Katibu Mkuu wa Chama cha
Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametaja utitiri wa kodi za Tanzania
kama kikwazo cha wafanyabiashara kutofanikiwa.
Kinana alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa
hadhara katika Viwanja vya Pasua mjini Moshi uliohudhuriwa na umati
mkubwa wa watu. Katibu huyo alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na kodi nyingi ambazo hazina manufaa. Alisema wafanyabiashara wanaumizwa zaidi na kodi hizo lakini hawana mtu wa kuwasemea zaidi ya kuendelea kunyonywa.
Hata hivyo, aliwatupia lawama wabunge wa CCM kuwa
wingi wao bungeni hausaidii kitu kwa sababu wameshindwa kuondoa sheria
zinazomkandamiza mwananchi. “Kila kona ni kodi na kila kukicha ni kodi,
Sumatra anadai kodi, Fire wanadai kodi, taasisi zingine zinadai kodi,
yaani ni kero tupu,” alisema Kinana.
Katibu huyo alisema idara pekee inayotakiwa kudai
kodi ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwani ndiyo waliobebeshwa
dhamana ya kutafuta fedha.
Akizungumza na wafanyabiashara wakati wa chakula cha usiku, kiongozi huyo aliwataka kupaza sauti zao pale wanapohisi kuonewa.
Alitolea mfano wa Uganda kwamba wafanyabiashara
waliigomea Mamlaka ya Mapato ya nchi hiyo hadi wakapelekana kwa Rais
Yoweri Museveni. “Sihamasishi wafanyabiashara mgome, lakini nasema
hivi, hata Museveni aliwaambia URA kwamba ninaweza kubadiri idara za
kodi lakini hawa wataendelea kulipa kodi, hivyo wafanyabiashara ni bora
zaidi kuliko idara za kodi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kinana alimwagiza Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro kulifungua soko la Kati ili wananchi waendelee na
biashara zao. Soko hilo lilifungwa tangu Machi, mwaka jana kwa madai ya kufanyiwa ukarabati mkubwa ingawa haujafanyika hadi sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alikubali kukutana na
wafanyabiashara Aprili 9, mwaka huu, ili kupanga mkakati wa kuanza
kufanyika kwa biashara sokoni hapo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment