Pages

Monday, March 16, 2015

KITUO CHA MZANI KIBAHA KUFUNGWA

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale.
Serikali imesema kuanzia kesho kituo cha mzani cha Kibaha kitafungwa na magari yote yataendelea kupimwa kwenye kituo kipya cha Vigwaza kilichopo Mkoa wa Pwani.
Pia inatarajia kutumia Sh. bilioni 8 kujenga mizani mipya mitano ya kisasa katika maeneo mbalimbali ikiwamo eneo la Mikese, Dumila, Nala mkoani Dodoma, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katika maeneo ya mizani.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, aliyasema hayo wakati wa utoaji wa taarifa juu ya kuanza kutumika kwa mzani mpya wa Vigwaza. Mfugale alisema kesho Serikali itakifunga rasmi kituo cha mzani cha Kibaha na magari yote yataendelea kupimwa kwenye kituo kipya cha Vigwaza.
Alisema kituo hicho ni cha kisasa chenye mtambo wa kuchambua magari yaliyozidisha uzito yakiwa yanatembea. Pia, alisema kituo hicho kina mzani mkubwa unaoweza kupima gari lote kwa mkupuo.
“Aidha barabara za kuingia kwenye mzani huo wenye urefu wa kilomita 1.8 zimejengwa kwa zege lenye uwezo wa kudumu kwa miaka 50 na una uwezo wa kupima gari moja kwa sekunde 30 badala ya dakika 1.5 kwa mzani wa zamani,” alisema Mfugale.
Mfugale alisema magari yanayotakiwa kupimwa kwa mujibu wa sheria ni yote yanayoanzia tani tatu na nusu, na kuongeza kuwa gari na gari yaachane kwa mita 30. “Magari yote yazingatie mwendo wa kilometa 50 kwa saa, na gari litakalozuia magari mengine kwenye barabara ya maingiliano ya mzani na kuzuia magari mengine kupima yatalipishwa faini ya Sh. 300,000 au kifungo cha mwaka mmoja,” alisema Mfugale.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment