Social Icons

Pages

Friday, April 17, 2015

WELEDI NA UMAHIRI VIPEWE NAFASI MRADI WA MABASI DAR

Mradi wa mabasi yaendayo kasi
Wakati Watanzania hasa wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakisubiri kwa hamu kuanza kwa mradi wa mabasi yaendayo kasi, kizungumkuti kimewakumba wadau wa mradi huo kuhusu nani apewe zabuni ya kuusimamia.
Kukiwa kumebakia karibu mwezi mmoja na nusu kabla ya kuanza kwake mwezi Juni, wadau wanahoji nani anapaswa kuuendesha mradi huo wa kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki kati ya wawekezaji wa kigeni au wazawa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, gharama tu za mabasi yatakayotumika katika mradi huo, achilia mbali zile za ujenzi wa miundombinu yake, zinagharimu zaidi ya Sh180 bilioni.
Watanzania tutaonekana kituko kama tutaacha fedha hizi na nyinginezo zipotee bure bileshi, kama Serikali yetu itatoa zabuni kwa mwekezaji asiye na sifa.
Hatuoni mantiki ya kizungumkuti kilichopo au mjadala unaoendelea kuhusu nani aendeshe mradi kati ya wazawa na wageni. Tunachoamini sisi ni kuwa ili mradi huu ulete matunda yaliyokusudiwa kwa wananchi na Serikali, hauna budi kusimamiwa vilivyo na mwekezaji mwenye weledi na umahiri mkubwa wa masuala ya usafiri hasa wa kisasa.
Sisi hatuamini katika aina, asili au mahala anakotoka mwekezaji, bali tunaamini katika sifa stahiki za uendeshaji wa mabasi haya ambayo tunasikitika kusema kuwa baadhi ya watu wanafikiri uendeshaji wake unaweza kuwa mithili ya ule wa mabasi ya daladala. Kuukubali tu mradi wenyewe unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, kunatoa picha ya namna Serikali yetu ilivyo na dhamira ya dhati ya kupambana na changamoto za usafiri katika jiji la Dar es Salaam.
Mradi huu unaelezwa kuwa pamoja na mambo mengine utasaidia kupunguza foleni za magari barabarani ambazo takwimu zinaonyesha zinachangia kupotea kwa takribani Sh 4 bilioni kila siku. Hiki si kima kidogo katika uchumi unaoyumbayumba wa nchi yetu. Hii ni dhamira njema, hivyo Serikali isikubali kuja kutoka mikono mitupu kwa kuukabidhi mradi kwa mwekezaji dhaifu.
Tunaamini Serikali ina mfumo mzuri wa kutoa zabuni katika miradi yake, tuache mchakato huo uchukue hatamu ili hatimaye apatikane mwekezaji makini na mwenye uwezo wa kusimamia mradi huo mkubwa.
Kama tunataka kuona athari chanya ya mradi huu katika uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi, katu tusiruhusu ubabaishaji au upendeleo kwa hoja ya uzawa au ugeni. Sote tunahitaji kuona mafanikio ya mradi huu pasipo kujali mwekezaji anatoka ndani ya nchi au nje.
Jambo zuri ni kuwa nchi hii tuna uzoefu mzuri wa kufeli kwa mashirika mbalimbali ya umma yaliyojishughulisha na sekta ya usafiri hasa wa abiria. Pamoja na sababu nyingizo mashirika haya yalianguka kwa sababu ya kuendeshwa kiubabaishaji.
Hakukuwapo na utashi wa wahusika kuviendesha vyombo hivyo kwa weledi, utaalamu na umahiri, hatimaye vikafa na sasa vimebaki historia. Hata pale baadhi vilipobinafishwa, tunadiriki kusema kuwa bado vimeendeelea na usimamizi uleule wa ‘bora liende’. Matokeo yake vyombo hivyo vinasuasua, huku vikiwa havina mchango wowote wa maana kwa nchi na wananchi walio wengi.
Huu si mradi wa kitoto na kama kweli tunaamini kuwa ni uwekezaji muhimu na mkubwa kwa Taifa, Serikali haina budi kumpa zabuni mwekezaji mwenye uwezo na sifa zinazorandana na umuhimu na ukubwa wa mradi wenyewe.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: