Social Icons

Pages

Wednesday, March 25, 2015

KODI ZA MABAGO ZAWAKERA WAFANYABIASHARA


Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA), mkoani Morogoro kimesema baadhi ya sheria ndogo zinazotungwa na halmashauri, zimekuwa zikiwakandamiza wafanyabiashara na kusababisha migogoro baina yao na vyombo vingine vya Serikali.
Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro, Bachoo Sidik wakati akifungua mdahalo wa wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya kilimo cha biashara ulioandaliwa na East Africa Business Media Training Institute (EABMTI) na kufadhiliwa na Taasisi ya Biashara na Mazingira (Best Diologue).
Bachoo alisema baadhi ya sheria hizo ni pamoja na sheria na ulipiaji mabango ya biashara, ambapo wafanyabiashara hutakiwa kuyalipia na wasipofanya hivyo huvunjwa au kuondolewa. Alisema sheria hiyo ndogo ya halmashauri inapingana na sheria mama ya biashara iliyotungwa na Bunge, inayomtaka mfanyabiashara kuweka bango linalotambulisha bidhaa au huduma anazotoa bila malipo yoyote.
Bachoo alisema kutokana na mkanganyiko wa sheria hizo, wafanyabiashara wamejikuta kwenye migogoro na halmashauri ambayo huvunja mabango yasiyolipiwa. Akichangia, mfanyabiashara Shabani Kaigai alisema ukadiriaji wa kodi TRA umekuwa kero kutokana na ukweli kuwa makadirio hayaendani na kipato halisi cha wafanyabishara.
Alisema kuwa TRA wamekuwa wakikadiria kodi kubwa na kusababsisha wafanyabiashara kufunga biashara zao, huku wengine wakitoa rushwa ili kupunguziwa kodi ama kukwepa kuilipa kabisa. Ofisa Kodi wa TRA Mkoa wa Morogoro, Bashiru Kahenaki alikiri kupanda kwa kodi. Hata hivyo, alisema TRA imekuwa ikiwashauri wafanyabiashara kuwa na taarifa sahihi za biashara zao, ikiwa ni pamoja vitabu vya risiti vinavyoonyesha mauzo yaliyofanyika.
Alisema wafanyabiashara wengi hawawasilishi taarifa zao kupitia vitabu vya risiti, huku baadhi wakikosa uaminifu na kukwepa kulipa kodi. Awali, Mkuu wa mdahalo huo kutoka EABMTI, Rosemary Mwakitwange alisema mdahalo unaendeshwa ili kubaini changamaoto za mazingira ya biashara na vipaumbele kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: