Pages

Friday, March 13, 2015

UMUHIMU WA UDHIBITI WA CHUMVI KWENYE MLO


Mwili wa binadamu usipopata chumvi, hauna uhai. Chumvi ni chanzo muhimu cha madini ya sodium ambayo ni muhimu sana katika mwili.
Mwili unahitaji madini ya sodium ili mfumo wa mishipa ya fahamu iweze kufanya kazi na misuli iweze kujikunja. Madini ya sodium yanasaidiana na yale ya potassium kuweka uwiano sawa wa hali ya umajimaji katika seli. Mwili una njia ya kudhibiti upotevu wa madini ya sodium, kwa hiyo mahitaji yake ya kila siku ni kiasi kidogo sana. Mtu akila chumvi kwa wingi anaongeza madini ya sodium, ambayo wingi wake unasababisha shinikizo la juu la damu.
Mtu akiwa katika hatua mbaya ya shinikizo la juu la damu mara nyingi viwango vya lehemu na sukari katika damu vinaongezeka, mishipa ya damu inaweza kupasuka, figo na moyo vinaweza kuathirika. Kiasi cha madini ya sodium kinachohitajiwa na mwili kila siku ni chini ya miligramu 1,000. Kiwango hiki kinapatikana mtu akila chumvi chini ya nusu kijiko cha chai kila siku.
Bahati mbaya, watu wengi wanakula vyakula vyenye chumvi nyingi na hivyo mwili unapata sodium nyingi kila siku. Hali hii inaongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na kiharusi. Kwa sasa nchini Marekani kila watu watatu, mmoja ana tatizo la shinikizo la juu la damu. Kipande cha samaki aina ya jodari kilichoungwa kwa chumvi kinaweza kuwa na madini ya sodium mpaka miligramu 1,300. Kiwango hiki kinazidi kidogo mahitaji ya mtu ya sodium ya kila siku.
Sasa mtu akila vyakula vingine vyenye chumvi au watu wenye tabia ya kuongeza chumvi hata hajaonja, dhahiri anapitiliza kiwango kinachotakiwa kwa siku. Tukizingatia maelezo ya hapo juu, kila mtu anaejali afya yake lazima atajitahidi kujifunza njia za namna ya kupunguza ulaji chumvi kupita kiasi, unaopelekea wingi wa madini ya sodium.
Chuo Kikuu cha Havard na Taasisi ya Taaluma ya Mapishi zote za nchini Marekani, wanaelekeza njia mbalimbali zinazokubalika kisayansi za kupunguza ulaji wa chumvi kupita mahitaji ya mwili. Moja ya njia hizo ni kuwa mlo wa mtu, nusu ya sahani yake iwe matunda na mboga za majani. Matunda na mboga za majani zina madini mengi ya potassium kuliko sodium. Mwili wa mwanadamu unahitaji zaidi madini ya potassium kuliko sodium.
Kwa hiyo, mtu akila mlo wa aina hiyo mwili wake utakuwa na uwiano mzuri wa potassium na sodium. Njia ingine inayoshauriwa na wataalamu wa Marekani ni mtu kufanya mazoezi ya ulimi wake kuzoea matumizi ya chumvi kiasi kidogo. Kiwango cha chumvi kipunguzwe hatua kwa hatua na kwa kipindi cha muda mrefu. Isiwe ghafla na kuacha kabisa kutumia chumvi, labda kwa mtu aliyeshauriwa na daktari ili kuokoa maisha yake. Wasomaji wakumbuke kuwa vyakula vina chumvi ya asili kiasi kidogo.
Njia nyingine ni kujihadhari na vyakula vyenye madini ya sodium iliyojificha. Baadhi ya vyakula vilivyotengenezwa viwandani vina madini ya sodium ambayo havionyeshi katika lebo, na ladha ya chumvi haisikiki. Mfano wa vyakula hivyo ni kama vile vinywaji vinavyoongeza nguvu au kuleta burudani katika michezo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment