Pages

Wednesday, March 25, 2015

CWT ISITOE MAJIBU MEPESI KWA MASWALI MAGUMU


Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ni chama kilicho mstari wa mbele kuhakikisha walimu nchini wanapata stahili zao kwa wakati.
Pamoja na ukweli kuwa CWT imejitahidi katika kutekeleza wajibu huo, bado ina upungufu kadhaa wa kimuundo na kiutendaji. Makala haya yanaangazia baadhi ya masuala kama vile uanachama, makato ya ada ya uanachama na muundo wa benki ya walimu kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Nimekuwa nikiandikamara nyingi kuhusu uanachama wa mwalimu katika CWT. Katiba inasema wazi kuwa kuna aina tatu za wanachama; mosi ni wanachama wa heshima ambao hupewa uanachama kutokana na mchango wao kwa CWT. Aina ya pili ni uanachama wa hiari na tatu ni wanachama halisi ambao wanatoa ada ya uanachama kila mwezi.Upungufu uliopo katika kipengele cha wanachama ni katiba kutotoa maelezo ya kutosha kuonyesha namna ya upatikanaji wa hao wanachama halisi.
Makato ya ada ya uanachama ni upungufu mwingine wa CWT. Tangu nimeifahamu CWT, haijawahi kuwa na kiwango sawa cha makato ya ada ya uanachama kwa wanachama wake. CWT imekuwa ikikata asilimia mbili ya mshahara wa kila mwalimu kila mwezi. Uvunaji wa fedha za walimu isivyo halali kila mwezi, hutufanya tujiulize; hivi CWT ni kwa masilahi ya nani?
Ni chama kilichoanzishwa kwa ajili ya kutetea na kulinda maslahi ya wanachama wake au ni chama cha kutetea maslahi ya viongozi wake na hata Serikali? Nasema CWT kinavuna fedha za walimu isivyo halali kutokana na ukweli kuwa, kwa sheria zilizopo CWT hakina mamlaka ya kuchukua ada ya uanachama kwa asilimia ya mshahara wa mtumishi.
Hata sheria ya ajira na uhusano wa kazi ya mwaka 2004, haisemi kuwa wanachama wakatwe kwa asilimia kwenda kwenye chama chao. Kwa mantiki hiyo, CWT kimekuwa kikivuna mabilioni isivyo halali kila mwaka kutoka kwa walimu pasipo ridhaa yao. Hapo juu, nimeeleza kuwa kuna walimu ambao kimsingi hawajawaridhia makato ya mshahara wao kwenda CWT lakini wamekuwa wakikatwa. Kuanzia Septemba mwaka jana baadhi ya walimu hao wameondolewa makato hayo na baadhi wakiendelea kukatwa.
Pamoja na viongozi kutambua CWT imekuwa ikipata mgawo kutoka hazina kama makato ya ada ya uanachama kwa walimu hao ambao kwa sasa hawapo katika makato, waliamua kuweka “kizingiti”. Kizingiti hiki kilihusu walimu hao ili wasipate fursa ya kuchagua au kuchaguliwa hata kama walikuwa wakikatwa ada kwa muda mrefu kiasi gani.
Hii si sawa hata kidogo! Jambo hili linaleta maswali zaidi ya majibu yanayotolewa kiasi cha kufanya wengine tupoteze imani kwa chama. Viongozi wa CWT wanakiri kuwa kuna walimu wameondolewa makato ya ada ya uanachama na njia pekee ya uchangiaji inayotumiwa ni mwajiri kukata mshahara wa mwalimu na kupeleka katika chama. Ikiwa makato hayo yamesimamishwa, je, ni nani anayewajibika na kusimamishwa huko ikiwa mwalimu hajawahi kuomba kusimamishiwa makato?
Je, ni halali mwalimu kunyimwa haki ya kushiriki shughuli za chama wakati ameshachangia zaidi ya miaka 10?
Ikiwa alikatwa kimakosa,(kama hajawahi kuridhia makato hayo), kwa nini chama kisirejeshe makato hayo kwa mwalimu husika?
Je, CWT haioni kuwa si sahihi kumzuia mwalimu aliyechangia kushiriki katika shughuli za chama? Uanzishwaji wa benki ya walimu ni wazo zuri ninaloliunga mkono. Viongozi wa CWT wanapita maeneo ya kazi kuhamasisha walimu kununua hisa ili umiliki wa benki hiyo, kwa sehemu kubwa uwe chini ya walimu.
Aidha, taarifa zinaeleza kuwa kila mwanachama hai wa CWT atanunuliwa hisa kupitia michango yake ya kila mwezi aliyoyochangia. Hofu yangu bado ipo kwa walimu ambao wameondolewa katika makato hayo.
Je, hawa hawana haki ya kushiriki pia katika shughuli za benki ya walimu?
Vipi kuhusu hatma na thamani ya michango waliyokwishachangia tangu zamani? Walimu tunahitaji majibu yenye mashiko kutoka CWT. Naandika makala haya kwa CWT na walimu kwa jumla, kwa kuwa naamini kwamba kitendo cha kuwanyima fursa walimu kushiriki kikamilifu katika shughuli za CWT ni jibu rahisi kwa maswali magumu. Naamini walimu ni waelewa na wenye hekima. Watatumia busara zao kulitathmini jambo hili na kulitafutia ufumbuzi.
Aidha, nawaandikia Watanzania kwa kuwa naamini kuwa wao ni watu makini na wenye busara ambao hawapo tayari kuona uonevu ukifanywa katika jamii yao.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment