Bandari ya Tanga inadaiwa kukabiliwa na
changamoto ya utendaji hafifu wa Shirika la Reli na kuchangia kwa
kiwango kikubwa kuhamishwa kwa shehena nyingi iliyokuwa ikipitia katika
bandari hiyo, hasa iliyokuwa ikienda na kutoka Kanda ya Ziwa.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Moshi Mtambalike
alisema kuwa, tangu 2009 hakuna shehena iliyosafirishwa kwa njia ya
reli hadi sasa. Mtambalike alisema hayo wakati akitoa taarifa ya
utendaji kazi wa Bandari ya Tanga katika kipindi cha mwaka 2013/14
kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC). Alisema mtiririko wa meli na shehena kwa mwaka
2012/13 ulikuwa na jumla ya meli za kimataifa 83 na za mwambao 140,
wakati kwa mwaka 2013/14 zilikuwa meli za kimataifa 68 na za mwambao 41.
Alitaja mabadiliko ya teknolojia ya muundo wa meli
nyingi mpya ambazo zinajengwa bila kuwekwa vifaa vya kupakulia mizigo
kuwa ni tatizo jingine.
Alisema kina kidogo cha maji kinachofanya meli
kubwa kushindwa kutia nanga kinasababisha kuhudumia shehena mbili kwa
wakati mmoja na kudai kuwa Mamlaka ya Bandari inatafakari namna ya
kupata treni inayoelea ili kumaliza changamoto hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula alimwomba
meneja huyo kutolea ufafanuzi wa madai ya kuwapo kwa urasimu
unaosababisha wateja kuacha kutumia bandari hiyo, suala alilokanusha. na kusema kwa sasa wamejipanga kutoa huduma bora kwa wateja wao licha kuwapo kwa changamoto hizo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment