Askofu Mkuu Jimbo kuu la Dar es Salaam, Polycarp Pengo.
Kanisa Katoliki Tanzania, limepinga rasmi kufanyika
kwa Kura ya Maoni April 30, na limeshauri zoezi la kupitisha Katiba
Inayopendekezwa lipewe muda zaidi, au liahirishwe hadi baada ya uchaguzi
Mkuu, wa Oktoba mwaka huu.
Msimamo wa kanisa hilo, umetolewa kwenye Barua ya Kichungaji ya
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), iliyosomwa jana kwenye
baadhi ya parokia na vigango vya Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, na
baadhi ya majimbo mengine.
Akisoma barua hiyo mbele ya waumini, Padre Venance Tegete, wa
Parokia ya Mtakatifu Agostino ya Ukonga, aliungana na maaskofu kuwataka
waumini kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa, iwapo muda zaidi
haitatolewa au kuahirishwa hadi baada ya uchaguzi, kama walivyoshauri
maaskofu.
“Mchakato mzima wa katiba inayopendekezwa, una kasoro nyingi,
zikiwamo zile za muda wenyewe kuwa mfupi, usambazaji wa nakala za katiba
inayopendekezwa hauridhishi, na maoni mengi yalitolewa na wananchi
yameachwa,” alisema.
Padre Venance alisema, iwapo Kura ya maoni haitaahirishwa au
kuongezwa muda, basi wananchi wajiandikishe kwenye daftari la kudumu la
wapiga kura, na wakaipigie kura ya hapana, katiba inayopendekezwa. Makanisa mengine ambako barua hiyo ilisomwa jimboni Da r es Salaam,
ni Parokia ya Mbezi Louis, Mji Mpya Relini, Kipunguni, na Kigango cha
Wazo Hill.
Barua hiyo ya kichungaji pia ilisomwa pia katika Jimbo Katoliki la
Iringa, kwenye parokia za Mtakatifu Consolata, mjini Iringa, Parokia ya
Moyo Mtakatifu wa Yesu, na parokia ya Kihesa. Aidha kwenye jimbo Katoliki la Bukoba, barua hiyo ilisomwa katika parokia zote za jimbo hilo.
Katika barua hiyo, iliyosainiwa na Rais wa TEC, Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa, Kanisa Katoliki limesema, limefikia msimamo huo, kutokana
na mashaka mbalimbali juu ya namna mambo yalivyoendeshwa, hadi
kupatikana kwa katiba inayopendekezwa.
“Hadi sasa, katiba inayopendekezwa haijawafikia wengi, na kuwa
hatua muhimu mno ambayo ni kuelimisha watu juu ya katiba inayopendekezwa
haijafanyika, kwa hiyo wananchi wengi, hawana ufahamu wa kutosha, juu
ya maudhui na misingi yake,” ilisema
Inasema, zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la
kudumu la wapiga kura, halijafikia hatua yenye mwelekeo wa
kulikamilisha. Ilisema hatua hiyo inawapa mashaka makubwa sana, na kwamba hawawezi
kuamini kama zoezi hilo litakamilika, kabla ya tarehe ya kupiga kura ya
maoni. “Katika hali hii tunabaki na mahangaiko, na mashaka makubwa ya
kutakiwa kupigia kura katiba inayopendekzwa, ambayo hawaielewi
kikamilifu, wala kujua matokeo yake, kwa mustakabali wa taifa letu.”
Inasema bahati mbaya sana wanasiasa viongozi wa nchi, wanaendelea
kutoa maelezo ya kisiasa, yanayotoa majibu mepesi kwa maswali magumu,
kwa lengo la kufanikisha malengo yao binafsi ya kisiasa.
“Huu si muda wa kufanya hivyo,” ilisema. Ikizungumzia msimamo wa TEC juu ya mpango wa kura ya maoni, inasema: “Tuangaliapo hali ya nchi yetu leo, tunapata hofu kwamba,
uharakishwaji wa zoezi hili unaongeza fadhaa, na mpasuko ambao tayari
upo katika jamii yetu,” inaeleza.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment