Social Icons

Pages

Wednesday, March 25, 2015

MISWADA YA HABARI: WADAU SASA WAMWANGUKIA SPIKA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Wakati miswada miwili ya habari ya mwaka 2015, wa Haki ya Kupata Taarifa na ule wa Huduma za Vyombo vya Habari ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki ijayo chini ya hati ya dharura, wadau wa habari wamewasilisha ombi maalum kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, wakimuomba atumie hekima zake kuishauri serikali kuiwasilisha katika mfumo wa kawaida.Kwa mujibu wa maombi hayo, wadau hao ambao wamejichimbia Dodoma tangu Jumamosi iliyopita wamemuomba Spika kutumia madaraka yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi kuishauri serikali kuwasilisha miswada hiyo katika utaratibu wa kawaida ili kutoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao kabla ya kupitishwa kuwa sheria.
Barua pia imeandikwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, ikimuomba naye aone umuhimu wa wananchi kushiriki kutoa maoni katika miswada hiyo kabla ya kupitishwa na Bunge kwenye mkutano wa 19 unaoendelea mjini Dodoma.
Naye Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ameandikiwa barua na wadau hao wakimuomba atumie nafasi yake kama msemaji mkuu wa kambi hiyo bungeni kuishauri serikali iwasilishe miswada hiyo chini ya mfumo wa kawaida na siyo chini ya hati ya dharura kwani unawanyima wananchi fursa ya kutoa maoni yao kwenye miswada hiyo kabla ya kupitishwa na Bunge.
Tangu serikali iseme kuwa inakusudia kuwasilisha miswada hiyo chini ya hati ya dharura, wadau wa habari wamekuwa wakiomba ibadili msimamo kwani kufanya hivyo kutawanyima wananchi fursa ya kutoa maoni juu ya miswada hiyo kabla ya kuwa sheria.

CHANZO: NIPASHE

No comments: