Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia
akizungumza na waandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi
Communications Limited alipotembelea makao makuu ya kampuni hiyo, Dar es
Salaam jana.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia amesema magazeti ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), yanasomwa na kuaminiwa na wananchi, hivyo yaendelee kufanya kazi kwa weledi. MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, ambalo ni gazeti la michezo na burudani.
Waziri Nkamia, ambaye katika hali isiyo ya kawaida
alihudhuria kikao cha kutathmini gazeti kinachofanyika kila siku
asubuhi kwenye ofisi za makao makuu ya MCL, Tabata Relini, aliwataka
aliwataka waandishi kufanya kazi kwa weledi ili kudumisha imani ya
wananchi kwa gazeti hilo sambamba na amani ya nchi kwa kuwa ndiyo gazeti
linalosambaa kwa haraka na kwa wingi katika maeneo mengi nchini.
“Gazeti lenu linafika sehemu kubwa ya nchi hii,
ukienda Mwanza saa hizi (saa 2:00 asubuhi) utalikuta. Mkiamua kupotosha
mtaivuruga nchi hii. Sitarajii kama mtafanya hivyo. Endeleeni kuwa
makini katika kazi yenu,” alisema Nkamia ambaye kitaaluma ni mwandishi
wa habari.
Mbunge huyo wa Kondoa Kusini alisema katika
kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, baadhi ya magazeti yameanza
kuibuka huku mengine yakitumiwa na baadhi ya watu kuwachafua wengine kwa
malengo yao ya kisiasa. Aliongeza kuwa, siyo nia ya Serikali kukifungia
chombo chochote cha habari, lakini kikikiuka utaratibu na sheria,
Serikali haitasita kuchukua hatua kama inavyofanya.
Naibu waziri huyo alibainisha changamoto kubwa
inayoikabili wizara hiyo kuwa ni kukosekana kwa sheria inayoweka uwiano
sawa kati ya Serikali na vyombo vya habari.
“Uhusiano kati ya Serikali na vyombo vya habari
siyo mzuri sana kwa muda mrefu. Sasa tumeandaa muswada ambao ukipitishwa
utasaidia kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili hizi,” alisema Nkamia
na kuongeza kuwa katika muswada huo pia wanataka kuwe na bodi
itakayokuwa ikisimamia vyombo vyote vya habari nchini. Nkamia aliwataka waandishi kujiheshimu ili tasnia
nzima ya habari nchini iheshimike tofauti na hali ilivyo sasa. Alisema
kuna waandishi ‘makanjanja’ wanaotegemea kupewa fedha wakati wa
kukusanya habari.
“Katika muswada huu tunalenga kila mwandishi wa
habari awe na ajira. Kwa hiyo waandishi wa habari ni wadau wakubwa wa
sheria hii tunayotaka kuianzisha, hamna budi kutuunga mkono ili
tufanikishe,” alisisitiza.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah
Mwambene ambaye aliongozana na Naibu Waziri Nkamia, alisema uendeshaji
wa magazeti unahitaji umakini mkubwa katika kuripoti.
Alisema gazeti la Mwananchi limekuwa likizingatia hilo kwa kiasi kikubwa hali inayofanya lijijengee imani kubwa kwa wananchi. Alisema magazeti ni sekta inayotoa ajira kwa wingi kama ilivyo
kwenye viwanda. Awali, akimkaribisha Waziri Nkamia, Mkurugenzi Mtendaji
wa MCL, Francis Nanai alielezea kufurahishwa kwake na ziara hiyo ya
kiongozi wa serikali kwenye ofisi za Mwananchi.
CHANZO: MWANANCHI
Alisema ndoto aliyokuwa nayo siku nyingi ni kukaa
na viongozi wakubwa na kubadilishana nao mawazo jinsi ya kuboresha
utendaji wa kazi. “Tunajua waziri ana ratiba ngumu, lakini ameweza
kutenga muda wake na kuja kututembelea. Tunakushukuru na tunaahidi
tutafanya kazi kwa weledi,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment