
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa
msaada wa mabati 850 ikiwa ni ahadi iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama
hicho, Freeman Mbowe, kusaidia waathirika wa mafuriko katika kijiji cha
Mwakata wilayani Kahama.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk. Willibrod Slaa (pichani), alisema msaada huo una thamani ya Sh.
milioni 12. Dk. Slaa alifafanua kuwa kati ya kiasi hicho cha fedha zilizonunua
mabati, Sh. milioni 10 ni sehemu ya ruzuku inayotolewa na serikali kwa
chama hicho na kiasi kingine ni michango iliyopatikana katika mikutano
ya hadhara ya chama hicho iliyofanyika mjini Kahama.
Alisema waliamua kununua mabati hayo kutokana na kamati ya mkoa
inayoratibu maafa hayo ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally
Rufunga, kupendekeza vinunuliwe vifaa vya ujenzi kutokana na chakula
kuwapo cha kutosha. Dk. Slaa aliwataka viongozi kuhakikisha wanasimamia vema ujenzi wa
nyumba za kuduma za makazi ya wananchi wa kata ya Mwakata kama
ilivyopendekezwa na Rais Jakaya Kikwete, alipotembelea waathirika hao
kwani mara nyingi serikali imekuwa ikishindwa kutekeleza kwa wakati
majanga kama hayo.
“Niwaombe viongozi wa mkoa kusimamia waathirika hawa wajengewe
nyumba kwa muda mwafaka. Watanzania wengi tanawakatisha tamaa kutokana na
kushindwa kutimiza ahadi zinazotolewa kama kule Kilosa hadi leo bado
watu wanaishi kwenye mahema, tangu nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge, naomba sana Shinyanga muwe wa mfano,” alisema Dk. Slaa.
Katika hatua nyingine, misaada imeendelea kutolewa kwa waathirika
hao baada ya Kampuni ya Simu (TTCL), kutoa chakula na vitu mbalimbali
vyenye thamani ya Sh. milioni tatu. Meneja wa TTCL Mkoa wa Shinyanga, Peter Kuguru, alisema kampuni
yake imeungana na Watanzania wengine walioguswa na maafa hayo kutoa
msaada wa kibinadamu na kuyaasa mashirika mengine na watu mbalimbali
kujitokeza kuwasaidia wananchi hao.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment