
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta,
amesema hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga
na chama kingine cha siasa, ingawa anavutiwa na baadhi ya sera za vyama
vinavyoeleza tunu za Hayati Mwalimu Julius Nyerere.Sitta alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu
taarifa zilizoenea kwamba anakifadhili chama kipya cha
siasa kinachojulikana kama Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (CKU)
Jumatatu iliyopita kilipata usajili wa muda. “Sera za CCM zinajitosheleza,japo navutiwa na baadhi ya vyama kama
ACT Wazalendo ambacho kinazungumzia tunu za Mwalimu Nyerere na kutetea
wanyonge,” alisema.
Alisema taarifa kwamba anataka kuhamia CKU ni uzushi na kwamba
mvuto wake aliokuwa nao kwa jamii ndio unaosababisha baadhi ya vyama
kutamani ajiunge navyo. Viongozi wa chama hicho kipya, wakisema hawatakuwa tayari kupokea
wanachama wanaotaka kujiunga nacho kutoka vyama vya upinzani na kutoa
mwaliko kwa Sitta kujiunga nacho akitaka.
Aidha, chama hicho kilijigamba kuwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba
kitajipenyeza na kupata mgombea urais atakayetoka CCM ambaye
atapeperusha bendera ya chama hicho kupambana na vyama vingine.
Mwenyekiti wa CKU, Ramadhani Semtawa, alisema ameanzisha chama
hicho kwa malengo na madhumuni ya kutaka kuirejesha nchi katika maadili
mazuri.
Alisema hivi sasa nchi inakabiliwa na matatizo kadhaa ikiwamo
ukosefu wa umoja wa kitaifa, kukithiri kwa vitendo vya rushwa, ufisadi,
ulanguzi na magendo ambavyo bado serikali haijachukua jitihada za
kutosha kupambana navyo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment