
Wabunge wa Kambi ya Upinzani wa kundi la Ukawa wakijadiliana jambo
bungeni jana baada ya kutaka bunge lisiendelee na kikao mpaka wapate
majibu kutoka Serikalini kuhusu zoezi la uandikishaji wa daftari la
kudumu la wapigakura (BVR).
Wabunge wa upinzani
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walianzisha tafrani
bungeni na kusababisha kikao cha Bunge kuvunjika saa 5.18 asubuhi baada
ya kusimama na kupaza sauti wakishinikiza Serikali itoe kauli juu ya
hatima ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na upigaji wa
Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Huku wakiwa wamesimama walikuwa wanapiga kelele
wakisema, ‘hatutaki kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’, Watanzania
wapo njia panda’ na ‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe kuilinda
Serikali’, ‘Waziri Mkuu yupo bungeni kwa nini asitoe kauli’ na maneno
mengine mengi bila mpangilio.
Wabunge hao wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na
CUF, kwa umoja wao walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa majibu
hayo muda huohuo, kabla ya jioni kutoa hutuba na kuahirisha mkutano huo
wa 19 wa Bunge.
Baadaye jana usiku katika hotuba yake ya
kuahirisha Bunge hadi Mei 12, utakapoanza Mkutano wa 20, Waziri Mkuu
Pinda alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatoa taarifa siku za
hivi karibuni kuhusu upigaji wa kura ya maoni. “Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisema.
Sakata lilivyoanza
Kelele hizo zilitokana na hoja za wabunge wawili,
Suleiman Jafo wa Kisarawe na yule wa Ubungo, John Mnyika waliotaka Bunge
lisitishe shughuli zake zote lijadili suala hilo kwa kuwa ni muhimu na
Taifa halielewi hatima yake, wakati Bunge lilikuwa linaahirishwa jana.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alikataa suala hilo
kujadiliwa, akisema ni hoja iliyowasilishwa katika mkutano uliopita,
akataka Bunge liendelee na shughuli zake, lakini wabunge wa upinzani
walikataa kukaa na wakaendelea kupaza sauti.
Hata alipobadili kauli akasema, “nimesema kauli
itatolewa, wabunge hao walisisitiza itolewe papohapo. Hata alipowataka
waondoke ndani ya ukumbi huo, wabunge hao ambao ni wachache
ukilinganisha na wale wa CCM, walikataa, wakisema; “hatutoki hadi kauli
itolewe.” Kelele za wabunge hao zilimfanya Spika Makinda
kutoa kauli kali, “Njooni mwendeshe (kikao) nyinyi basi. Njooni hapa
mkae tena wote.”
Baada ya kuona kelele hizo zimedumu kwa dakika
tatu, Spika Makinda alilazimika kusitisha shughuli za Bunge hadi baadaye
(jioni), bila kutaja muda ambao Bunge lingerejea na kuwaacha wabunge
wakiwa wamesimama katika makundi ndani ya ukumbi wakijadili tukio hilo.
Jafo ndiye aliyeanza kuomba mwongozo wa Spika
akitaka chombo hicho cha kutunga sheria kisitishe kujadili jambo lolote
lile, badala yake kijadili mustakabali wa Katiba Mpya, akitaka Serikali
iwasilishe muswada wa sheria kwenye mkutano wa 20 wa Bunge (wa Bajeti)
ili Katiba ya Mpito ipitishwe.
Jafo alitaka Katiba Inayopendekezwa ipitishwe kwa mpito ili
kuondoa sintofahamu ya watu wanaotaka kuwapo mgombea binafsi, kupinga
matokeo ya urais mahakamani, kuweka ukomo wa Bunge na wabunge na kuwapo
kwa Tume huru ya uchaguzi. Alisema mambo hayo manne ambayo yamekuwa
yakipigiwa kelele yamo katika Katiba Inayopendekezwa, hivyo ni vyema
ikapitishwa kwa mpito ili mambo hayo tu manne yatumike katika Uchaguzi
Mkuu.
Alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi
kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lakini kuna
changamoto za upungufu wa vitendea kazi, zikiwamo mashine za
kielektroniki za Biometric Voters Registration (BVR). Alisema kutokana na hali hiyo, ni vigumu upigaji
Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu
kama ilivyopangwa.
Alisema upigaji kura ya maoni lazima utanguliwe na
utoaji wa elimu kwa mpigakura, jambo ambalo kwa muda uliobaki ni vigumu
kufanyika. “Tutumie mkutano wa 20 tuhakikishe Serikali
inaleta muswada wa hati ya dharura ili Bunge lipitishe katiba ya mpito,
kwa sababu Taifa sasa hivi lipo katika hali tete kila mtu anasema lake.
Endapo tutafanya hivyo tutakuwa na katiba ya mpito ya kati ya miezi sita
hadi 12, itaturuhusu kufanya uchaguzi na baadaye watu watakwenda kwenye
Kura ya Maoni wakiwa wamepata elimu ya kutosha juu ya Katiba
Inayopendekezwa.”
Alisema uamuzi huo utalinusuru Taifa na si busara kuruhusu nchi kuingia katika kura ya maoni huku kukiwa na mvutano. Baada ya kauli ya Jafo, Spika Makinda alisema:
“Ulichokizungumza wala siyo utaratibu. Kwanza suala hilo litatolewa
ufafanuzi jioni wakati Waziri Mkuu akiahirisha Bunge.”
Wakati Jafo akiomba mwongozo huo, Halima Mdee
(Kawe - Chadema), John Mnyika (Ubungo - Chadema), Felix Mkosamali
(Muhambwe - NCCR), Moses Machali (Kasulu Mjini - NCCR), Mchungaji Peter
Msigwa (Iringa Mjini - Chadema) na Mbatia walisimama bila kufuata
utaratibu na kupaza sauti wakipinga mwongozo huo.
“Hivi huyu katumwa au nini. Anazungumza vitu gani
humu ndani,” alisema Mdee na kuungwa mkono na Machali, huku wakitakiwa
kukaa chini na Makinda. Baada ya kutulia kwa mvutano huo uliodumu kwa
takribani dakika nne, Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia
kanuni ya 47 (1) na kusema: “ Mpaka sasa uandikishaji wa wapigakura nchi
nzima haujakamilika hata katika mkoa mmoja tu wa Njombe. Watanzania
wapo katika sintofahamu kuhusu ni lini wataandikishwa kwenye Daftari la
Kudumu la Wapigakura.”
Aliongeza, “Jambo hili ni la dharura kwa sababu
limeshatolewa hoja ya dharura katika mkutano uliopita wa Bunge, ukaagiza
(Spika) kamati ya bunge ilishughulikie, majibu yatolewe kwenye mkutano
huu wa Bunge. Leo hii (jana) mkutano unakwenda kufungwa bila majibu
kutolewa.” Mnyika alitaka shughuli zote za Bunge kwa siku ya jana zisitishwe na majibu juu ya masuala hayo mawili yapatikane.
Majibizano
“Nimeomba miongozo juu ya jambo hili mara mbili na
mara zote Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu umeipa maelekezo ya kutoa
majibu lakini inakwepa kutoa majibu,” alisema.
Alisema kwa mazingira hayo, hakuna sababu ya kuendelea na mjadala wowote katika kikao hicho cha Bunge mpaka majibu yapatikane, akisisitiza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya nchi, kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali. Huku akimnyooshea kidole Pinda Mnyika alisema: “Waziri Mkuu (Pinda) yupo hapa anaweza kutoa majibu na tukajadili jambo hili.”
Alisema kwa mazingira hayo, hakuna sababu ya kuendelea na mjadala wowote katika kikao hicho cha Bunge mpaka majibu yapatikane, akisisitiza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya nchi, kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali. Huku akimnyooshea kidole Pinda Mnyika alisema: “Waziri Mkuu (Pinda) yupo hapa anaweza kutoa majibu na tukajadili jambo hili.”
Baada ya Mnyika kuwasilisha mwongozo wake, Makinda
alisema: “Hoja ya Mnyika inafanana na ile iliyotolewa na Jafo.
Tuendelee Katibu (akielekeza kuendelea na ratiba za Bunge).”
Katibu wa Bunge alianza kusoma miswada minne
iliyokuwa ikisomwa kwa mara ya kwanza, ikiwamo miwili ya habari na hapo
ndipo wabunge hao wa upinzani waliposimama na kuanza kupiga kelele.
Wakiwa wamesimama, wabunge hao walianza kupaza
sauti, akianza Machali ambaye aliwasha kipaza sauti kuwa, “Hoja hii
haifanani kabisa na ile ya (Jafo), ile ya kwanza inataka majibu mkutano
wa 20 na hoja hii ya pili inataka majibu katika kikao hiki cha leo”.
Majibizano
Mnyika: Hoja hii itolewe majibu na Waziri Mkuu yupo hapa. Atoe majibu
Machali: Tunataka majibu, tumechoka kuburuzwa.
Makinda: Anawaburuza nani, nimewaambia kwamba
swali lile litajibiwa leo (jana) na Waziri Mkuu. Waziri kivuli njoo
usome hotuba ya kambi ya upinzani.
Huku wabunge hao wakiwa bado wamesimama, Spika
alimwita waziri kivuli wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
ili asome maoni ya kambi hiyo juu ya Mswada wa Sheria ya Miamala ya
Kielektroni ya mwaka 2014 na ule wa Makosa ya Kimtandao wa mwaka 2015.
Nje ya ukumbi
Hata hivyo, msemaji huyo hakwenda kusoma maoni yake na badala
yake wabunge hao waliendelea kusimama na kushinikiza kutaka majibu
kutoka kwa waziri mkuu.
Baada ya kuona hali hiyo inaendelea, Makinda
aliahirisha kikao hicho na kiliporejea saa 10 jioni, hoja hizo
hazikuendelea, badala yake miswada iliendelea kujadiliwa. Habari
zilizopatikana zilieleza kuwa Kamati ya Uongozi ilikutana na kukubaliana
majibu yatolewe katika hotuba ya kuahirisha Bunge.
Nje ya ukumbi
Wakiwa nje ya Ukumbi wa Bunge, Mbunge wa kuteuliwa
(NCCR-Mageuzi), James Mbatia na mwenzake wa Bariadi Mashariki (UDP),
John Cheyo walisema wanachokitaka kwa Serikali ni kauli tu juu ya suala
hilo na si jambo jingine.
Tofauti na ilivyozoeleka kwamba wangeitana na
kukaa kikao cha Kambi ya Upinzani, wabunge hao baada ya kutoka bungeni
kila mmoja aliondoka zake, huku wakisikika wakiambiana, “Tukutane
baadaye bungeni.”
Baadaye, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah
alisema Bunge lingeendelea saa 10 jioni, huku akitupa lawama kwa
upinzani kwamba walifanya makosa kugomea kuendelea kwa kikao cha Bunge,
badala yake kama walikuwa na hoja walitakiwa kuiwasilisha kwa Spika.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment