
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, amewasimamisha
kazi vigogo watano wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), akiwamo Mkurugenzi
Mtendaji wake, Kipallo Kisamfu, kutokana kubainika kuihujumu serikali
katika sakata la ununuzi wa mabehewa feki 274 ya mizigo na
kuisababishia hasara ya Sh. bilioni 230.
Wengine waliosimamishwa ni Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile
Ngosomiles; Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper
Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka. Sitta alisema baada ya kuwasimamisha vigogo hao, utafanyika uchunguzi dhidi yao kwa wiki tatu kuanzia Jumatatu ijayo.
Kufuatia uamuzi huo, Sitta amemteua aliyekuwa Mhandisi wa TRL,
Elias Mshana, kuwa Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo, na kumwagiza Katibu
Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, kusimamia kuundwa kwa
kamati ya uchunguzi huo.
Alisema kamati hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) akishirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya
Umma (PPRA) pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sitta alichukua uamuzi huo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya
kamati iliyoundwa na Waziri aliyemtangulia wizarani hapo, Dk. Harrison
Mwakyembe, ambaye alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, ambayo imegundua kuwako kwa hujuma mbalimbali katika
kuendesha TRL.
Kabla ya kuchukua uamuzi wa jana, Waziri Sitta aliiagiza bodi ya
Wakurugenzi ya Reli kupitia taarifa hiyo na kutoa maelezo kwake juu ya
suala ya ununuzi wa mabehewa hayo. Aliongeza kuwa baada ya bodi kupitia taarifa hiyo, ilibaini kuwa
mabehewa mengi kati ya yaliyoagizwa nchini yalikuwa na kasoro, kuwapo
kwa uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kuanzia kiwandani yalipokuwa
yanatengenezwa na kuwako kwa uzembe katika mchakato wa kuyapokea licha
ya ubovu wake.
Sitta alisema kamati hiyo iliyokuwa ikichunguza suala hilo ilibaini
ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi na masharti ya mkataba wa
ununuzi wa mabehewa hayo ambao ulipangwa kufanyika kwa awamu tatu,
lakini malipo yalifanyika yote kwa asilimia 100.
Alisema katika makubaliano ya ununuzi, walikubaliana kufanya malipo
kwa awamu kwa kuanza na asimilia 50 awamu ya kwanza, asilimia 40 awamu
ya pili na awamu ya mwisho asilimia 10 ambayo ilipaswa kufanyika baada
ya mabehewa hayo kufanyiwa majaribio kwa mwaka mmoja.
“Siku ya Jumatatu, Aprili 13, mwaka huu, Wizara ilishtushwa na
kugundua kinyume cha taarifa za awali na masharti ya mkataba wa ununuzi
wa mabehewa hayo, kwamba malipo yangefanyika kwa awamu, lakini malipo ya
mabehewa hayo mabovu yamefanyika kikamilifu, yaani watengenezaji
wamelipwa asilimia 100 ya fedha kinyume cha masharti ya mkataba,”
alisema Sitta.
Alisema: “Mazingira ya utekelezaji wa mkataba huu yana dalili za
hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo uzembe, na pia tumebaini
haikushirikisha watendaji wa chini. Jambo hili limenisikitisha sana na
siwezi kumfumbia macho yeyote aliyehusika katika hujuma hii kwa sababu
Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimetuweka hapa kwa ajili ya kufanya kazi kwa
kutenda haki na si vinginevyo, natamani wakibainika wapelekwe mahakamani
na wafungwe kabisa.”
Sitta alisema hayuko tayari kuona watu wanaifanyia serikali hujuma kama hizo na kuahidi kupambana nao bila kumwangalia mtu. Alisema katika mkataba huo, mabehewa yaliyoagizwa ni 274 na
yaliyoletwa nchini ni 150 huku mengine 124 yakizuiliwa kuletwa baada ya
kubainika yaliyoletwa kutokuwa na ubora unaotakiwa.
Alisema wataomba ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kuangalia hatua za kuchukua kuhusiana na mabehewa hayo feki
yaliyoingizwa nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na
Biashara, Luaga Mpina, hivi karibuni alisema kamati yake iliwahoji PPRA
kuhusu ushiriki wao kwenye ununuzi wa mabehewa hayo na kubaini kuwa
mamlaka hiyo haikushirikishwa.
Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa (CCM), alisema hali hiyo
inaonyesha mambo kufanywa kinyume cha taratibu katika mchakato wa
ununuzi wa mabehewa hayo na imechangia kuingizia hasara serikali. Mabehewa hayo yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya
M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited ya India ikishirikiana
na kampuni moja nchini inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja ambaye
amekuwa akijihusisha na biashara nyingi za kulaghai mashirika ya umma na
kujipatia ukwasi wa kupindukia.
Mabehewa hayo yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa
majaribio na baadhi kuanguka kwa kukosa ‘stability’ yakiwa relini na
yaliyopokelewa na Dk. Mwakyembe Julai 24, mwaka jana, hayakupitiwa na
jopo la mafundi wa TRL ili kuthibitisha ubora wake.
KIPANDE AONDOLEWA RASMI BANDARINI
Katika hatua nyingine, Sitta, alitangaza kumuondoa rasmi kwenye
nafasi yake aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA), Madeni Kipande kwa makosa ya utawala mbovu. Aidha, Sitta amemteua Awadhi Massawe, kuendelea kukaimu nafasi
iliyoachwa na Kipande ambaye sasa atapelekwa Idara Kuu ya Utumishi
kupangiwa kazi nyingine. Sitta alitangaza uamuzi huo baada ya kupokea
ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tuhuma zinazomkabili Kipande,
kuanzia Februri 16 hadi Machi 20, mwaka huu.
Sitta alisema ripoti hiyo aliisoma na kushauriana na taasisi
mbalimbali zinazohusika na masuala hayo na kukubaliana kumuondoa katika
kazi ya kuongoza bandari. “Baada ya kuisoma ripoti ya kamati pamoja na kushauriana na taasisi
zinazohusika, tumejiridhisha pasipo na shaka yoyote kwamba isingefaa
Madeni Kipande, kuendelea na kazi hii. Hii inatokana na kudhihirika
utawala wake ni mbovu, hawezi kuiongoza Bandari kwa sababu ana mabavu na
maamuzi ya papara, ambayo yamesababisha manungu’niko kwa wafanyakazi,”
alisema Sitta.
Alisema kutokana na utawala mbovu, mamlaka ilipata manung’uniko
mengi miongoni mwa wateja na wadau wa Bandari na kusababisha mgawanyiko
kwa wafanyakazi. Kuhusu kumrejesha kazini mtumishi ambaye ameshindwa kufanya kazi
kikamilifu kazi aliyopangiwa, Sitta alisema jukumu la kumpangia kazi
inayofaa litafaywa na Katibu Mkuu Kiongozi. “Kipande amebainika hawezi kuiongoza Bandari, kwa hiyo tumemuondoa
baada ya tume kumchunguza na tukajiridhisha kwa kushirikiana na taasisi
nyingine,” alisema.
“Mamlaka ya kumpangia kazi ambayo ataweza kuifanya anayo Katibu
Mkuu Kiongozi, kwa maana hii, ni sifa mbaya ya kushindwa kuongoza sekta
ambayo amepewa,” alisema Sitta.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment