamesema hawatarajii kuona jipya isipokuwa mipasho
inayolenga Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Serikali imepanga kukusanya na kutumia Sh22.4
trilioni katika mwaka wa fedha 2015/16 ikiwa ni nyongeza ya Sh2.6
trilioni ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2014/15 ambayo ilikuwa Sh19.8
trilioni.
Kwa miaka iliyopita, baadhi ya wizara zenye
majukumu mengi zilikuwa zinatengewa siku mbili au tatu, lakini safari
hii hali itakuwa tofauti kwa kuwa zitajadiliwa kwa siku moja tu au mbili
kulingana na mjadala utakavyokuwa na mapumziko yatakuwa Jumapili pekee. Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano
wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka alisema badala ya Bunge kuanza
saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana na baadaye saa 11 jioni hadi saa
1.45 usiku; sasa litaanza 3.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na kuendelea
saa 10.00 jioni hadi saa 2.00 usiku.
“Ili kuendana na muda, tumeongeza saa kadhaa ili
kumaliza shughuli zote zilizopangwa. Siku za Jumamosi zitahesabika kama
siku za kazi kama kawaida.” alisema. Alisema Bunge hilo litamalizika Juni 27 lakini
akaongeza: “Tumeacha siku tatu za dharura, kuanzia Juni 28 hadi 30 ili
kama kuna jambo lolote la muhimu litajitokeza Bunge linaweza kuendelea
kwa muda huo wa siku tatu.”
Alisema kutokana na mabadiliko ya uwasilishaji, ni
lazima bajeti iwe imesomwa kabla ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya
mwaka unaofuata Julai Mosi.
“Inawezekana tukapata kiongozi wa kulihutubia
Bunge au katika upitishaji wa bajeti za wizara akidi isitimie na
kulazimika shughuli husika kuendelea siku inayofuata. Zamani Bunge la
Bajeti lilikuwa likianza Juni hadi Agosti, lakini kwa mabadiliko haya
sasa lazima limalizike Juni,” alisema.
Alisema bajeti zote za wizara hadi kufikia Juni 10
zitakuwa zimeshasomwa, Juni 11 itasomwa Bajeti Kuu ya Serikali na
kuanza kujadiliwa.
Alisema ratiba hiyo pia inaweza kuvurugika utakapoanza mfungo wa Ramadhani.
Maoni ya wasomi
Wabunge wanena
Alisema kuchelewa kuanza kwa Bunge kumetokana na kuahirishwa kwa tarehe ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
“Kama mtakumbuka Katiba Inayopendekezwa ilikuwa
ipigiwe kura Aprili 30, sasa baada ya kutangazwa kuwa imeahirishwa,
tuliamua kupanga upya ratiba,” alisema.
Alisema Bunge hilo litavunjwa kwa tangazo la
Serikali linalotolewa na Rais na si Mkuu huyo wa Nchi kulihutubia Bunge
na kulivunja: “Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atalihutubia Bunge Juni 27.”
Maoni ya wasomi
Profesa Prosper Ngowi kutoka Idara ya Uchumi, Chuo
Kikuu cha Mzumbe alisema mbali na Bunge hilo kutekwa na mijadala ya
kuelekea uchaguzi ujao, mambo mengine yanayotarajiwa ni wabunge wengi
kuonyesha mbwembwe za kuhoji mambo yanayohusu masilahi ya wananchi
katika majimbo yao.
Alisema wabunge watakuwa na hoja za kuibana
Serikali juu ya miradi mingi iliyokwama katika bajeti zilizopita
kutokana na kiwango kidogo cha fedha kilichowasilishwa.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Profesa Humphrey Moshi
kutoka Idara ya uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akisema
wabunge watahoji utekelezaji wa bajeti iliyopita kwa kuangalia uhalisia
wake na mipango ya bajeti itakayojadiliwa kwa Bunge.
“Kila mbunge anatamani kuona mradi wa maendeleo
ukikamilika katika jimbo lake, lakini ukiangalia fedha ambazo zimekuwa
zikitengwa ni kidogo na za utegemezi, kwa hivyo ningeshauri kwa sasa
wangejadili na kushughulikia viporo vya miradi, badala ya kuanzisha
vingine wakati kuna madeni ya makandarasi,” alisema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Maofisa Watendaji Wakuu wa
Kampuni Binafsi Tanzania (CEOs), Ali Mufuruki alisema hatarajii kuona
jambo lolote jipya zaidi ya mijadala ya kuelekea Uchaguzi Mkuu. “Ninachotegemea kwa sasa ni kuona sehemu kubwa ya mapato yakitumika kwa shughuli za kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema.
Wabunge wanena
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David
Kafulila alisema bajeti hiyo haina matumaini kwani miradi ya maendeleo
katika bajeti inayomalizika Juni 30 haikutekelezeka kwa asilimia 80.
“Kukwama kwa msaada wa kibajeti zaidi ya Dola 500 milioni kutoka
kwa wahisani, kukwama kwa mkopo wa kibiashara ambao siyo kawaida kabisa
ambapo Serikali ilitarajia kukopa Dola 800 milioni na kuambulia 300
milioni ni ushahidi tosha wa namna Serikali inavyopumulia mashine,”
alisema.
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla
alisema muda wa kuijadili bajeti ni mfupi hali ambayo hujitokeza kila
mwaka wa uchaguzi lakini haiwezi kuwanyima wananchi fursa ya kuijua
bajeti ya nchi yao.
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi
alisema bajeti hiyo haina jipya, huku akitolea mfano mpango wa Serikali
wa kuboresha reli kwa mwaka mmoja wakati ilishindwa kufanya hivyo kwa
miaka 50.
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa alisema
tatizo la bajeti hii ni kupunguzwa kwa asilimia 50 fedha za maendeleo...
“Unapopunguza fedha za maendeleo wakati tunaambiwa bwawa la umeme la
Mtera maji yamepungua hapo si tutegemee kurudi kule kwa Aggreko na
Symbion kuuziwa umeme wa ghali.”
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
alisema fedha za maendeleo ambazo zimepungua zitapatikana kabla ya Juni
30, mwaka huu... “Niwathibitishie wananchi kuwa fedha hizi zitapatikana
bila matatizo yoyote.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment