Social Icons

Pages

Wednesday, April 08, 2015

VIONGOZI WAELEZA UMAHIRI WA MZEE KARUME

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein amewaongoza wananchi mbalimbali katika dua ya kisomo cha hitma cha kumuombea rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Aman Karume aliyefariki Aprili 7, mwaka 1972.
Kisomo hicho cha dua kiliongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, kilihudhuriwa na watu mbalimbali wa ndani na nje ya Zanzibar wakiwamo viongozi wa serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilifanyika katika ofisi kuu za CCM Kisiwandui mjini hapa.
Baada ya kisomo hicho, Sheikh Mussa aliwapongeza viongozi wa Zanzibar kwa kufanikisha kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo imejenga maelewano miongoni mwa viongozi na wananchi. Alisema kuwa Zanzibar ya sasa siyo Zanzibar ya miaka iliyopita ambapo amani ilipotea na kutokuwepo kwa maelewano miongoni mwao kutokana na mambo ya kisiasa.
“Hilo ndilo jambo la kujivunia kuwa na amani katika nchi na viongozi wanadhamana kubwa ya kuilinda amani isitoweke kwani hata siku ya ufufuo mbele ya Mwenyezi Mungu utaulizwa jinsi mambo mema uliyoyafanya ikiwamo amani huko huendi kuulizwa chama kama wewe ulikuwa CUF, CCM au Chadema,” alisema Mussa.
Aidha, alimpongeza rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Karume kutokana na mchango wake mkubwa wa kuwaunganisha Wazanzibari kuwa kitu kimoja bila ya kujali dini, rangi au kabila.
Baadhi ya watu waliozungumza na NIPASHE jana walisema Mzee Karume ni kiongozi wa kupigiwa mfano kutokana na mchango wake mkubwa wa kimaendeleo. Askofu wa kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh, alisema Karume ameacha mambo mengi mazuri katika kuwaletea maendeleo Wazanzibar bila ya kujali dini.
Alisema misingi hiyo ya Karume katika kudumisha umoja miongoni mwa waislamu na wakiristo inapaswa kuendelezwa kwani misingi mema ya kiongozi huyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: