Pages

Tuesday, March 31, 2015

MUSUSA MWENYEKITI MPYA MCL

Mhasibu mzoefu nchini, Leonard Mususa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), akichukua nafasi ya Zuhura Muro.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alimpongeza Mususa kwa uteuzi huo akisema ujuzi wake unahitajika zaidi katika kipindi hiki ili kuikuza na kuiendeleza kampuni. “Mususa amekuja Mwananchi wakati mzuri ambao kampuni inahitaji ujuzi wake, akiwa Mwenyekiti wa Bodi, atasaidia kuikuza na kuiendeleza,” alisema Nanai. Kampuni ya MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Alisema katika siku za karibuni, MCL imepitia changamoto nyingi hasa baada ya Serikali kupunguza bajeti katika matangazo, wafanyabiashara kutangaza zaidi katika runinga na redio na mabadiliko ya namna wasomaji wanavyopata habari (kukua kwa mawasiliano kwa njia ya teknohama). “Haya yote yana athari kubwa katika sekta ya habari, changamoto hizi zinaathiri idadi ya usambazaji wa magazeti na mapato. Hata hivyo, MCL imejitahidi kupambana na changamoto hizo na kuendelea kushika usukani katika sekta zote, usambazaji, mapato na matangazo,” alisema Nanai.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Nation Media Group (NMG), kampuni mama ya MCL, Wilfred Kiboro alimkaribisha Mususa kwenye Bodi ya MCL na NMG na kusema kampuni imebahatika kumpata mtu mwenye ujuzi na weledi. “Mususa ameungana nasi katika kipindi chenye changamoto nyingi lakini pia ni kipindi chenye fursa, tunautegemea zaidi mchango wake ili kuwa na gazeti lenye weledi katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Kiboro.
Akizungumzia uteuzi wake, Mususa aliipongeza MCL akisema imekuwa ikifanya kazi nzuri na kujenga soko imara kwa miaka mingi. “Ninapongeza timu ya MCL, wakurugenzi, wafanyakazi na bodi kwa kile walichokipata katika kipindi hiki chote kigumu hapa nchini,” alisema.
Mususa aliyewahi kuwa Mwakilishi mwenza wa Kampuni ya Ukaguzi ya Price Housewater Coopers Ltd nchini kwa miaka 14, alisema akiwa ndani ya MCL atahakikisha wasomaji wanapata kilicho bora. Akizungumzia mikakati kazi ndani ya MCL, mwenyekiti huyo alisema: “Tutatathmini dhamira ya magazeti yetu, tutaangalia nyanja za usambazaji na kuhakikisha idadi kubwa ya wasomaji wanapata habari zetu na habari zetu zinapatikana katika majukwaa mengine ya kihabari.”
Alisema MCL itaendelea kuandaa timu ya waandishi bora wenye ujuzi wa juu wa mawasiliano ambao wanaelewa mahitaji ya kihabari ya wasomaji wao. “Nataka MCL iendane na mabadiliko yaliyopo katika sekta ya habari. Haina budi kutoa habari za uhakika na sahihi kwa wasomaji,” alisema.
Wajumbe wengine wa Bodi ya MCL ni Profesa wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Palamagamba Kabudi, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Foundation for Civil Society, John Ulanga; mhasibu, Hanif Jaffer na mfanyabiashara na mhandisi, Mohamed Rweyemamu.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment