Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeelezea wasiwasi
wake kuwa kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa huenda isifanyike
mwezi ujao kutokana na kusuasua kwa uandikishwaji wapiga kura katika daftari la kudumu lawapigakura mkoani Njombe.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana mjini Njombe, Mwenyekiti
wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alisema kuwaupigaji wa kura hiyo huenda usifanyike Aprili 30, mwaka huu na badala yake utasogezwa mbele
kupisha kukamilisha kazi ya uandikishaji wananchi katika daftari la
kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa kielekroniki (BVR).
Wakati Mwenyekiti huyo akisema hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
amesema serikali imekwishaipatia Nec, asilimia 70 ya fedha zote za BVR zinazohitajika na kwamba kinachotakiwa sasa ni kuandikisha
wapigakura, kazi ambayo itafanyika kwa ufanisi pindi vifaa vyote 8000
vitakapowasili.
Jaji Lubuva alisema kuwa daftari hilo ni moja kati ya hatua za
kufikia kura hiyo ya maoni ya Katiba mpya na kuwa kura haitafanyika kama
uboreshaji wa daftari hilo halitakamilika nchi nzima. “Vitu hivi vinakwenda kwa kufuatana kikikamilika kimoja kinafuata
kingine, hatutapiga kura ya maoni kama hautakamilika uboreshaji wa
daftari la kudumu la wapigakura kwa mfumo wa BVR mkoani hapa,” alisema Jaji Lubuva.
Mwenyekiti huyo alisema licha ya msimamo wa serikali kuwa kura ya
maoni ifanyike Aprili 30, mwaka huu, lakini kwa mwenendo wa
uandikishaji wapigakura italazimika kusogezwa mbele. “Ndugu waandishi mwendo wa daftari la kudumu na nyinyi mnauona,
hivyo tutatoa siku ya kupigia kura ya maoni kulingana na tutakavyoona
mwelekeo wa uandikishaji, lakini siwezi kusema sasa kuwa imeahirishwa mpaka lini,” alisisitiza.
Alisema uandikishwaji wananchi mkoani Njombe utaendelea hadi Aprili 15, mwaka huu. Kauli hiyo ni tofauti na iliyotolewa na Nec wakati uandikishaji unaendelea kuwa mkoani humo, utakamilika Aprili 12, mwaka huu. Jaji Lubuva alisema BVR kits 7,750 zipo njiani na baada ya kuwasili
zitatumika nchi nzima na ratiba itawekwa wazi na kwamba kwa mkoa wa
Njombe zinatumika 250.
Pinda wakati akizindua uandikishwaji wa daftari la kudumu la
mpigakura, Februari 23, mwaka huu, katika halmashauri ya Mji wa
Makambako mkoani Njombe, alisema vitambulisho vinavyoandikishwa vitatumika katika kupiga kura ya maoni ya katiba hiyo.
Mara kwa mara Rais Jakaya Kikwete alikaririwa na vyombo vya habari
akisema kuwa kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka huu. Tangu kuanza uandikishaji wa majaribio katika majimbo matatu ya
Kawe, Kilombero na Mlele, Desemba mwaka jana, na Februari 23, mwaka
huu, mkoani Njombe, kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya mashine
kushindwa kufanya kazi kwa muda wote, kutosoma vidole vyenye ngozi ngumu na uchache wa vifaa.
Baada ya uandikishaji wa majaribio, Nec ilitangaza kuanza na mikoa
mitatu ya Mtwara, Njombe na Ruvuma, lakini hadi sasa uandikishaji
unafanyika kwa Njombe pekee na hadi sasa haujakamilika. Jaji Lubuva amekuwa akiwaeleza waandishi wa habari kuwa BVR kits
7,750 zipo njiani na zitawasili wakati wowote kwa kuwa serikali imetoa
asilimia 50 ya fedha.
Wadau wa uchaguzi ambao ni vyama 22 vya siasa, vilivyokutana na Nec
Februari 12, mwaka huu, waliitaka kuweka wazi ratiba ya uandikishaji, mzabuni wa vifaa, kiasi cha fedha kinachotakiwa na wapiga kura wanaokadiriwa kuandikishwa kila kata. Licha ya maswali ya wadau hao, majibu ya Nec yamekuwa ni kuwa
wanaamini uandikishaji utamalizika kabla ya Aprili 30, mwaka huu, ili
daftari hilo litumike katika kura hiyo na uchaguzi mkuu.
Hali iko hivyo, huku zikiwa zimebaki siku 26, ukitoa siku za
Jumapili na sikukuu , ambazo uandikishaji haufanyiki, kufika siku ya
kura ya maoni kama ilivyotangazwa na serikali.
HALI ILIVYO NJOMBE
Machi 22, mwaka huu, wakati uandikishaji ulipokamilika katika mji
wa Njombe, baadhi ya wananchi hawakuandikishwa kutokana na nyongeza ya
siku moja kutotosheleza kutokana na uchache wa vifaa. Mkazi wa Njombe, Freddy Kifasi, ameomba kuongezwa kwa muda zaidi
kwa kuwa alifika kituoni siku ya mwisho lakini hakufanikiwa kutokana na utaratibu uliopo kumtaka kuandikisha jina siku ya Jumapili na kwenda kuandikishwa Jumatatu, utaratibu ambao alidai hakuufahamu.
Msimamizi wa uchaguzi katika mji huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa
mji wa Njombe, Venance Msungu, alisema hakuna nyongeza ya muda na kuwataka wananchi kuwa na subra hadi nec itakapotangaza nyongeza ya muda.
PINDA: SERIKALI IMEJIPANGA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema serikali imejipanga
kuhakikisha uboreshaji wa daftari la wapigakura kwa mfumo BVR,
unafanikiwa hivyo kila kata itapelekewa seti mbili au tatu ya vifaa hivyo. Akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Bunge mjini
Dodoma jana, alisema hadi mwezi ujao, uandikishaji utakuwa umeanza nchi nzima.
Hata hivyo, Pinda hakueleza ni lini vifaa hivyo vitawasili nchini kwa kuwa wanaosimamia jambo hilo ni Nec yenyewe. “Uandikishaji kule Njombe umekwenda vizuri na tumejifunza kwamba
maeneo ya mijini BVR ziwe nyingi tofauti na vijijini kwa sababu presha haikuwa kubwa vijijini kama mjini. Kwa sasa tunaona kila Kata
tukiandikisha kwa siku saba na tukawa tumepeleka BVR mbili au tatu, zoezi litakwenda vizuri,” alisema.
Kuhusu kamati za kampeni kuhusu Katiba inayopendekezwa ambazo
zinapaswa kuanza kazi Aprili Mosi, Pinda alisema jambo hilo
linashughulikiwa na Nec, lakini serikali imejipanga kuhakikisha kura ya maoni inafanyika Aprili 30, kama ilivyopangwa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment