
Jana gazeti hili lilikuwa na habari iliyosema
‘JK akerwa polisi kubughudhi wananchi’. Habari hiyo ilikuwa ikielezea
namna Rais Jakaya Kikwete alivyokerwa waziwazi na kitendo cha polisi
kuwazonga na kuwasukuma wananchi waliokusanyika eneo la Jangwani, Dar es
Salaam kumsikiliza.
Kukerwa kwa Rais Kikwete kuliongezeka pale
alipoona juhudi zake za kuwataka polisi kuacha kuwabugudhi wananchi
kushindikana, hadi alipofikia kutamka “Jamani waacheni waje kwa nini
mnawapiga? Mbona hamsikii? Kova hebu waambie askari wako wawaache
kuwasumbua.” Kwanza tuwashangae polisi kwa kitendo chao cha kuwapiga
wananchi, kwa kuwa Rais Kikwete ndiye aliamua kuwafuata kwenye maeneo
yao baada ya kusikia wameathirika na mvua.
Tunawashangaa polisi kwa sababu Rais ni mwanasiasa
na mtaji wa wanasiasa ni wananchi, kitendo chao cha kuthubutu kunyanyua
rungu kuwapiga wananchi mbele ya kiongozi wao waliyemchagua
kidemokrasia na hadi kufikia hatua mwenyewe kukasirika, kunaonyesha
jinsi polisi walivyopitiliza kwa uonevu.
Kwa muda mrefu ripoti nyingi za haki za binadamu
zimekuwa zikilalamikia Jeshi la Polisi kwa uonevu, rushwa, mauaji ya
raia na unyanyasaji. Mfano, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
katika taarifa yake kuhusu tukio la Januari 27 la polisi kuwapiga
wafuasi wa CUF, huko Mbagala Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam,
ilisema ni kitendo kilichoashiria uvunjifu wa haki za binadamu.
Mfano mwingine ni ripoti ya Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari Daudi
Mwangosi. LHRC ilisema tukio hilo ni uvunjwaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Uonevu dhidi ya raia na wanasiasa unaofanywa na
polisi ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977,
Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la 1948, Mkataba wa Kimataifa
kuhusu haki za kiraia na kisiasa wa 1966 na Mkataba wa Mataifa ya Afrika
kuhusu Haki za Binadamu na Watu wa 1981.
Tunamshukuru Rais Kikwete kwa kutofumbia macho
uonevu huo, tena uliokuwa ukifanywa bila soni na mbele ya macho yake.
Pia, turudishe kumbukumbu nyuma kwa Rais kwamba uonevu huu umekuwa
ukifanyika kwa muda mrefu bila hatua stahiki kuchukuliwa kwa wahusika.
Kuna baadhi ya makamanda wa polisi ambao wamehusishwa na uonevu huo
lakini badala ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu wameishia kupandishwa
vyeo, kuhamishwa maeneo ya kazi na hata kupongezwa kwa kazi nzuri.
Sisi tunasema kwa kuwa Rais ameshuhudia kwa macho
yake, ni wakati sasa wa kuchukulia hatua stahiki, tunaamini bado
hajachelewa kukomesha vitendo hivi kwa kuwa nchi inakwenda kwenye
Uchaguzi Mkuu, polisi watatumika kuonea watu. Hivyo, tunaamini kama
hatua zitachukuliwa sasa inaweza kuwa kinga na kuufanya uchaguzi kuwa wa
amani na utulivu.
Tunasema hivyo kwa sababu siku za karibuni
tumeshuhudia malumbano kati ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta
Jenerali Ernest Mangu na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu wimbi la
uanzishaji wa vikundi vya ukakamvu vya vijana vyenye mwelekeo wa
kijeshi. Tunaamini iwapo Rais Kikwete atachukua hatua stahiki huenda
akarejesha imani ya wananchi kwa polisi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment