Mwenekano wa makazi ya watu katika eneo la Ilala Sharifu Shamba jijini Dar es Salaam. Karibu nusu ya
wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaishi katika nyumba za kupanga ambazo
pamoja na kuwa ni chanzo cha mapato kwa wanaozimiliki, kwa upande
mwingine ni karaha kwa wapangaji.
Utafiti uliofanywa kwa wapangaji pamoja na
madalali katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam umebaini kadhia
wanazokabiliana nazo zikiwamo masharti makali na mikataba bubu ya
upangaji. Miongoni mwa kadhia hizo ni pamoja na kufukuzwa
kwenye nyumba kabla ya mkataba kwisha, kupewa masharti magumu kama vile
kukataa wapangaji wenye watoto, kupika aina fulani ya chakula na
wamiliki wengine wakichagua wapangaji kutokana na dini zao au makabila.
Matatizo mengine ni foleni za kwenda chooni
ambacho pia ni bafu, ratiba za usafi, matatizo ya maji na nyumba
kutokufikika kirahisi. Katika maeneo ya Tandale, Kinondoni na Vingunguti
ilibainika kuwa wenye nyumba ni wepesi kuwageuka wapangaji hata kama
waliandikishiana mkataba.
“Unaweza kukubaliana na mwenye nyumba ukaingia
naye mkataba vizuri, lakini baada ya siku chache, anakwambia uondoke
wakati ulishampa kodi, anaweza kukutafutia sababu yoyote tu,” alisema
dalali wa Tandale hadi Kinondoni Studio, Nassoro Maskani.
Dalali mwingine, Saleh Mkumbila alisema kuna
nyumba ambazo wanataka wapangaji wa kike tu kwa sababu wapangaji wa
kiume wanaweza kuwarubuni mabinti wa wenye nyumba. Mkazi wa Magomeni kwa
Bibi Nyau, Selemani Kaisi (maarufu Cholo), alisema ni kawaida kukutana
na masharti mazito ya kutatanisha kutoka kwa wenye nyumba. “Si ajabu kumsikia mwenye nyumba akiwa hataki wapangaji wanaume au wanawake. Kila mmoja ana sababu zake,” alisema.
Mkazi wa Barafu, Kigogo Mburahati, Anna Yohana
alisema wapo wenye nyumba ambao wanataka wapangaji wanaume ambao
hawajaoa na wanafanya kazi. “Hawa wana faida kwa sababu hawana usumbufu
lakini hawafanyi usafi, badala yake wanatakiwa kutoa fedha ya usafi wa
choo na uwanja,” alisema Yohana.
Ujanja wa madalali
Katika biashara ya kupanga nyumba na kupangisha,
kundi la madalali linatajwa kuongoza kwa utapeli. Dalali mmoja anaweza
kuwapeleka watu 10 katika chumba kimoja kwa siku moja, kila mtu kwa muda
wake na kila mmoja anampa Sh5,000 ya udalali, kwa siku atakusanya
Sh50,000. “Yaani madalali ni wababaishaji sana na ndiyo wanaosababisha
nyumba zipande bei Sinza kwani anaweza akakutajia mazingira ya chumba
ukahisi ni kizuri sana lakini ukifika unakuta tofauti,” alisema mkazi wa
Sinza, Ruth Ahazi na kuongeza kuwa lengo la dalali ni kutaka mgawo
wake, kodi ya mwezi mmoja, uwe mkubwa. Mmoja wa madalali kutoka Sinza,
Chesco Athanas alisema huwa wanawatoza wateja fedha ya kuwapeleka
kuangalia vyumba kufidia usumbufu na muda wao. Hata hivyo, alisema yapo
baadhi ya maeneo kama Buza Barabarani, Pile, Temeke Mwisho, Mwembe Yanga
ambako kuna nyumba nzuri lakini kodi zake ni kubwa kutokana na kuwa na
kuwa salama zaidi ikilinganishwa na sehemu nyingine. “Huko ipo nyumba ya
Sh200, 000 kwa mwezi lakini gari, pikipiki unalaza kwenye kituo cha
mafuta kilichopo jirani au kwenye ofisi za chama, hizi zipo nyingi
wateja wake hawapatikani sana,” alisema dalali kutoka Tandika Yusuf
Mkumba. Katika maeneo mengi ambayo Mwananchi iliyatembelea wenye nyumba
waliweka masharti ya mpangaji kuwahi kurudi, kukataa ulevi kupita kiasi
na masharti kwa vijana ambao hawajaoa. “Vijana ambao hawajaoa
wanakatazwa kuingiza wanawake tofauti, hili wenye nyumba wanalipigia
kelele sana,” alisema Cholo. Huko Sinza, madalali wanayataja masharti
mbalimbali wanayopata wapangaji wa maeneo hayo kuwa ni kama vile
kutochoma ubani. Wamiliki wa nyumba hasa wa dini ya Kikristo wengi kwao
hili ni tatizo kidogo na kwa wenye nyumba wenye msimamo mkali wa dini ya
Kiislamu wengi wanakataza familia kubwa na unywaji wa pombe kupita
kiasi.
Mwenye nyumba atetea
Mmiliki wa nyumba iliyoko Tabata, Mawenzi,
Kashushu Kisala alisema masharti kwa mpangaji ni muhimu wakati wa
kuingia mkataba kwani bila masharti, nyumba haitadumu, haitakuwa na
heshima wala kodi haitapatikana kwa wakati. “Masharti mengine ni kwa
manufaa ya jamii nzima, kama ulevi, wanawake wengi au kuchelewa kurudi.
Huwezi kunisumbua kwenye nyumba yangu,” alisema Kisala. Matatizo ya
nyumba na upangaji yaliwahi kufikishwa bungeni, hasa kwa kipengele cha
mpangaji kutakiwa kulipa kodi ya mwaka au miezi sita kwa mkupuo wakati
mapato yake, hasa mshahara, yanapatikana kwa mwezi.
Februari 12, 2012, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba aliomba kupeleka muswada wa Sheria ya Kudhibiti Upangaji wa Nyumba za Makazi. Katika muswada huo, January ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, alitaka sheria hiyo iweke utaratibu na udhibiti wa sekta ya upangaji wa nyumba nchini kwa ujumla. Kadhalika, alitaka sheria hiyo iwezeshe kuanzishwa kwa mamlaka ya usimamizi wa sekta ya nyumba, real estate regulatory authority (Rera). “Sheria hiyo itaainisha wazi haki na wajibu wa wapangaji na wenye nyumba, pia itasaidia wapangaji na wenye nyumba kupata haki zao,” alisema January. Hata hivyo, hoja yake binafsi ilipingwa na Serikali na kukataliwa na Bunge. Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema pamoja na kuwa hoja hiyo ni ya msingi, Serikali inahitaji muda kwanza kumaliza sera ya nyumba ili vyombo stahiki vifanye kazi yake kwa kuangalia sheria gani na uhakiki utakaowekwa ili suala hilo lishughulikiwe kwa haraka.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment