Social Icons

Pages

Tuesday, March 17, 2015

'UAHRIBIFU WA BARABARA SASA BASI'

 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), Patrick Mfugale
Kituo kipya cha mzani cha Vigwaza kilichopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, kitakachoanza kutumika hivi karibuni kinatarajiwa kuwa mwarobaini wa uharibufu wa barabara unaotokana na madereva hasa wa malori kuzidisha mizigo na kupelekea baadhi ya barabara kuharibikia. Pia kituo hicho, kilichotumia Sh11 bilioni kwenye ujenzi wake kitasaidia kupunguza msongamano wa magari katika mzani wakati wa kupima mizigo tofauti na ilivyo sasa. Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale aliwaambia waandishi wa habara jana kuwa, mzani wa Vigwaza ni wa kisasa na wa kipekee nchini.
“Unaweza kupima gari moja kwa sekunde 30 badala ya dakika moja na nusu kama ilivyo kwa kituo cha zamani cha Kibaha.” Alisema, wanatarajia kwamba kituo hicho kitaonyesha ufanisi mkubwa na kuondoa matatizo yaliyopoa sasa.
Kutokana na hilo, alisema kabla ya kuzinduliwa rasmi mzani huo wataanza na majaribio ya muda. “Hivyo magari yote yatapimwa pale. Kituo cha Kibaha hakitatumika kwa muda hadi pale muda wa majaribio utakapokamilika,” alisema na kuongeza kuwa uzinduzi utafuata baada ya majaribio hayo.
Alifafanua kuwa, utaratibu za upimaji kwenye kituo hicho utakuwa wa tofauti na kwamba magari yasiyozidisha uzito yataendelea na safari na yaliyozidisha uzito yataelekezwa kwenye mzani mkubwa kwa taa nyekundu ili yapimwe.
Pia kwenye mzani huo kutakuwa na kamera za CCTV kwa ajili ya kuhakikisha hakuna ukiukwaji wa sheria. “Dereva atakayeonyesha anataka kukwepa taa nyekundu atalazimika kulipa tozo ya dola 2,000 za Kimarekani sawa na Sh3.6 milioni,” alisema.
Mfugale alisema, magari yanayotakiwa kupimwa kwenye mzani huo kwa mujibu wa sheria ya barabarani ni yale yote yenye uzito unaoanzia tani tatu hadi tatu na nusu. Pia, alitumia nafasi hiyo kuwataka madereva wanaoendesha magari hayo kuhakikisha wanaendesha magari kwenye upande unaostahili bila kukanyaga mstari mweupe, kuzingatia mwendo wa kilomita 50 kwa saa. “Madereva wahakikishe matairi yanapia juu ya ‘plates’ za mashine ya kupima uzito, magari yao yaachane kwa umbali wa mita 30.
Iwapo gari likizuia magari mengine kwenye barabara ya kuingilia kwenye mzani na hivyo kuzuia magari mengine dereva mwenye gari hilo atatakiwa kulipa faini ya Sh300,000 au kifungo kisichopungua mwaka mmoja,”alisisitiza Mfugale.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: