Pages

Wednesday, March 25, 2015

KINANA AWATULIZA WANAKIJIJI WANAOPAKANA NA KIA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Wananchi wa vijiji vinane vinavyopakana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA), wametakiwa kuendelea na shughuli zao mpaka hapo serikali itakapotafuta ufumbuzi wa mgogoro kati yao na uwanja huo.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana (pichani), kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mtakuja wilayani humu juzi. Kinana alisema mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi na  kampuni ya Kilimanjaro Airports Development Company (Kadco), unahitaji ufumbuzi wa haraka.
Alisema atahakikisha analifikisha suala hilo katika kikao cha juu ambacho Mwenyekiti wake ni Rais Jakaya Kikwete, ili utolewe uamuzi ya haraka huku akisisitiza kuwa eneo wanalomiliki KIA kwa sasa bado lina nafasi kubwa. “Naomba mtulie na muendelee na shughuli zenu kama kawaida huku Chama Cha Mapinduzi kikiendelea kulipeleka suala hili katika vikao vya uamuzi wa juu," alisema Kinana.
“Niliwahi kusema sera ya ubinafsishaji si mbaya, lakini kuwauzia watu maeneo wasiyoyatumuia si sawa, Kadco wana uzoefu wanaweza kuleta ndege, biashara na hata ajira, lakini ninachosema watuonyeshe vizuri hekta 460 zimetumikaje kabla hawajachukua nyingine za ziada,” alisema Kinana.
Awali, mwakilishi wa kijiji hicho, Steven Laizer, alisoma risala mbele ya Kinana ambayo ilijaa malalamiko dhidi ya serikali hasa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutaka kupora eneo lao takatifu ambalo kwa mujibu wao, ndipo jamii ya Maasai ilipoanzia.
Alisema Kadco inadai wananchi hao wamevamia ardhi yake yenye ukubwa wa hekta 11,085, wakati siyo kweli kiuhalisia kampuni hiyo inajaribu kuvipora vijiji hekta 11,448.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment