Wanawake wakifanya jitihada ya kutafuta maji kwa ajili ya matumizi katika familia zao.
Taifa leo linaanza maadhimisho ya
Wiki ya Maji, lakini vilio vimetawala kila kona ya nchi kutokana na
uhaba mkubwa wa huduma hiyo muhimu kwa afya na kufanya maashimisho hayo
yaoneane kuwa ni ya kutafuta maji.
Wiki ya Maji huadhimishwa kila mwaka kuanzia Machi
16 hadi 22 kwa kujadili kero ya huduma hiyo ya msingi na kuzindua
miradi mingi, na mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa wilayani
Musoma, ambako mradi wa maji ya Ziwa Victoria bado haujawa na ufanisi
mkubwa.
Uhaba wa maji umekuwa kero sugu na ya muda mrefu
kwa wananchi katika mikoa mingi, hasa ya Dar es Salaam, Dodoma, Singida,
Mara na Tanga na Kilimanjaro, mikoa ambayo idadi yake ya watu ni zaidi
ya robo ya idadi ya watu nchini kwa mujibu wa sense ya mwaka 2012, na
juhudi za kukabiliana na tatizo hilo hazijazaa matunda.
Ongezeko la tatizo la maji linachangiwa na ukuaji
wa shughuli za uzalishaji mali katika sekta mbalimbali, hususan ni
kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji umeme, viwandani, utalii, uchimbaji
madini, ufugaji, uvuvi na hali kadhali ongezeko la idadi ya watu. Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya
maji, shughuli za binadamu zinachangia kuharibiwa kwa vyanzo vya maji,
ubovu wa miundombinu ya kusambaza maji, bajeti ndogo isiyokidhi mahitaji
ya wizara husika na mipango mibovu ya kushughulikia tatizo hilo.
Dira ya taifa ya Maendeleo 2015, Mpango wa
Maendeleo ya Milenia 2015 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini Tanzania (Mkukuta), sambamba na Programu ya Maendeleo ya Sekta
iliyoanza mwaka 2007/08 ni mikakati inayolenga kufikisha maji kwa
asilimia 100 kwa wakazi waishio mijini na asilimia 90 vijijini. Wakati takwimu za Serikali zikionyesha kuwa
asilimia 58.6 ya watu waishio vijijini wanapata maji salama na asilimia
86 ya watu waishio mijini wanapata maji safi, idadi ya watu waishio
vijijini ni asilimia 80, kitu kinachoonyesha kuwa tatizo hilo bado ni
kubwa.
“Mimi nafanya biashara saa zote, hata maji ya
Mchina (ya bomba yaliyotandazwa na Wachina) yakitoka, bado nitapata
tenda ya kuwapelekea wale wasioweza kubeba ndoo kichwani,” alisema
Hamisi China, mkazi wa Tabata anayejinufaisha na tatizo hilo kwa kuuza
maji. Wafanyabiashara hao wana uwezo wa kupata kiasi cha angalau kati ya Sh5,000 hadi 10,000 kwa siku.
Maeneo ya Mbezi Kimara kuna uhaba wa maji wa
kudumu na wakazi wa maeneo hayo hulazimika kununua maji yanayosambazwa
kwa kutumia malori licha ya bomba la maji kutoka Ruvu kupita maeneo yao. Wakazi hao hununua boza la lita 10,000 za maji kwa
Sh75, 000, wakati kwenye maeneo mengine maji hupatikana kwa Sh250 hadi
Sh500 kwa dumu moja la lita 20, kama maeneo ya Tabata. Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili
wamesema Wiki ya Maji haina maana yoyote kwao, na wengine wamesema
ingeitwa Wiki ya Uhaba wa Maji au kupendekeza fedha zinazotumika kwenye
maadhimisho hayo zitumike kuchimba visima.
Biashara ya maji
Licha ya uhaba wa maji kuwatesa wananchi walio
wengi, hasa akina mama, kwa upande mwingine umewafanya vijana wachache
kupata ajira kwa kuuza maji. Biashara hiyo imewanufaisha pia wafanyabiashara
wenye magari ya kusambaza maji, waliojenga visima na wakati mwingine
hata Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kutumia
tatizo hilo kuuza maji kwa kutumia magari badala ya kutandaza mabomba
ili huduma hiyo iwafikie wananchi kirahisi kwa unafuu.
Ahadi za maji
Mbali na ilani ya CCM ya 2010 -2015 iliyoahidi
kuwapatia maji watu wa mijini kwa asilimia 90 na vijijini kwa asilimia
65 ambayo haijatekelezwa, hata ahadi za viongozi mbalimbali kuhusu
tatizo hilo hazijatimia. Januari 2013 Rais Jakaya Kikwete alipokagua hali
ya maji jijini Dar es Salaam, aliahidi kuwa angeitisha kikao cha wadau
Ikulu kujadili suala hilo, lakini hadi sasa hajatekeleza ahadi hiyo.
Agosti 2014, Waziri wa Maji, Profesas Jumanne
Maghembe alimweleza Rais Kikwete kuwa kuna miradi 1,055 inayojengwa
nchini, kati ya hiyo miradi 250 imekamilika na inatoa huduma kwa watu
2,000 nchini. Alisema miradi mingine 538 inaendelea kujengwa
katika vijiji 540 na ingekuwa imekamilika ndani ya miezi sita na
kuwahudumia wananchi 4,000 na miradi mingine 525 ilikuwa inafanyiwa
maandalizi ya ujenzi na ingeanza kujengwa kuanzia Oktoba mwaka jana hadi
Mwachi 2015 lakini haijakamilika.
Kauli ya Serikali
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa
Wizara ya Maji, Amos Makalla alisema chimbuko lake ni uzalishaji mdogo
wa maji ukilinganisha na mahitaji ya wakazi wa Dar es Salaam, ambao
idadi yao kwa mujibu wa sense ya mwaka 2012 ni milioni 4.4. “Nafahamu tuna changamoto ya upatikanaji wa maji
katika jiji letu lakini ukweli ni kwamba uzalishaji ni mdogo. Hivi sasa
tunazalisha lita milioni 300 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Dar
es Salaam wakati mahitaji ni lita milioni 450 kwa siku, na kufanya
upungufu wa lita milioni 150,” alisema Makalla ambaye wiki iliyopita
aliahidi kuifumua Dawasco ili kupunguza ukubwa wa tatizo. Makala alisema Serikali inatarajia tatizo kupungua baada ya kukamilika kwa miradi mitatu ya Ruvu Juu, Ruvu Chini na Ruvu Mpiji.
“Tunatarajia miradi hiyo itakamilika ndani ya mwaka huu... tena
mmoja ulikuwa ukamilike mapema lakini kutokana na sababu mbalimbali
haukuwezekana. Hivyo itakapokamilika yote tutazalisha lita milioni 700
za maji kwa siku, kiasi ambacho ni zaidi ya kile kinachohitajika,”
alisema. Akiwa wilayani Igunga mkoani Tabora mwaka 2010,
Rais Kikwete aliahidi kuwa wananchi wa Tabora wangeanza kutumia maji
kutoka Ziwa Victoria na hadi sasa ahadi hiyo haijatimia.
Machi 5, mwaka huu Waziri Maghembe aliwaeleza
wanahabari kuwa mradi huo umeanza na utakamilika ndani ya miezi 30 kwa
gharama ya Dola 268.35 milioni za Marekani.
Uhaba wa maji na afya
Mei 2014, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya
utafiti kwa kushirikiana na taasisi 14 duniani na kubaini kuwa vifo
842,000 vilivyotokana na kuhara na kipindupindu mwaka
2014,vilisababishwa na uhaba wa maji. Hii ni sawa na asilimia 1.5 ya
vifo vitokanavyo na magonjwa. Katika ripoti maalumu iliyofanywa wilayani Handeni
na gazeti hili mwaka 2010, ilionekana kuwa uhaba wa maji umekuwa chanzo
cha matokeo mabaya kwa shule za wilayani humo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment