Pages

Wednesday, April 22, 2015

MANGULA: KANUNI ZITAWAMEZA

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi wa chama hicho katika jimbo la Ukonga, Dar es Salaam jana.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amesema kanuni za uchaguzi za chama hicho zitawameza makada wake wanaotumia fedha kuwanunua wapigakura kama maandazi.
Mangula alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wanaCCM wa Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam katika ziara yake katika majimbo mawili ya Ukonga na Segerea.
Mangula alisema wapo wagombea wanaodhani kuwa wao ni maarufu na wanasahau kuwa fedha walizotanguliza mbele ndiyo maarufu na siyo wao wenyewe, hivyo wanajidanganya. “Unatawanya fedha kila kona, kwa kila kundi, halafu unajiita maarufu badala ya kuona fedha zako ndiyo maarufu unajidanganya ukijua kuwa unajidanganya,” alisema.
Aliwataka wanachama hao kuwa makini na watu wenye tamaa ya kwenda Ikulu, huku akinukuu alichowahi kukisema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa; “mtu yeyote anayetafuta kwenda Ikulu kwa fedha muogopeni kama ukoma.”
Akifafanua maadili na kanuni za wagombea wa CCM, Mangula anayeongoza pia Kamati Ndogo ya maadili, alisema, “Yeyote anayekukuruka kuutafuta uongozi kwa kutumia fedha, kununua wanachama ili apigiwe kura au apitishwe, akiona jina lake halikutoka ajue limemezwa na kanuni na sheria za uchaguzi.”
Kauli hiyo ya Mangula imekuja wakati kamati ya maadili anayoiongoza ikiendelea kuwachunguza makada sita wa chama hicho kwa madai ya kuanza kampeni mapema na kufanya vitendo vinavyokiuka maadili.
Alisema CCM ni umoja, hivyo wanaoleta migogoro ni watu waliopotoka ambao wanashindwa kutekeleza sheria walizojiwekea na wenye tamaa ya madaraka.
Mangula alisisitiza kuwa anayowaeleza makada hao si hadithi, bali ni ya kweli na yaliwahi kufanyika huko nyuma akitolea mfano mwaka 2000 akiwa Katibu Mkuu wa CCM walipowasimamisha wagombea wa majimbo ya Morogoro ambao wagombea sita walihonga, uchunguzi ukafanyika ilipobainika walisimamishwa wote na wahusika wakapigwa marufuku kugombea.
Alisema hata mkoani Singida makada waliobainika kusambaza fedha ili wachaguliwe walitimuliwa na nafasi ikatangazwa upya. “Wakalalamika demokrasia ipo wapi, tukawajibu hakuna cha demokrasia, unalazimisha vipi demokrasia kwa kutumia fedha?” alisema.
Alisema kutumia fedha kwenye uchaguzi ni tatizo sugu, hadi watendaji wanakula rushwa kwa wagombea mpaka wanafikia kupanga hadi bei ya hongo. “Ni aibu, watu wanajua kabisa watapata shilingi ngapi, wamepanga hadi bei ya hongo na wanachukua kila upande, wanasema ndiyo wakati wao wa kuvuna, wamekuwa malaya wa kisiasa, kutokana na kutokuwa na maamuzi wala kufuata kanuni za chama,” alisema Mangula. Alisema kutokana na kukithiri kwa tabia ya utovu wa nidhamu kwa wagombea wa CCM, hivi sasa kadi za chama ni kama keki ya moto, kila mtu anazitaka, wagombea wanawanunulia kadi wanachama, wanawalipia kadi za Jumuia ya Wazazi ili waje kuwachagua baadaye, jambo ambalo ni kosa.
Alisema kuna watu wana mawakala wa kuwasikilizia kama majina yao yamepita au la, hao wanakiuka kanuni na sheria za chama, hawana sifa ya kuwa wagombea, ikibainika watashughulikiwa.

Makundi ndani ya chama
Alisema makundi ndani ya chama yanakisababishia udhaifu, kwani vita ya panzi furaha ya kunguru, hivyo makundi hayo yanawapa nafasi wapinzani kufanya vizuri.
Alisema katika uchaguzi uliopita, wapinzani hawakushinda kwa uwezo wao, bali walishinda kutokana na kuwapo kwa makundi ya tangu baada ya uchaguzi wa mwaka 2000. “Mnataka kukiingiza chama katika udhaifu mkubwa, hakiwezi kuwa chenye nguvu iwapo kuna makundi yanayolazimisha lisilowezekana liwezekane, baada ya uchaguzi anayechaguliwa kugombea anakuwa wa CCM na siyo yeye binafsi,” alisema.

Machafuko na vurugu
Makamu mwenyekiti huyo pia alizungumzia machafuko kwa kuweka wazi kuwa katika hilo wanaotakiwa kuangaliwa ni viongozi wa dini, kwani mengi huanzia huko.
Alisema siyo dini moja, bali zote Waislamu na Wakristo “utakuta dhehebu moja halielewani na jingine na kwa Waislamu pia dhehebu hili halipatani na jingine.”
Alisema mbali na viongozi wa dini, wanaoleta machafuko wengine ni wanasiasa kwa kutaka madaraka, huku wakitumia kauli mbaya kama patachimbika, lazima kieleweke ambazo ni za kichochezi.
Alisema ikitokea hali hiyo, madhara ni makubwa na nchi itakuwa ngumu kutawalika, hakutakuwa na amani wala maelewano.
Alitolea mfano wa Somalia akisema ilikuwa nchi inayojiamulia mambo yake lakini tamaa ya kwenda Ikulu ikaleta yote hayo, ikiwamo kuwapo kwa makundi ya yaliyoishia kutukanana, kukashifiana na mwisho wa yote wakaingia katika mapigano na nchi hiyo sasa haitawaliki.
Alisema nchi kama Sudan Kusini, ilikuwa na chama kimoja cha Sudan People’s Liberation Army (SPLA), lakini kwa uroho wa madaraka ya kuingia Ikulu, kikagawanyika na kuwa makundi matatu ambayo yameiingiza nchi hiyo kwenye vurugu kubwa. “Kwenda barabarani, kutupa mawe, siasa za chuki, siyo suluhisho la matatizo bali ni kuyaongeza,” alisema.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment