Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (kushoto) akiwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Jumamosi
iliyopita.
Mlinzi wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima jana alijisalimisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu na kusomewa mashtaka mawili ya kukutwa na bastola aina ya
Berretta pamoja na risasi 20 kinyume na sheria.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka
alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobera kuwa baada ya kuomba
mahakamani hapo hati ya wito ya kumuita mshtakiwa George Mzava (43)
Aprili 17, jana alijisalimisha akiambatana na Wakili Peter Kibatala.
Kweka aliiomba mahakama imruhusu amsomee mashtaka
ili Mei 4 aunganishwe katika kesi inayomkabili Askofu Gwajima,
msaidizi wake, Yekonia Bihagaze (39) na Mchungaji Georgey Milulu (31).
Akimsomea hati ya mashtaka, Kweka alidai kuwa
Machi 29 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, akiwa na wenzake
Bihagaze na Milulu walikutwa na bastola aina ya Berretta yenye namba ya
siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali cha mamlaka inayohusika na silaha
na milipuko.
Alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo
kinyume na Kifungu cha 32 (1) na cha 34 (1)(2) na(3) cha Sheria ya
Silaha na Milipuko, Sura ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa
siku hiyo ya tukio, Mzava akiwa na wenzake hao walikutwa wakimiliki
isivyo halali, risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki
aina ya shotgun.
Mshtakiwa huyo baada ya kusomewa mashtaka hayo aliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika.
Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya
kukamilisha masharti ya kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye
alisaini hati ya maneno ya dhamana yenye thamani ya Sh1 milioni.
Ijumaa iliyopita, Askofu Gwajima na wenzake wawili
walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka mawili na mawakili wa
Serikali, Tumaini Kweka na Shadrack Kimaro.
Askofu Gwajima anadaiwa kutoa lugha chafu kwa
Mwadhama Polycap Kardinali Pengo na kuacha silaha risasi tatu za bastola
na 17 za bunduki aina ya shotgun katika mikono isiyo salama. Wote
walikana mashtaka yote.
Kibatala aliiomba Mahakama hiyo kumruhusu Askofu
Gwajima ajidhamini katika kosa la kwanza na Hakimu Wilfred Byansobera
alikubaliana na upande wa utetezi na kumpa masharti ya kutoa Sh1 milioni
ya ahadi.
Kosa la pili aliloshtakiwa na pamoja na wenzake,
Biyagaze, Mzava, Milulu, Askofu Gwajima aliwekewa dhamana ya Sh1 milioni
na Wakili Neema Masawe.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment