
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta
amemsimamisha kazi kwa muda mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Reli
(TRL), Kipallo Kisamfu na watumishi wengine wanne baada ya ripoti ya
uchunguzi kuwahusisha na sakata la ununuzi wa mabehewa mabovu 274 na
kulisababishia shirika hasara ya Sh230 bilioni.
Wakati kigogo huyo wa TRA akisimamishwa, Waziri
Sitta pia alitangaza kurejeshwa kazini kwa aliyekuwa akikaimu nafasi ya
mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Madeni Kipande, lakini akasema
atapangiwa kazi nyingine.
Watendaji wengine wa TRL waliosimamishwa ili
kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao ni mkurugenzi mkuu wa ndani wa
TRL, Jasper Kisiraga, meneja mkuu wa manunuzi, Fedinarnd Soka, mhasibu
mkuu, Mbaraka Mchopa na mhandisi mkuu wa mitambo, Ngosomwile Ngosomiles.
Machi 21, mwaka juzi, TRL iliingia mkataba wa
kununua mabehewa hayo aina ya Ballist Hopper Bogie (BHB) kutoka kampuni
ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited ya India yenye
thamani ya Sh4.316 bilioni kwa ajili ya kutumika katika uimarishaji wa
njia za Reli ya Kati na yaliwasili Julai mwaka jana. Hata hivyo, baada ya kuanza kazi yalilalamikiwa
kuwa hayakuwa na ubora unaotakiwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe aliunda kamati kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo na
kamati iliyo ilikabidhi ripoti yake Desemba Mosi mwaka jana na waziri
huyo kuahidi kuishughulikia bodi ya zabuni ya TRL.
Akitangaza kwa waandishi wa habari uamuzi wa
kusimamisha watendaji hao jana, Sitta alisema kamati ya uchunguzi
iliyoundwa imebaini kuwa wazabuni wa mabehewa hayo walilipwa fedha
kinyume cha masharti ya mkataba baada ya kupewa asilimia 100 ya malipo.
“Inaonekana kuwa mazingira ya utekelezaji wa
mkataba huu yana dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo
uzembe tu,” alisema Sitta. “Tutaunda kamati ya kuchunguza tuhuma zao,
itakayojumuisha ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), Takukuru na Ofisi ya Mamlaka ya
Udhibiti wa Ununuzi katika sekta ya Umma(PPRA),” alisema Sitta.
Sitta alisema kamati hiyo itafanya kazi ndani ya
wiki tatu kuanzia Jumatatu ya Aprili 20 na kwamba taarifa ya kamati hiyo
itatoa mwelekeo na ushauri wa hatua gani zifanyike ili kukomboa fedha
zilizopotea wakati wa malipo ya mabehewa hao. “Wakati naingia wizarani nilikuta tayari mabehewa
150 yameshaingia yakiwa mabovu hivyo, hivyo kwa hivyo ikanibidi
kusitisha kwanza yale mengine 124 yasiletwe,” alisema Sitta.
“Kilichonishtua zaidi ni baada ya kupitia mchakato
wa malipo ya mabehewa hayo na kukuta walishalipwa asilimia 100 yote
ikiwa ni kinyume cha mkataba, uliotaka kulipa asilimia 50 kwanza, baada
ya kumaliza kuyaingiza asilimia 40 nyingine walipwe na baada ya kufanya
kazi mwaka mmoja ndio walipwe asilimia 10 iliyobakia lakini haikuonekana
hatua hiyo.”
Kutokana na hatua hiyo, Sitta aliagiza Bodi ya
Wakurugenzi wa TRL kufanya kikao cha dharura kuteua watumishi wenye sifa
za kukaimu nafasi hizo mpaka uchunguzi utakapokamilika.
Kuhusu kurejeshwa kazini kwa Kipande, taarifa ya Wizara ya
Uchukuzi imeeleza kuwa kigogo huyo hatarejeshwa kazini kuendelea kukaimu
nafasi ya ukuu wa bandari kwa kuwa uongozi wake ulikuwa unalalamikiwa
na wateja na wadau wa bandari. “Baada ya kuisoma taarifa ya Tume na hatimaye
kushauriana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala haya,
tumeridhika pasipo shaka yoyote kwamba isingefaa Ndugu Madeni Kipande
kuendelea na kazi ya kuongoza Mamlaka ya Bandari,” inasema taarifa hiyo.
“Kutokana na hali hiyo, Serikali imeamua
kumrejesha Ndugu Madeni Kipande Idara Kuu ya Utumishi ili aweze
kupangiwa majukumu mengine,” inasema taarifa hiyo ambayo imeongeza kuwa
Awadhi Massawe ataendelea kukaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu wa mamlaka
hiyo nyeti kwa uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine, Sitta alizungumzia
changamoto ya usafiri wa treni jijini Dar es Salaam akisema kikwazo
kikubwa katika usafiri huo ni kutumika kwa mashine ziilizochakaa.
Sitta alisema kwa sasa wizara yake imeshaagiza
vichwa vya treni vinne kutoka karakana ya Morogoro ambavyo vitaletwa Dar
es Salaam kwa ajili ya safari za treni hizo zilizopachikwa jina la
“Treni za Mwakyembe”. “Pamoja na hatua hiyo pia kuna mazungumzo ambayo
tumeshafanya na kampuni ya Kifaransa ambayo itakuja Tanzania wakati
wowote kufanya uchunguzi wa miundombinu na kuangalia jinsi gani tunaweza
kuwekeza katika usafiri wa treni hapa jiji la Dar es Salaam. Kampuni
hiyo inaitwa Alstorm ambayo itafanya kazi hiyo miezi sita,” alisema
Sitta. “Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuangalia kama
miaka ijayo tunaweza kuanzisha usafiri wa treni kwenda Mbagala, Gongo la
Mboto, Temeke na Maeneo mengine ya mbali hapa jijini.”
Kuhusu Viongozi wa dini
Katika hatua nyingine, Sitta ametetea mpango wa
Serikali kuzifungia taasisi na vyama vinavyojihusha na harakati za
kuchochea makundi ya kijamii kupinga Katiba inayopendekezwa.
Juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe
alisema Serikali itaanza kufanya ukaguzi wa vyama na taasisi hizo ili
kujiridhisha na usajili wake na kutoa tahadhari kwa taasisi hizo
kujihusisha na siasa.
Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, Sitta
ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alisema: “Itakuwa ni jambo
la kushangaza sana kwa viongozi wa dini kuonekana wakishinikiza waumini
wao kutopigia kura ya ndiyo Katiba inayopendekezwa. Kama ni hivyo basi
tusingekuwa na vyama vya siasa.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment