Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon, imesema kwamba wafungwa watano
katika gereza la Marekani la Guantanamo wamepelekwa katika nchi
nyengine. Wanne kati ya hao wamepelekwa Oman na mwengine nchini Estonia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara ya ulinzi ya Marekani, wafungwa
wanne waliopelekwa katika falme ya Ghuba ya Oman ni Al Khadr Abdullah,
Muhammad al-Yafi, Fadel Hussein Saleh Hentif, Abd Al-Rahman Abdullah Au
Shabati na Mohammed Ahmed Salam. Mwenzao wa tano amepelekwa nchini
Estonia.
Kiasi ya watu 122 bado wangali katika gereza hilo la Guantanamo ,
linalotumiwa kuwaweka watu wanaoshukiwa kuhusika na ugaidi, kufuatia
mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 mjini New York na wengi wao
hawajashtakiwa. Wizara ya ulinzi ya Marekani imezishukuru Oman na Estonia kwa kuonyesha
ishara hiyo iliotajwa kuwa ni ya kiutu pamoja na moyo wa kuiunga mkono
Marekani katika juhudi za kulifunga gereza hilo la Guantanamo.
Republicans wataka kuzuwia kuachiwa kwa wafungwa
Hatua hiyo ya kuwahamishia wafungwa hao watano katika nchi hizo mbili,
imekuja siku moja tu baada ya wajumbe kadhaa wa chama cha Republican
katika Baraza la Seneti akiwemo Kelly Ayotte kutoka New Hampshire kutaka
paweko na sheria ya kuzuwia kuachiwa kwao wakisema bado ni hatari kwa
Marekani na washirika wake. Rais Barack Obama ameahidi kulifunga gereza hilo ,linalolaaniwa
kimataifa na ambalo lilifunguliwa mwaka 2002, katika kampeni ya Marekani
dhidi ya ugaidi. Juhudi zake zimekwamishwa na wabunge akiwemo Seneta
John McCain anayeupinga mpango huo. McCain, Mrepublican aliyekuwa mpinzani wa Obama katika Uchaguzi wa Rais
mwaka 2008 alisema wiki iliopita kwamba, asilimia 30 ya wafungwa
walioachiwa kutoka katika gereza hilo wamerejea katika mapambano dhidi
ya Marekani.
Msimamo wa Obama
Lakini hivi karibuni Rais Obama aliahidi kuharakisha juhudi za kulifunga
gereza la Guantanamo na utawala wake ukawahamisha wafungwa 28 mwaka
jana. Mjumbe wa Rais huyo aliyehusika na zoezi la kuachiwa huru wafungwa hao
Cliff Sloan alijiuzulu mwezi Desemba baada ya kuripotiwa kwamba
amevunjika moyo na jinsi wizara ya ulinzi inavyochelewa kuidhinishwa
kuachiwa wafungwa na kupelekwa nchi nyengine. Miongoni mwa wafungwa 122 waliobakia baada ya watano kupelekwa Oman na
Estonia jana, imethibitishwa kuwa 44 wakiwemo raia wa Yemen wameonekana
wanaweza kupelekwa nchi nyengine, wakati waliobakia wanatajwa kuwa ni
hatari kuachiwa huru. Mashirika ya haki za binaadamu yamelitaja gereza la Guantanamo kuwa "
Shimo jeusi," ambalo wafungwa husota kwa miaka mingi bila ya kufikishwa
mahakamani.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment