Rais Jakaya Kikwete.
Kikosi cha kupambana na ujangili nchini, kimebaini
mtandao wa majangili na kwamba kinafuatilia nyendo za mtuhumiwa na
anayedaiwa kuwa kinara wa ujangili nchini (jina linahifadhiwa), mkazi wa
Arusha.
Mkuu wa Idara ya Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mratibu wa kikosi hicho,
Robert Mande, aliwaeleza waandishi wa habari wa Chama cha Habari za
Utalii nchini (TJT) kuwa mtandao huo umejigawa katika makundi matano
tofauti.
Pia alisema kundi la sita la ujangili liko nje ya nchi. Rais Jakaya Kikwete aliwahi alimzungumzia kinara huyo
anayetafutwa na kikosi hicho, pamoja na kwamba Mratibu Mande hakumtaja
kwa jina lake.
Uchunguzi huo unaendeshwa chini ya kikosi hicho kinachojumuisha
vyombo vya usalama kwa kushirikiana na vikosi vya kuzuia ujangili,
katika Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA),Hifadhi ya Manyara,
Serengeti na Tarangire.
“Kundi la kwanza linahusisha wakazi wa kando kando mwa hifadhi
wanaofahamu mazingira, hivyo wanatoa taarifa mbalimbali kuhusu hifadhi
na wanyamapori,” alisema Mande. Alisema kundi la pili ni wataalam wa utumiaji silaha za moto
maarufu kama ‘Sharp Shooter’ kwa kuwa wanakabidhiwa risasi kulingana na
idadi ya wanyama wanaotakiwa kuuawa.
Alilitaja kundi la tatu, kuwa ni madalali wanaofanyakazi ya
kuwasiliana na kundi la nne, ambalo kimtandao linajengewa uwezo mkubwa
kiuchumi kwa sababu ndilo linalowasiliana moja kwa moja na majangili wa
kundi la tano, ambao ni vinara kwa hapa nchini.
“Majangili walioko kwenye kundi la nne wamegawanywa katika kanda,
wanawezeshwa kiuchumi baadhi wamenunuliwa magari aina ya Nissan Patrol
ili kuwarahisishia utendaji hata inapotokea kukamatwa, nguvu kubwa
hutumika kuvuruga kesi dhidi yao,” alieleza Mande. Mande alisema kundi la tano wanapokea oda na ufadhili kutoka kwa
kundi la sita ambao wapo nchi za nje na kuwasilisha kwa mawakala wao
ambao ni kundi la nne kwa ajili ya utekelezaji kupitia makundi
yaliyotajwa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment