Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana ameishika nafasi hiyo tangu Novemba 2012. Kuanzia hapo hajapumzika wala kulala usingizi.
Anatembelea mikoa yote na kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Ni nadra kukosa habari za Kinana kwenye vyombo vya habari nchini, mara leo yuko Mbeya, yuko Dodoma, yuko Tanga, yuko. Yupo kila siku na yupo katika kila eneo, anapokwenda haachi kufukua mawe yaliyoota mizizi na kisha kuyapindua na kuyageuza, anasema, anaelekeza, anakemea na anapongeza.
Amejielekeza kama ni mtu huru, yuko kote kote, kwa
 wananchi na kwa chama, anauma na kupuliza. Hasiti kuikosoa Serikali 
pale anapoona imekwenda mrama, analia kilio cha wananchi bila kujali 
kama yeye ni mtendaji mkuu wa chama kinachoongoza Serikali.
Anachofanya ni kukisafisha chama mbele ya macho ya wananchi, kazi hiyo amekuwa akiifanya kwa takriban miaka mitatu sasa. Utamkuta vijijini akishirikiana na wananchi 
kujenga, kulima na hata kuhamasisha. Hivi sasa anawahamasisha wananchi 
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kisha kushiriki 
katika kupiga Kura ya Maoni.
Yuko ‘bize’, hashughulishwi na yasemwayo dhidi yake wala dhidi ya chama chake, ilimradi yeye anajua akitendacho. Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa 
alimfananisha Kinana na Karl Rove, gwiji la mikakati ya siasa wa 
Marekani. Kama Rove, Kinana ni bingwa wa stratejia na ni zaidi ya meneja
 wa kampeni.
Mwaka 2005 alikuwa meneja wa kampeni wa Jakaya 
Kikwete na alifanikiwa kumuingiza madarakani. Mwaka 2010 alihakikisha 
kuwa Rais Kikwete anaendelea kubaki madarakani.
Kuanzia mwaka 2012, Kinana amekuwa akifanya kazi 
ya kukiimarisha chama na kufufua matumaini ya wanachama. Ndiyo maana 
anazunguka nchi nzima kuwa karibu na wananchi. Wananchi wanamuona yeye 
na wanamsikia yeye, huyu ni mwenzao, anayezungumza lugha yao, lakini 
anacho anachokiwakilisha na kukiwasilisha.
Wakati vyama vingine (vya siasa nchini) vinafanya 
kampeni za kushtukiza na za zimamoto, Kinana ana stratejia makini kwa 
chama chake, hajawahi kupumzika, anapita kila penye pori na nyika, 
anatifua. Vyama hivi vitakapojikita katika kampeni za uchaguzi katikati 
ya mwaka huu, CCM zamani imemaliza kupiga kampeni, sasa itakachofanya ni
 kumnadi mgombea wake tu, kwani tayari Kinana ameshafanya kazi ya awali.
Mengine anayoyazungumza dhidi ya Serikali yake, 
yanatia shaka, hee, anaibomoa Serikali inayoongozwa na chama chake? Watu
 wanaulizana, lakini wasichokijua ni kuwa Kinana anaijenga Serikali 
ijayo.
Anakemea rushwa na viongozi wabovu, anashangazwa na ubovu wa 
huduma vijijini, anajifanya haelewi kwanini mpaka sasa maji safi na 
salama hayapatikani. Hatambui kwanini huduma za afya vijijini bado duni,
 anataka kuonyesha kwamba wananchi kupata huduma bora ndiyo kipaumbele 
cha CCM, lakini tatizo ni ubinafsi wa baadhi ya viongozi waliopo 
serikalini.
Anachofanya ni kuwaonyesha wananchi kama kwamba 
kinachofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali, CCM haijakibariki wala
 haikipendi, hivyo CCM haihusiki kwa sababu haijawatuma.
Anaendelea kuikita mizizi ya CCM mashinani, yeye 
hana habari na kilele kwa sababu anajua kuwa akiimarisha mizizi kwa 
kuimwagilia maji, kuiwekea mbolea na kuipalilia, bila shaka kilele 
kitanawiri. Wakati vyama vya upinzani vikijikita mijini na katika baadhi
 ya mikoa, CCM haichagui, iko kila pembe ya Tanzania, hawa kweli 
wanakusudia kufanya biashara.
Pamoja na ukweli kwamba vyama vya upinzani 
viliongeza ushawishi wake wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 
lakini bado CCM imefika ambako vyama vya upinzani havijafika bado. Katika baadhi ya vijiji nchini, wananchi wanawaona
 wapinzani kama ‘wahuni’ tu, na ukiwauliza kama upinzani upo watakwambia
 kuwa ‘wapo wahuni wachache’ wanaotukorofisha kidogo.’
Si ajabu pia kama utafanya utafiti kwa kuuliza 
swali kama uchaguzi utafanyika leo, wewe utachagua chama gani, 
wakakujibu: “Chama cha Mwalimu Nyerere.” Wakati wa kampeni za uchaguzi uliomuingiza George 
W. Bush madarakani mwaka 2001, Karl Rove alitumia ‘Grassroots Political 
Strategy.’ Kwa tafsiri si-si-si, grass ni majani na roots ni mizizi. 
Hivyo huo ni mkakati wa chini kabisa kuanzia kwenye mizizi inayootesha 
majani.
Kamusi ya Tuki, imeitafsiri roots kama umma. Hivyo
 anachofanya Katibu Mkuu wa CCM ni kwenda kwenye mizizi ya umma, mwanzo 
kabisa na kutengeneza msingi kwa kuuwekea zege ili uwe madhubuti.
Kwa kweli Kinana hata akipigwa madongo hayamfiki 
kwa sababu ametengeneza staili ya kuyakwepa, yeye hajibu mapigo kwa 
mdomo, bali anafanya mambo kwa vitendo. Huyo ndiye mwana-stratejia Kinana anayeyaendea 
majimbo yote ya uchaguzi, hata kabla ya uchaguzi, anaeleza dhamira, 
mipango na mikakati ya chama chake, anakipeleka chama kwa wananchi, je, 
wale wanaopiga kelele juu, wanayo nafasi?
Operesheni Sangara, Operesheni Vuguvugu la 
Mabadiliko (Movement For Change - M4C), Operesheni Pamoja Daima, 
Operesheni Zinduka, Operesheni Mchakamchaka na nyingine nyingi, ni 
operesheni za maji moto, zinaunguza kwa muda lakini hii operesheni ya 
kuijenga CCM kuanzia mashinani ni maandalizi ya muda mrefu na mazuri ya 
kushinda Uchaguzi Mkuu. Wapinzani wanapaswa wamuone Kinana kama Okwi 
anapiga mashuti na kufunga goli.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment