Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi amevitaka vyama kurekebisha katiba zao kwenye kipengele
kinachoruhusu kuanzishwa kwa vikosi vya ulinzi na usalama.Vyama vyenye vikosi cha ulinzi na usalama ni Chadema chenye Red Brigade, CCM (Green Guard), CUF (Blue Guard) na sasa ACT-Wazalendo (ACT Amani).
Mutungi alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo unakwenda kinyume na Katiba ya nchi inayolipa jeshi la polisi mamlaka ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza baada ya mkutano wake na vyama hivyo
jana, Jaji Mutungi alisema katiba za vyama vingi vilivyosajiliwa kabla
hajaingia ofisini vilikuwa na kifungu kinachoruhusu kuanzishwa kwa
vikosi vya ulinzi na usalama wa mali za chama au viongozi wao wawapo
katika mikutano.
“Haturuhusu kifungu hicho kuwapo kwenye katiba za
vyama vinavyosajiliwa sasa (hakugusia ACT - Wazalendo). Hatuvifundishi
vyama vya siasa namna ya kuandaa katiba zao lakini tunasimamia kifungu
hiki kwa vile kinapingana na sheria.”
Jaji Mutungi alisisitiza kuwa vyama vya siasa
nchini havina uelewa wa sheria ya vyama vya siasa ambayo ndiyo
inayovisimamia, ndiyo maana vinashindwa kuendesha shughuli zao kwa
mujibu wa sheria hiyo.
Kauli ya polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest
Mangu alisema watapambana na vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya
vyama vya siasa wakati wa Uchaguzi Mkuu endapo vitaingilia majukumu ya
jeshi la polisi.
Alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo ni kinyume
cha sheria inayolipa Jeshi la Polisi dhamana ya kulinda usalama wa raia
na mali zao.
Alisema vikundi hivi vilianzishwa kama chipukizi
au halaiki lakini baadaye vilikuwa na kubadili malengo na kuanza
kuingilia majukumu ya polisi na kuhatarisha amani.
Maoni ya wadau
Hata hivyo, kauli za Msajili na Mangu zilipokewa
kwa hisia tofauti na viongozi wa vyama hivyo na baadhi vikiweka wazi
kuwa havipo tayari kuachana na vikundi hivyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema
vijana wa Green Guard hawaandaliwi kijeshi na kuwa tishio kama vyama
vingine, bali kuwafanya wawe vijana bora, wakakamavu na kuwajengea
uzalendo ndani ya nchi yao.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema chama
chake hakipo tayari kuivunja Red Brigade huku akiilaumu CCM kuwa
kikundi chake cha Green Guard kimepata mafunzo ya kijeshi kikifundishwa
na askari tofauti na wao ambao wanafundishwa na raia.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Nzega jana,
Mbowe alisema suluhisho la tatizo hilo haliwezi kuwa sheria bali
kuhakikisha haki inatendeka na inaonekana kutendeka kwa kila chama,
akitolea mfano jinsi viongozi wa chama hicho walivyopigwa na Green guard
bila polisi kuchukua hatua.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment